Vitu vitatu navikumbuka siku Michuzi Blog ilipozaliwa. Kwanza ni kaka Ndesanjo Macha, aliyenilekeza na kunipa tips muhimu zote za kublog, aliponishangaza pale nilipomuuliza yeye anawakilisha chombo kipi katika mkutano huu wa Helsinki Conference? Aliposema yeye anajiwakilisha mwenyewe kupitia blog yake ya Jikomboe, ghafla nikawa macho kumchuzi kwa kutomuelewa. Haikuniiingia akilini ni vipi mtu anayeendesha blog aalikwe kwenye mkutano mkubwa kama huo.

Pili ni pale kaka Ndesanjo Macha aliponitahadharisha kwamba ukianza kublog ni sawa na kujiambukiza ugonjwa usiotibika. Yaani mtu unakuwa kama umeehuka na hufikilii jambo linguine zaidi ya kublog. Macho kumchuzi yakaja tena. Ilikuwa ngumu kumuamini kwamba haka ‘kaugonjwa ka kublog’ kakikuingia mwilini hakatoki. Sasa naamini maneno yake maana haipiti dakika bila kuwaza niwatumikie vipi wadau.

Tatu ni pale kaka Ndensanjo Macha aliponitahadharisha kuhusu comment moderation. Yaani hii ya kupitia maoni yote yanayotumwa na kuchuja yanayofaa kusomeka na yasiyofaa, kwa mujibu wa sera za blogu yako. Macho kumchuzi yakaja tena. Safari hii ni kwa sababu wakati huo sikuwahi kuwaza kwamba kuna wadau ambao kazi yao ni kutukana, kujeruhi hisia za watu na kuchafua hali ya hewa. Hakika sikuwa nimemuelewa hadi baada ya kuanza kupitia maoni takriban 3000 kwa siku. Nashukuru kwamba kazi hiyo, yenye lawama tele kutokana na baadhi ya wadau wachache kutaka kutema cheche zao kupitia Globu ya Jamii kujikuta wakikwama, wakisahau kwamba sera ya Globu ya Jamii iliyotanabaishwa kila unapotaka kutuma maoni ya 'Angalia usijeruhi hisia za mtu/watu' inabakia pale pale kwa nia njema hiyo hiyo, na si vinginevyo.

Mtu mwingine aliyenitia hamasa kuendeleza libeneka baada ya kuanzisha blog ni kaka yangu, rafiki yangu na mpiganaji mwenzangu, Fidelis Tungaraza, aka Mti Mkubwa, aka FIDE. Huyu bwana, ambaye anaishi Helsinki, finland, kwa miaka kibao sasa, alikuwa daima akinicharuta mimi na waandishi wenzangu kuwa hatuwatendei haki wadau wa ughaibuni, kwani habari na taswira za nyumbani walikuwa wanazipata kiduchu mno kiasi kwamba ilikuwa sawa na kusema hakuna.
Fide, ambaye kasomea sanaa na kuhitimu pale chuo cha sanaa Bagamoyo, na Mzalendo wa kufa ijapo swala la kutetea maslahi ya Tanzania na wananchi wake, ndiye aliyekuwa mtu  wa kwanza kusoma Globu ya Jamii na kuanza kuitangaza kwa nguvu zote kwa kila mdau wa ughaibNa suni; kwamba Michuzi kaingia katika anga ya Blogu. Na siku naondoka Helsinki alinipeleka Chelsea club ya mji huo na kunitambulisha kuwa nimeingia katika anga za blog. Siisahau siku hiyo.
Baada ya hapo, na kama wanavyosema wahenga wetu, kila kitu ni historia. Niliporejea Tanzania nikaanza kufuata maelekezo ya Fide, kwamba niachane na mikutano, makongamano, warsha na mengineyo, bali niwaletee mambo ya jamii. Na ni yeye Fide aliyenipa majina ya Globu ya Jamii na wadau.
Mwaka mmoja baadaye, yaani mwaka 2006, nikiwa jijini New york, nikapata barua pepe toka kwa muasisi wa Globu ya Jamii, kaka Ndesanjo Macha. Akanipa pongezi na pole kwa kuendelea kuteseka na ugonjwa wa Ku-blogu. Pia akanikumubusha kwamba comment moderation nisiache hata siku moja, kwani SERA ya blog inaimarisha blog husika kwa kuzingatia hayo.
Mambo kadhaa yalijiri kuitambulisha Michuzi Blog kwa jamii baada ya hapo. Na mambo hayo yote yaliibuka chini ya kichwa cha habari cha BREKING NYUUUUZZZZZZ……ambapo kila mara hii ilimaanisha kwamba habari na taswira hizi ni za kipekee, za sasa hivi na hakuna ambaye anazo zaidi yangu mimi.
Nachelea kutaja BREKING NYUUUZZZ ZZ zote kwa uhaba wa nafasi, lakini zile za kuuwawa kwa wapendwa wetu Marekani (Nkya na Mazula), Kifo cha Mh Amina Chifupa na kujiuzuru kwa Waziri mkuu  Mh Lowassa pamoja na kutajwa kwa baraza jipya la mawaziri ni baadhi tu ya habari moto ambazo Globu ya Jamii iliweza kuwa ya kwanza kutangazia ulimwengu kabla ya mtu yeyote ama chombo kingine cha habari.
Yooote hayo tisa; kumi ni hii imani na uaminifu ambayo Globu ya Jamii imejijengea kwa wadua katika miaka hii sita. Yaani hakuna hata siku moja ambayo imetokea habari iliyokanushwa ama kuripotiwa kwa makosa. Kwa hili nashukulu weledi wa timu yangu ambayo daima naiasa kufuata hatua zote muhimu katika tasnia ya habari, hasa kuuliza tena na tena na tena kabla ya kuchapisha habari. Na kuuliza huko ni kwa sehemu zote tatu. Yaani sehemu ilipotokea tukio, kuuliza mhusika na pia kuuliza upande rasmi ama wasemaji wakuu wa tukio husika.
Kama nilivyosema awali, mengine yote  ni historia. Itoshe tu kusema kwamba nitachukua muda mrefu kueleza kila kitu na nisiweze kueleza robo ya mambo yote. Kwa maelezo hayo naomba ruksa niishie hapa na kuwaomba wadau mbofye sehemu ya ‘KUMBUKUMBU’ na kurejea katika posti za nyuma na kuapata hisoria kamili ya Michuzi Blog. Kila kitu kipo hapo.
Mwisho naomba nisema kwamba Michuzi Blog aka Globu ya Jamii ni mtumishi wa wadau wote duniani. Haichagui wala haibagui, kwani atayetuzika hatumjui. Hivyo nawakaribisha wadau wote tusherehekee siku hii huku nikiwaambia kwamba wakati wa kutimiza miaka 10 (InshaAllah) kutakuwa na MichuziTV na MichuziRadio Online, ambazo ziko njiani hivi karibuni.
Pia napenda kuwahakikishiwa wadau wote kwamba jina la Globu ya Jamii litabakia hili hili la Michuzi Blog kutokana na ushauri wa wamiliki wa mtandao huu ambao ni wadau wote. Logo  uzionazo hapa kurasani zitakuwa zinatumika katika kutambulisha Globu ya Jamii katuka Libeneke mbalimbali.
Natoa shukrani kwa mdau aliyetoa wazo la kubadili jina ili Libeneke liwe la kimataifa, huku nikimhakikishia kwamba kuwa kimataifa sio lazima lugha iwe tofauti na Kiswahili, kwani tayari watu takriban milioni 400 wanazungumza lugha yetu ya Taifa ambao ndio walengwa wakuu.
Ahsanteni sana wadau kwa sapoti yenu katika muda wote huu na InshaAllah Mola akipenda na panapo majaaliwa MichuziTV na MichuziRadio Online itaibuka hivi karibuni humu humu ndani ya Globu ya Jamii kukuletea mambo kwa sauti na taswira zinazotembea. Tuombeane uzima tu.


Ni vigumu kumshukuru kila mtu aliyechangia mafanikio madogo haya ya Globu ya Jamii. Ila kwa uchache niwashukuru washauri, wachangiaji, walezi pamoja na timu nzima ya Michuzi Blog kwa kufanikisha haya yote. 


Nianzie kwa washauri wakuu ambao baadhi ni kama JK, kaka Jeff Msangi wa Bongo Celebrity, Profesa Mark Mwandosya na mama Lucy Mwandosya, Jacob Mwambegele, Freddy Macha, Da'Chemi Chemponda, Balozi Juma Mwapachu, Balozi Peter Kallaghe, Balozi Mwanaidi Sinare Maajar, Da' Maura Mwingira, kaka Charles Hilary, kaka Abubakar Liongo, kaka Abou Faraji, kaka Ayoub Mzee, Da' Flora Nducha, kaka Freddy Maro,  Dr Emmanuel Nchimbi, kaka Hilary Bujiku, Mh Zitto Kabwe, Mh. January Makamba, Mh John Mnyika, kaka Max Melo, Dr Prosper Mosha, Dr Blandina Kilama, Bi Ainde Ndanshau, Da' Teddy Mapunda, kaka Baraka Msiilwa, kaka Frank Eyembe, Da' Sporah  Njau, Da' Subi, Da' Jestina George, Da' Mishi Marshall, Kaka Imani Kajura, Da' June Warioba, kaka Assah Mwambene, kaka James Shang'a, Dr Ramadhani Dau, Dr Kashilila, Da' Suzan Mzee, Da'Mariam Mungula, kaka Beda Msimbe, Dr John Shoo, Sensei Rumaza  na Sensei Malekia,  kaka John Mashaka, Profesa John Mbele, Dr Hassan Mshinda, Da' Mindi Kasiga, Ras Makunja 'FFU', Da'Janeth Mtonyi, Mh Mohamed Dewji, kaka Azim Dewji, Da' Mwamvita Makamba, Da' Taggie Daisy Mwakawago, Kaka David Minja, kaka Ephraim Mafuru, kaka Wilna, Dr Faustine Ndugulile na wengineo kadhaa ambao ni wengi mno.


Pia niwashukuru wana Globu ya Jamii wakuu kina Christopher Makwaia 'MK', Francis Dande, Audax Mutiganzi, Woinde Shizza, Muhidin Amri, Othman na Ahmad Michuzi, John Nditi, Prosper Minja, David Owen, Dixon Busagaga, John Mashaka, Dr Hildebrad Shayo, Frank Kallaghe, Othman Mapara, Richard Mwaikenda, Fide Tungaraza, Maggid Mjengwa, Haki Ngowi, Gadna G Habash, Lady JD.


Nawashukuru sana sana sana kwa sapoti yenu. Mie sina cha kuwapa Ila Mola ndiye atayewazawadia kwa wema na ushirikiano wenu.

-MICHUZI
 Ankal akipongezwa na Ndesanjo Macha mara baada ya kufungua Michuzi Blog katika ukumbi wa Finlandia hall jijini Helsinki, Sweden, Septemba 8, 2005.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Happy Birthday Blog Ya Jamii. vital tool for our linkage across the globe.

    Mungu Ibariki Tanzania
    John Mashaka

    ReplyDelete
  2. http://mjengwa.blogspot.comSeptember 08, 2011

    Kaka Michuzi,
    Hakika ni Siku Kuu. Michuzi blog ni zaidi ya blogu. Ni sehemu yetu ya maisha. Unajua kaka, kuna tulio nyuma yako. Tunajifunza. HONGERA SANA!
    Maggid,
    Iringa.

    ReplyDelete
  3. Blog ilifunguliwa jijini helsinki finland na sio sweden kama ilivyoandikwa.Happy birthday

    ReplyDelete
  4. Nichukue fursa hii kukupongezeni kwa Blogi yetu ya Jamii kutimiza miaka 6 toka kuhasisiwa kwake.
    Pia, nikiwa mdau niliyeshauri maboresho ya jina la blogi yetu hapo juzi,nichukue nafasi hii kuwashukru wadau waliotoa maoni yao bila woga na kwa uwazi zaidi kwa mantiki ya kuiboresha blogi yetu hii ya jamii katika nyanja ya habari.
    Mwisho,napenda kuwashauri wamiliki wa blogi nyingine ndani na nje ya nchi,waige mfano wa kaka Issa na blogi ya jamii kwa ujumla ili kufikia malengo yao na malengo ya jamii kama ilivyokusudiwa kupitia tasnia ya habari.

    Mdau: Joachim Kulwa Junior.
    India.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...