![]() |
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Mh. Hamad Masoud Hamadi |
Na Nafisa Madai - Maelezo,Zanzibar
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Hamad Masoud Hamadi amesema wakati umefika sasa kwa madereva na matingo kuwa na mikataba maalumu ili iweze kuwalinda katika kazi zao za kila siku.
Amesema hayo alipokua akifungua Kongamano la kuanzimisha wiki ya kimataifa ya wafanyakazi wa sekta ya usafiri kwa njia ya barabara huko katika ukumbi wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo Kikwajuni Zanzibar
Waziri Masoud amesema si wakati tena huu kwa Utingo na Madereva wa daladala na taxi kufanya kazi kwa kubahatisha kwani nao wanapaswa kisheria kufanyiwa mikataba ya kazi kwa vile wanategemewa na familia zao.
Aidha amesema kutokana na umuhimu wa mikataba ya kazi wizara yake italishughulikia suala la madereva na Utingo wa daladala kuwa na Mikataba ya ajira ili kuwa na uhakika wa kazi wanayoifanya.
Aidha alisema mikataba hiyo itawawezesha madereva hao na Utingo kupata mapumziko na kufanya kazi kwa mujibu wa kufuata sheria za kazi na kusaidia kupunguza uchovu na kuondosha ajali barabarani za mara kwa mara.
Hata hivyo alisema wizara yake pia itachukua juhudi ya kuimarisha ofisi ya ukakuzi wa magari kwa kuipatia vifaa vya kisasa vya ukaguzi wa magari ili iweze kuendana na teknolojia mpya inayokwenda sambamba duniani kote.
Waziri Masoud amesema utaratibu maalum unaandaliwa na wizara wa kutoa mafunzo ya kutosha kwa Utingo na madereva ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Hata hivyo amesema wizara itaimarisha alama za barabarani, taa,sehemu za kuegesha magari na kusimamia vituo kwa uhakika ili kupunguza misongamano isiyo ya lazima.
Waziri Masoud aliwataka madereva kuacha kutumia lugha chafu, dharau na kejeli na kuondosha gari kabla abiria hajakaa kwenye kiti hali ambayo imekua ikilalamikiwa sana na abiria.
Kwa upande wake katibu mkuu wa chama cha wafanyakazi wa sekta hiyo Muhamedi Ali Salum amesema chama chao kinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa mikataba jambo ambalo limekua likiwarejesha nyuma kimaendeleo.
Hata hivyo alisema kutokuwa na mikataba ya kazi kwa madereva hao na Utingo ndiko kunakosababisha kufanya kazi kinyume na sheria za barabara na kusababisha ajali za mara kwa mara.
Aidha amesema lengo la kufanya kongamano hilo ni kuweza kupata fursa ya kukaa pamoja kama wadau kutafakari na kujadiliana namna ya kutafuta mbinu mbadala za kutatua matatizo yanayoikabili katika sekta hiyo.
Kongamano hilo limewashirikisha wadau mbalimbali kupitia jumuia zao wakiwemo madereva, Utingo wa magari yote ya abiria yakiwemo daladala na taxi ambapo ujumbe wa mwaka huu kimataifa ni “Usalama Sasa” (SAFETY NOW) .
Mkataba wa dereva na konda utawaumiza mwenye daladala. Daladala ikiwa nzima itafanya kazi malipo ya dereva na konda yatapatikana. Daladala ikiwa mbovu italala, hakuna mshahara lakini mkataba hauelewe haya. Business model ya biashara ndogo ndogo kama za daladala ni kusaidiana kati ya mmiliki na dereva na konda wake.
ReplyDeleteMkataba utaweza kuwabana madereva na wamiliki wa magari pindi kunapotokea ajali,mara nyingi kunapotokea ajali za uzembe madereza hukimbia na serikali inashindwa kuwakamata madereva hao.
ReplyDeleteMtindo wa kupeana gari ovyo ovyo utasaidia kwa mmiliki wa gari kufanhamu nani alimkabizi gari yake,hata trafic police kufahamu dereva mahasusi wa gari wakati atakaposimamisha.
Jengine itakuwa njia nzuri kuwatetea wafanyakazi wa daladala hasa katika mishahara yao,waziri unawajibu wa kuwaekea kinga juu ya hilo,ili madereva na tingo kuoweza kupata haki zao za msingi,ikiwa mmiliki tashindwa kuliendesha gari gari lake au biashara yake,atalika kwake na kutoa report.
Kama watu binafsi watashindwa kuendesha biashara ya dala dala,ningeshauri serikali ya mapinduzi ya zanzibar kutoa biashara hii kwa muekezaji mmoja tu,ambae ataendesha daladala zote unguja,na pemba halkadhalika. hii itasaidia katika kuweka usalalama wa abiria au wananchi.