![]() |
Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo,Zanzibar Mh. Abdilah Jihad Hassan |
Na Hamad Hija-Maelezo Zanzibar
WAZIRI wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Abdilah Jihad Hassan amesema kuwa Sekta ya Utalii Nchini mbali ya kuwapatia ajira Wazanzibar walio wengi lakini pia sekta hiyo imekuwa ikichangia asilimia 20 ya pato la Taifa Nchini.
Alisema kuwa Sekta ya utalii ndio inayochangia maendeleo kwa kiasi kikubwa kwa vile mbali ya kutowa ajira kwa vijana hapa Zanzibar imekuwa ikichangia kwa asilimia 80 fedha za kigeni ambazo hutumika katika masuala mbali mbali ya kimaendeleo.
Alisema Waziri Jihad kuwa kila sekta ina nafasi yake kubwa katika kuchangia kila Nyanja lakini sekta hii ya utalii imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika kuchangia masuala mengi yakiwemo ya kijamii na ya kiuchumi ambapo sekta hii imekuwa ikitowa mchango mkubwa katika masuala ya uajiri kwa ujumla.
Jihad aliyasema hayo leo katika hotel ya Bwawani mjini zanzibar ndani ya ukumbi wa Salama Hall katika mkutano wa baraza la sita la biashara la zanzibar wakati akitoa ufafanuzi juu ya suala la utalii hapa Zanzibar.
Alibainisha kwa kusema kwamba Zanzibar imekuwa kivutio kikubwa cha utalii na kila mwaka imekuwa ikipokea jumla ya watalii 145,000 kutoka Nchi mbali mbali duniani ambapo Italy ndio Nchi ambayo Watalii huja kwa wingi kutoka Nchi hiyo.
Amesema kuwa kufurika kwa watalii kila mwaka kuja hapa zanzibar lengo lao kubwa sio tu kutembea lakini lengo kuu la watalii hao ni kuja kusoma mambo mbali mbali yakiwemo ya historia ya Nchi yetu pamoja na mazingira yetu kwa ujumla.
Alifahamisha kuwa pamoja na kupokea idadi hiyo ya watalii ambao hutembelea nchi yetu hii,suala la usalama ndio tiketi ya kuendelea kupokea watalii hao ambapo Mtalii hujali suala la usalama tu na sehemu ambayo haina usalama mtalii haipendelei sana.
Amesema tukiendelea na usalama katika nchi hii kama ulivyo kwa sasa, utalii wetu utaendelea kustawi na maendeleo yatapatikana ikiwa ni pamoja na masuala ya ajira ambayoyanapatikana nchini katika nafasi mbali mbali na sehemu mbali mbali.
Kwa upande mwengine Wadau waliohudhuria katika mkutano huo wa sita wa Baraza la Biashara la Zanzibar walisema kuwa mapato katika sekta hiyo yamekuwa yakivuja kwa asilimia 40 na hii inatokana na kwamba safari ya mtalii inakuwa inatayarishwa kutoka huko wanakotoka lakini kama kutakuwa na mabadiliko katika hali hii mapato yanaweza kuongezeka hadi asilimia 70.
Katika kupunguza kuvuja kwa mapato hayo walishauri kuwa Zanzibar iwe na shirika lake la ndege jambo ambalo limetajwa kuwa gumu kwa hivi sasa ambapo imeelezwa ni vigumu kuwa na shirika lakini wawekezaji wanaweza kuja kuwekeza kwa ajili ya kuanzisha safari za ndege.
Hebu kuweni wawazi zimeingia kiasi gani kutoka sekta ya utalii na sio idadi ya watalii walioingia. Au mnachakachua mapato kwani hatuoni maendeleo yoyote labda kuathirika kwa mila na desturi ya Wazanzibari.
ReplyDelete