Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar

ZANZIBAR JUMATATU SEPTEMBA 19, 2011. Watuhumiwa watatu kati ya wanne waliofikishwa kwenye Mahakama Kuu Mjini Zanzibar wiki iliyopita wakikabiliwa na kosa la uzembe na kusababisha vifo vya watu 203 waliokuwa wakisafiri kwa Meli ya MV Spice Islander na kuzama katika bahari ya Hindi, Septemba 10 2011, wamepewa dhana na haikutaja siku ya kurejea tena Mahakamani hapo.

Watuhumiwa waliopewa dhamana ni Abdallah Mohammed Ali(30) mkazi wa Bububu, ambaye ni Afisa Mkuu wa Meli ya MV Spice Islander, Yussuf Suleiman Jussa(47), mkazi wa Kikwajuni ambaye pia ni Mmoja wa Wamiliki wa Meli na Msimamizi Mkuu wa Mizigo katika meli hiyo na Simai Nyange Simai(27) mkazi wa Mkele, ambaye ni Mfanyakazi wa Mamlaka ya Mamlaka ya Usafiri Baharini anayehusika na usalama wa abiria melini.

Watuhumiwa hao, Ijumaa iliyopita walirejeshwa rumande baada ya kuzuka mabishano ya kisheria ya kutaka wapewe dhama ama wasipewe, ambapo Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar Mh. George Kazi, aliamuru warejeshwe rumande hadi leo Jumatatu atakapotoa uwamuzi wake.

Walipofikishwa Mahakamani hapo hii leo, Wakili wa Utetezi Bw. Hamidi Ali Saidi Mbwezeleni aliiomba Mahakama iwaachie huru watuhumiwa hao ili tume iliyoteuliwa na Rais kuchunguza chanzo cha kuzama kwa meli hiyo iendelee na kazi yake la sivyo tume isitishe kazi yake hadi pale kesi itakapomalizika.

Wakili huyo amesema kuwa kutakuwa na utata kama watuhumiwa wataendelea kubaki rumande kwani watakosa haki yao ya msingi katika tume iliyoundwa na Rais wa Zanzibar wakati ikiendelea na kazi yake endepo itataka kupata taarifa ama maoni kutoka kwa watuhumiwa hao hivyo wakiwa mahabusu watakosa haki yao ya kujieleza mbele ya tume hiyo.

Amesema hivi sasa inaonekana kuna makundi mawili yanayofanya kazi moja kwa maana ya Mahakama na Tume jambo ambalo alisema litakuwa na utata na lenye makusudio ya kuwalinda baadhi ya watu fulani.

Hata hivyo, ingawa Mwanasheria wa Serikali Ramadhani Ali Nassib alitetea uwamuzi wa kutaka watuhumiwa hao wabaki rumande wakati tume ikiendelea na kazi yake lakini Mh. Kazi alikubaliana na hoja ya upande wa utetezi na kuamuru watuhumiwa hao wawe nje kwa dhamana hadi pale tume ya Rais itakapomaliza kazi yake.

Watuhumiwa wote watatu walipewa dhamana ya maandishi ya shilingi milioni kumi na wadhamini wawili kila mmoja kwa kiasi hichohicho na watuhumiwa hao waliondoka huku mtuhumiwa wa kwanza katika kesi hiyo Saidi Abdallah Kinyanyite(58) ambaye alikuwa Nahodha wa Meli ya Spice Islander akiendelea kusakwa na Polisi.

Ijumaa iliyopita watuhumiwa hao walifikishwa Mahakamani na kusomewa shitaka la uzembe wa kusababisha vifo kwa watu 203 waliokuwa kwenye Meli hiyo na Mh. Kazi alisema hataki kukurupuka kutoa dhamana kwa vile kesi hiyo ina unyeti wake.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Waandishi mnatuzingua kuna siku mlisema nahodha wa meli aeleza tukio lilivo kua,mlidai yupo hosptl,leo anatafutwa,mbona mnazinguaWaandishi mnatuzingua kuna siku mlisema nahodha wa meli aeleza tukio lilivo kua,mlidai yupo hosptl,leo anatafutwa,mbona mnazingua

    ReplyDelete
  2. Yaheee...hii imebonezwa kizenji...watu wamepoteza maisha na ushahidi upo! au mpka meli ipatikane na nahodha wake!

    ReplyDelete
  3. Ina maana hiyo tume ya uchunguzi hata ikichukua miaka minne hao watu watakua nje wanapeta tu na kula maisha na familia zao? Jamani tumwogope Mungu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...