Na Salama Juma - Maelezo
Maadhimisho ya siku ya Tiba Asili ya Mwafrika yanatarajia kufanyika kitaifa tarehe 09 hadi 13 mwezi huu katika viwanja vya Mwembeyanga wilayani Temeke jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Kitengo cha Elimu, Habari na Mawasiliano kwa Umma imesema kuwa Serikali itaendelea na urasimishaji wa tiba asili wenye lengo la kuboresha tiba hiyo hapa nchini.
“Kupitia urasimishaji dawa za tiba asili zikifanyiwa utafiti unaokidhi viwango zinaweza kutumika kutibu magonjwa mbalimbali na hata kuuzwa nje ya nchi kama nchi nyingine zinavyofanya.
Kwa kuwa Tanzania ni moja ya nchi za kitropiki na mazingira yake hayajachafuliwa sana, dawa zetu bado zina ubora unaokubalika kwa matumizi ya binadamu”, ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha waganga na Wakunga wa tiba asili wametakiwa kushirikiana kwa dhati na Serikali katika kurasimisha tiba hiyo na kuifanyia utafiti ili kuboresha tiba na dawa zitumikazo.
Maadhimisho hayo ambayo ni ya tisa hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha uendelezaji na uboreshaji wa tiba asili katika nchi za Kiafrika huku kwa mwaka huu yakiwa yamebeba Kaulimbiu isemayo “Hifadhi mitidawa: urithi wa Mwafrika’’.
Kutokana na kauli mbiu hiyo kila mmoja anapaswa kuwa askari wa kuyalinda maeneo yenye uoto wa asili na miti dawa ili kuboresha na kuendeleza tiba asili nchini.
Nashauri babu Loliondo awe mgeni rasmi.
ReplyDelete