Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi
Maiti zilizopatikana hadi sasa ni 192 na watu 601 wameokolewa wakiwa hai katika eneo la Nungwi mkoa wa Kaskazini Unguja kati ya watu 760 waliosajiliwa kusafiri na meli ya MV Spice Islander iliyokuwa ikielekea kisiwani Pemba jana usiku wa Septemba 9, 2011.
Baadhi ya Abiria walionusurika walisema kuwa abiria walijaa kupita kiasi katika Meli hiyo kongwe ya MV Spice Islander iliyokuwa ikielekea Pemba.
MV Spice Islander ilianzia safari yake kwenye Bandari ya Dar es Salaam ambapo iliondoka mchana wa Septemba 9, 2011 ikielekea Pemba kupitia Zanzibar.
Ingawa haijafahamika mara moja kuwa Dar es salaam iliondoka ikiwa na abiria wangapi na mizigo yenye tani ngapi, lakini meli hiyo ilitia nanga kwenye Bandari ya Zanzibar na kuondoka kuelekea Pemba usiku wa kuamkia Septemba 10, 2011 ikiwa na abiria 670 waliosajiriwa.
Mnamo majira ya saa 7.30 usiku meli hiyo ikiwa katika eneo la Nungwi mkoa wa kaskazini Unguja ilianza kupinduka polepole na hadi ilipofika saa 9.00 usiku meli hiyo ilipinduka na hatimaye kuzama kabisa kwa kuelemewa na mizigo pamoja na abiria.
Baadhi ya wananchi wameitupia lawama mamlaka ya bandari na Sumatra kwa kushindwa kudhibiti uchukuzi wa abiria na mizigo kupita kiasi.
Kazi ya utafutaji wa watu walio hai na uopoaji wa maiti bado unaendelea na vikosi vya Jeshi la Polisi wanamaji, KMKM na JKU wanaendelea na kazi hiyo.
Jeshi la Polisi limetuma timu ya wataalamu wa Upelelezi na Madaktaji pamoja na Meli moja ya uokoaji MV Mamba ikiwa na boti nyingine ndogondogo ziendazo kasi za msaada majiuni.
Serikali ya Zanzibar na ile ya Muungano kupitia marais JK na Dk. Shein wametangaza siku tatu za maombolezo kuanzia kesho Septemba 11, 2011 na bendera zote zitapepea nuzu mlingoti.
Hakutakuwa na sherehe zozote ama mikusanyiko yenye kuonyesha buurudani na michezo.
Mh. Zito Kabwe, yeye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA na Waziri Kivuli wa Fedha, alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa vyama vya Siasa waliofika katika viwanja vya Maisala mjini Zanzibar na kutoa Pole kwa wafiwa na kusema Chama chake kimesitisha kwa muda shughuli za kampeni katika jimbo la Igunga mkoani Tabora kutokana na msiba huo mzito.
Hiyo ni meli ya pili kuzama baharini ikiwa safarini kuelekea Pemba na meli ya kwanza ilikuwa ni MV Fatahi iliyozama mwaka jana 2010 ikiwa Bandari ya Zanzibar ikielekea Pemba.
Meli nyingine mbili ziliungua moto zikiwa bandarini Zanzibar na meli nyingine ya MV El- Salaam ilizama Baharini ikiwa na bidhaa mbalimbali ikielekea Songosongo Kilwa kwenye utafiti wa mafuta.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Jamani hizi mamba watu wanaziangalia kabla ya kuzitoa. Mara tunaambiwa watu 760. Kati ya hao maiti zilizopatikana mpaka sasa 192 na waliokolewa wazima ni 601. ukijumlisha kwa upesi jumla mpaka hapo ni 793 na sio 670 au 760 ambao tunaambiwa wamesajiliwa. Taarifa zone zinatupa number mbili tofauti za waliosajiliwa 670 na 760 ipi ni ipi maana zote zinapitwa na jumla za watu waliiookolewa na kufariki. Naomba tuwe makini katika kuripoti na sio kuficha au kuripoti uongo kuficha makali.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...