Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Mahadhi Juma Maalim (MB) akichangia majadiliano  katika Mkutano wa Kamati ya Kwanza na Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa kuhusu silaha za kawaida ( Conventional  Weapons) zikiwamo silaha ndogo ndogo na nyepesi Mkutano huo unafanyika  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.  Aliye kaa nyuma yake ni Balozi  Mohamed Hamza, Mkurugenzi wa Idara ya  Mambo ya Nje  Zanzibar


Na Mwandishi Maalum
New York

            Wakati   Jumuia ya Kimataifa ikiendelea  kujadialiana, kuvutana na kutokufikia maamuzi ya msingi na madhubuti kuhusu udhibiti wa  biashara na matumizi haramu ya silaha ndogo ndogo na nyepesi pamoja na silaha  za maangamizi. Maisha ya Mamia ya wanawake, watoto na wanaume yanaendelea kupotea.  

Kwa takribani  siku tatu mfululizo wiki hii, wajumbe wa  Kamati ya Kwanza ya Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, wamekuwa katika majadialiano yaliyoambatana  na upitishaji wa rasimu za maazimio  matatu yanayolenga  pamoja na mambo mengine. Kutafuta njia muafaka za kudhibiti, kupunguza na kuratibu biashara ya silaha ndogo ndogo na nyepesi, silaha za maangamizi zikiwamo za kibaiolojia pamoja na mabomu ya ardhini,   matumizi yake na ulimbikizaji wa silaha  hizo.

Karibu kila mjumbe aliyechangia majadiliano hayo, amekuwa akielezea kwa hisia kali  namna ambavyo  usambaaji wa  silaha hizo na matumizi yasiyosahihi yameendelea kuziweka   nchi  nyingi na raia wake katika hali tete huku pia zikihatarisha uchumi na maendeleo endelevu ya nchi hizo.

Baadhi ya wajumbe walifikia hatua ya kutamka bayana  kwamba,  je  Umoja wa Mataifa  ulikuwa unahitaji maazimio mangapi yapitishwe   ili itambue kwamba  ulimbikizaji ,usambazaji, uuzaji na matumizi haramu ya silaha hizo sasa  kunahitaji maamuzi madhubuti  ili kunusuru maisha ya watu hasa wale wasiokuwa na hatia.

Akichangia majadiliano hayo, Naibu Waziri wa  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Mahadhi Juma Maalim ( Mb), amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba,  matarajio ya nchi  yake (Tanzania)  ni kutoendelea kushuhudia maisha ya watu wasio na hatia yakiendelea kupotea   kwa sababu tu dunia imeshindwa kufikia makubaliano juu ya  kudhibiti    matumizi  haramu ya silaha hizo.

 Ni jambo lililowazi, na hata jumuia ya kimataifa mmekuwa mashahidi,wananchi wetu na wale za nchi jirani kila siku wanaendelea kupoteza maisha kutokana na  matumizi  mabaya ya silaha hizi. Nchi yangu isingepeda kuendelea kuona maisha ya watu wasio na hatia yanaendelea kupotea” akasema.

Aidha Naibu Waziri amesema  tamaa ya madaraka,  umaskini na ubinyaji wa   misingi ya uhuru na haki mara nyingi vimekuwa chanzo cha matumzi mabaya ya silaha zikiwamo silaha ndogo ndogo na nyepesi.

Mhe. Mahadhi Juma Maalim akasema kuwa  ingawa Umoja wa Mataifa,  Umoja wa Afrika na Jumuia za Kikanda zimetumia raslimali nyingi kujaribu kulitafutia ufumbuzi tatizo la kuzagaa kwa silaha, bado ufumbuzi madhubuti haujapatikana na  dunia imeendelea kushuhudia matukio ya kutisha.

Akasema ni kwa sababu hiyo, Tanzania inaungana na  mataifa mengine katika kusisitiza kwamba  Jumuia ya Kimataifa inatakiwa kuungana na kushirikiana ili kulimaliza tatizo la ulimbikizaji, usambazaji na matumizi haramu ya silaha zaina zote zikiwamo  ndogo ndogo na nyepesi.

Amesisitiza kwa kusema kwamba Wajumbe wa Kamati hiyo ya Kwanza ambayo  jukumu lake kubwa pamoja na mambo mengine ni kusimamia masuala ya amani na usalamana , upokonyaji wa silaha,washirikiane   ili  dunia iwe mahali salama pa kuishi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Wakati wa    Mkutano huo, baadhi ya wazungumzaji wengi wao kutoka nchi za Afrika, Latini ya Amerika na  Visiwa vya Carribian walitoa wito wa kutaka nchi zilizoendelea kudhibiti uzalishaji na uuzaji wa silaha hizo ambazo mwisho wa yote huishia katika nchi zinazoendelea.

Aidha wazungumzaji wengine wengi  hasa wale wa kutoka nchi za  Afrika, wameiomba jumuia ya kimataifa  na nchi zilizoendelea  kuzisaidia nchi za  Afrika katika mchakato wa ukusanyaji na uangamizaji wa silaha haramu hasa zile ndogo ndogo na nyepesi  silaha ambazo zimezagaa sana barani Afrika.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...