Mwenyekiti wa umoja wa madereva wa magari makubwa kanda ya kaskazini,Rashid Salehe (katikati) akihutubia kwenye mkutano wa madareva wa magari makubwa uliofanyika katika shule ya msingi mwangaza,Ngarenaro mjini Arusha,kulia ni katibu wa umoja huo mkoa wa kilimanjaro,Shaban Ramadhani na kushoto ni mwenyekiti wake kutoka mkoa huo wa kilimanjaro Apolinary Mallya.
Baadhi ya madereva wa magari makubwa mkoa wa Arusha, wakiwa kwenye kikao wakisikiliza hoja mbalimbali kutoka kwa viongozi wao.picha na Woinde Shizza,Arusha.

Na Woinde Shizza,Arusha

UMOJA wa madereva wa magari makubwa mkoa wa Arusha umeungana na wenzao wa Tunduma kwa kuandaa mgomo wa nchi nzima baada ya tarehe 30 mwezi huu iwapo serikali itashindwa kutoa ufumbuzi na mustakabari wa madai yao.

Akizungumza kwenye kikao cha pamoja cha madereva hao ,kilichoandaliwa mahususi kwa ajili ya kujiweka tayari na mgomo huo,kilichofanyika katika shule ya msingi Mwangaza, Ngarenaro mjini hapa,mwenyekiti wa kanda wa Umoja huo,Rashidi Salehe,alisema kuwa mgomo huo wa nchi nzima hautakuwa na kikomo,kwani wamevumilia muda mrefu manyanyaso kutoka kwa matajiri wao.

Aidha alisema kuwa sababu kubwa ya kufanya mgomo huo ni kuishinikiza serikali iwabane waajiri wao ili watambue mikataba yao ya kazi,ajira,posho za kujikimu wanaposafiri nje ya nchi wakitaka walipwe kwa dola badala ya shilingi za kitanzania ,fedha ambayo walidai wanapofika nchi nyingine na kuibadilisha huwa fedha kidogo.

Madai mengine ni kupunjwa kwa posho za kutoka mkoa mmoja kwenye mkoa mwingine ambapo walidai kwamba wamekuwa wakilipwa shilingi 20,000 hadi elfu 25 kwa siku,badala ya shilingi 65,000 na posho ya kwenda nje ya nchi wanataka ilipwe dola 76 kwa siku.

‘’sisi madereva lazima tuwe na umoja ,hatuwezi kukubali kuendelea kunyanyaswa na waajiri wetu kila siku,lazima awamu hii kieleweke tushikamane mpaka tuzijue haki zetu,na ifikapo tarehe 30 kama serikali itakaa kimya ,tarehe 31 hakuna dereva kugusa gari’’alisema Salahe.

Alifafanua kwamba madereva hao wamekuwa wakikumbana na kadhia ya kunyanyashwa na kufukuzwa ovyo na waajiri wao ikiwa ni pamoja na kutolipwa kabisa mishahara na kuishia kulipwa posho tu.

‘’dereva akibahatika kulipwa mshahara basi lazima ukumbane na makato mbalimbali ikiwemo,kuambiwa uliiba mafuta,umepasua tairi ,umevunja spiringi na kujikuta ukiambulia patupu na mara nyingi unafukuzwa kama mbwa na anaitwa dereva mwingine anakabidhiwa gari hiyo’’alisema

Nae mwenyekiti wa umoja wa madereva mkoa wa Kilimanjaro,Apolinary Mallya aliwataka madereva hao kujenga umoja madhubuti utakao wasaidia kudai na kupata haki zao za msingi bila kuleta vurugu wala maandamano.

Hata hivyo aliwataka madareva hao kupunguza anasa wanapokuwa wamekabidhiwa gari kwani wengi wao wamekuwa wakichangia uzembe na kuongezeka kwa ajali,ambapo alidai baadhi ya madereva wamekuwa wakiendekeza pombe na kushindwa kulimudu gari kutokana na ulevi wa kupindukia.

Pia aliwaonya Madereva wenzake hao kuacha kushiriki ngono wawapo safarini kwani hali hiyo imekuwa ikiwasababishia uchovu na kujikuta wakisinzia wanapokuwa wakiendesha gari hali ambayo imekuwa ikiongeza ajali za barabarani.

Mallya alikemea kitendo cha baadhi ya madereva hao kushinda wamekaa kwenye mageti ya makapuni wakivizia kazi,na kudai kwamba , hatua hiyo imekuwa ikishusha hadhi na heshima ya madareva hao,kwani hata mwajiri hawezi kuwathamini na kuwapa haki zao, kwani mwajiri anaamini akiacha kazi mmoja ,wapo wengi hapo nje wanasubiri kazi hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Madai yao ya kipato na mafao ni ya msingi na niawaunga mkono kwa hilo. Nawapongeza sana kwa kuanza umoja wa kudai haki zenu. Lakini, nilidhani wangeiomba serikali ikazanie usalama barabarani na mafunzo kwao wote. Hawa madereva hawajali sana usalama wao binafsi, magari yao na watumia barabara wengine. Ninadhani wangetilia mkazo suala la mafunzo ya udereva. Udereva kama proffesion usiishie kujua kuendesha gari tu, ni lazima uendeane na kujua miiko ya barabarani. Lazima ujue kuwa hilo gari ni ofisi yako likiharibika huna ofisi, hivyo tunza gari, jua kuwa una dhamana ya maisha yako na maisha ya watu wengine hivyo endesha kistaarabu. Kawia Ufike

    ReplyDelete
  2. Wawache na kuvuta bangi na kujiona wao ndio wafalme wa barabarani kwani wana dharau sana kwa magari madogo wanapokuwa wanaendesha barabarani.

    Vile vile wajitahidi kuendesha magari yaliyo mazima, hayo magari yanayopata ajali na kuvunjika kama chungu cha udongo basi tena hapa nchini.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...