NA MARZOUK KHAMIS-MAELEZO PEMBA
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana CCM Mkoa wa Kusini Pemba Ali Suleiman Juma amesema kazi kubwa inayowakabili Viongozi wa Jumuiya za Chama Cha Mapinduzi hivi sasa ni kuyafufua Madarasa ya Itikadi ya chama katika ngazi za Matawi na Majimbo ili kuimarisha uhai wa chama.
Ali Suleiman ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Tekelezaji ya Vijana Taifa ameyasema hayo katika Tawi la CCM Matale alipokuwa akizungumza na Viongozi na wanachama wa tawi hilo ikiwa ni ziara yake ya kuimarisha uhai wa chama na jumuia zake katika Jimbo la Chonga.
Amesema kutoendelea kwa madarasa hayo katika ngazi za Matawi na Majimbo kunawavunja moyo vijana wengi ambao ni tegemeo katika chama cha Mapinduzi na Jumuiya zake.
Suleiman amefahamisha kuwa Mchango wa kuwepo kwa madarasa hayo katika uimarishaji wa shughuli za Chama ni mkubwa mno kwani kunawakutanisha vijana na kuwapa fursa katika kuchangia masuala mbali mbali yanayowahusu.
Aidha amesema iwapo vijana watapatiwa mafunzo hayo katika ngazi husika ni dhahiri kuwa watahamasika kujiunga na jumuia za chama pamoja na kushiriki katika nafasi mbali mbali za uongozi katika Chama.
Akizunumzia kuhusu suala la ajira kwa Vijana amesema kuwa hivi sasa ni vigumu kwa serikali kuwapatia ajira vijana wote,lakini hata hivyo serikali inajitahidi kutafuta kila njia kuona kuwa vijana wanawezeshwa kwa kupatiwa mikopo kupitia vikundi vyao vya ushirika.
Amesema Chama cha Mapinduzi kupitia Jumuiya ya Umoja wa Vijana Tanzania imeandaa mpango wa kufungua Benki za mikopo zitakazotoa mikopo kwa viajana kupitia vikundi vya ushirika hivyo aliwataka vijana kuanzisha vikundi vya ushirika katika matawi ili waweze kufaidika na mikopo hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...