Ndugu Zangu,

Ninavyoandika mjadala wa sheria ya marejeo ya Katiba kwa mwaka 2011 unajadiliwa bungeni Dodoma. Utamalizika Jumatano ya keshokutwa. Ni saa 72 za ama matumani au huzuni kwa WaTanzania. Yote mawili yatategemea sana na Wabunge wa CCM ambao kwa wingi wao, wanaweza kuupitisha muswaada au kuukataa.

Itakuwa ni tumaini kwa Watanzania kama Wabunge wataukataa muswaada huo, na kinyume chake. Kama wataupitisha.

Na wabunge wa CCM wakiupitisha, basi, tumaini la mwisho kwa WaTanzania litabaki kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Yeye ndiye mwenye ’ Kura ya Veto’. Ana uwezo wa kuamua kusaini au kutosaini muswaada huo.

Jana niliangalia kipindi cha TBC1 kuhusu semina ya Wabunge juu ya mchakato wa Katiba. Nikiri, mara kipindi kile kilipomalizika, nami nilitingisha kichwa kwa masikitiko. Niliziona ishara za njia mbaya tunayokwenda kupitishwa.

Kwa mtazamo wangu, Maprofesa waendesha semina wale wawili; Profesa Palamagamba Kabudi na mwenzake Haule walionekana zaidi kwa sura ya ‘ ukada’ kuliko utaaluma na uanazuoni hivyo basi, kuthibitisha kauli ya Profesa Shivji anayesema mchakato huu wa Katiba umekosa uhalali na hofu yake ya Rais kupewa mamlaka makubwa.

Mbunge David Kafulila ( NCCR- Mageuzi) naye alisema kile ambacho ndicho kitakachofanya mchakato huu uwe wa gharama kubwa bila matunda tarajiwa kwa umma. Kafulila amezungumzia juu ya IMANI ya umma kwa mchakato mzima akimrejea Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki- Moon aliyesema , kuwa tatizo kubwa la Serikali nyingi si nakisi ya bajeti bali nakisi ya imani ya Wananchi kwa Serikali hizo. Ndio, kupungua kwa imani.

Tuwe wakweli kwa nchi yetu. Nionavyo, Sheria ya kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya itakayojadiliwa na kupitishwa na wabunge walio wengi wa chama tawala ndani ya saa 72 ikitanguliwa na semina ya siku moja ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano ambao hawakujaza ukumbi wa Msekwa kamwe haiwezi kutuacha salama kama taifa.

Na hofu hiyo imeelezwa pia na Chama Cha Wanasheria wa Tanzania bara katika taarifa yao ya jana. Wanazuoni wetu hawa wa sheria wameweka wazi, kuwa si sahihi kwa muswaada huo kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu. Unawanyima wananchi wengi fursa ya kushiriki kuujadili. Wanazuoni wetu wanasema kinachotakiwa kutungiwa sheria ni Mchakato wa Maandalizi. Na kwa DHATI kabisa, wamesema, hata kama Wabunge watapitisha muswaada huu wa mchakato, basi, wamemshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano asiusaini muswaada huo.

Na jana ile Profesa Kabudi alisema; ” Katiba si Muharobaini”. Wengine sisi hata kama hatuna shahada za udaktari wa falsafa lakini tunauona ukweli pia, kuwa tunachohitaji ni mzizi wa muharobaini. Kwamba yumkini Katiba kwetu yaweza kuwa mzizi wa muharobaini.

Profesa Kabudi anasema pia, ” What we are doing is Constutional building and not Constutional making”. Kwamba tunachokifanya ni Ujenzi wa Katiba na si Kutengeneza Katiba.

Swali kwa anachokisema Profesa ni je; “ Ni kina nani wanaostahili kushirikishwa kwenye maandalizi ya ujenzi huo?”. Ndipo hapa hoja ya Profesa Shivji inapokuwa na mashiko pale anaposema huenda mchakato mzima umekosa uhalali.

Ndio, kinachojionyesha ni hiki; tunajenga nyumba moja lakini tunagombania fito. Na kibaya zaidi, tumefikia mahali pa kuchagua nani wa kuchangia fito kwenye ujenzi wa nyumba yetu. Hivyo basi, kubagua. Ni dhambi kubwa.

Na muswaada huu ukipitishwa utakuwa na maana hii; kumruhusu Rais kuanzisha mchakato kwa kuwateua wajumbe wa Kamati itakayoratibu mchakato , kuwateua wabunge 116 wa Bunge la Katiba. Wabunge hao wakiletewa mapendekezo ya Katiba Mpya wataijadili na hatimaye kuipitisha au la. Wakiipitisha itapelekwa kwa wananchi kupigiwa kura. Na kura za ndio zikitosha itakuwa na maana ya Katiba hiyo mpya kupata uhalali na kuanza kutumika.

Na tafsiri kuu hapa ni hii; Watanzania tutakuwa tumepewa Katiba Mpya tunayoililia chini ya saa 100. Na lifuatalo nina hakika nalo, kuwa Watanzania HATUTARIDHIKA nayo. Kwanini?

Nilipata kuandika kupitia safu yangu kwenye Raia Mwema, kuwa; ” Nauona, mwelekeo mbaya wa upepo wa kisiasa nchini mwetu. Nina shaka kubwa. Naamini, tuko wengi wenye mashaka na mwelekeo wa nchi yetu tunayoipenda.” ( Mraba Wa Maggid, Raia Mwema, Aprili 6, 2011 )

Kwenye makala yangu ile niliweka wazi, kuwa katika hili la mchakato wa kupata Katiba Mpya tumeanza na mguu mbaya. Tumeyaona Dodoma na Dar es Salaam . Sikuhitaji kuwa na Elimu ya Unajimu kubaini hilo. Tulishaziona ishara.

Hakika, ikitaka, Serikali inaweza kurudi nyuma na kuanza upya. Wahenga walitwambia, ni heri nusu shari kuliko shari kamili. Katiba ni ya Watanzania, kwanini usiwepo ’ Mchakato Kivuli’- Shadow process utakayojumuisha makundi mbali mbali ya kijamii. Wajadili kwa uhuru kabisa, yote. Kisha nao waje na mapendekezo yao. Ingeepusha shari kamili.

Haiyumkini suala nyeti kama la Muswaada wa Mapendekezo ya Sheria itakayosimamia mchakato wa Katiba likajadiliwa na wadau kwa siku tatu tu. Ndio, chini ya saa 100. Maana, Katiba ya nchi ni kitabu nyeti chenye kuhusu maisha ya kila siku ya Mtanzania. Hauingii akilini, utaratibu wa wadau kujadili Muswaada huu kwenye kumbi za Msekwa Dodoma na Karimjee Dar. Halafu ikawa basi, imetosha. Urudishwe kwa Wabunge, waujadili, kisha waupigie kura, na zaidi kuupitisha.

Watanzania tuko zaidi ya milioni 42. Ni vema na ni busara kukawepo na wigo mpana zaidi wa kuwafikia Watanzania wengi zaidi kadri inavyowezekana. Hivi, inatoka wapi, ’ghafla’ na ’dharura’ hii ya wadau kutakiwa kutoa maoni yao ndani ya saa 72? Maana, hili ni suala nyeti kwa Watanzania na lenye kuhusu mustakabali wa nchi. Kwa nini tusipewe muda zaidi wa kutafakari?

Na wahusika wana nafasi ya kujisahihisha na kuokoa sura zao. Maana, tukubali, kuwa mchakato unaoendelea hautasaidia kupata Katiba itakayowapa imani Watanzania kuwa italinda maslahi ya taifa lao na yenye kukidhi matakwa ya wakati tulionao. Hayo ni mashaka ya kweli ya Watanzania walio wengi, yasipuuzwe. Na Watanzania wanajua, kuwa wanachokitafuta sasa walikuwa nacho, walikipoteza, kwa bahati mbaya.

Na kuna kisa kutoka Uganda. Milton Obote, mbali ya mambo mengine, anakumbukwa na Waganda kwa tukio la kihistoria la ’ Kuchakachua’ Katiba ya nchi hiyo kwa kuifanyia mabadiliko kinyemela. Ilikuwa Aprili 15, 1966. Ilikuwa aubuhi moja. Wabunge wa Uganda, kabla ya kikao, walielekezwa kwenye masanduku yao ya makabrasha bungeni wakachukue ’ Muswaada wa dharura’ wa Marekebisho ya Katiba.

Muswaada ule wa Marekebisho ya Katiba ukajadiliwa ’ kishabiki’ na kupitishwa ndani ya saa moja. Unakumbukwa kwa jina maarufu la ’ Pigeon-hole’ Constitution- Katiba ya Sanduku la Makabrasha. Ni kitendo kile cha Obote, ndicho kilichopelekea Uganda kupitia wakati mgumu kwa miaka miaka mingi zaidi baadae.

Obote alikuwa na ugomvi na chama cha KY- Kabaka Yekka. Hivyo basi, alikuwa na ugomvi na Mfalme Fredrick Kabaka na WaBaganda. Katiba mpya ikampa nguvu nyingi Obote na UPC yake- Chama chake. Kabaka na WaBaganda walimtambua haswa Obote. Aliwanyanyasa kwa kuwafunga na hata kuwaua. Ndio, aliwanyamazisha, kwa muda.

Lakini naye, Obote, hakubaki salama. Idi Amin akaja akampindua na kushangiliwa sana na WaBaganda wa Kampala na kwengineko. Kosa alilofanya Obote ni hili; kubadilisha Katiba kukidhi mahitaji yake na ya Chama chake katika wakati uliokuwepo. Obote hakuiangalia Uganda ya miaka 50 hadi 100 iliyofuata. Na hilo ndilo tatizo la viongozi wetu wengi Afrika.

Tukirudi hapa kwetu, haitarajiwi Wabunge wa CCM walio wengi kuukwamisha Muswaada huo unaojadiliwa sasa bungeni. Na ikitokea wakafanya hivyo, kwa maana ya Wabunge hao wa CCM wakaukwamisha Muswaada huo wa sheria, basi, Wabunge hao wa CCM watakuwa wameanza kazi ya kweli ya ’ Chama kujivua magamba’ na baadhi yao kunusurika na adhabu ya wapiga kura ifikapo 2015.

Nchi yetu iko njia panda. Mbele yetu kuna njia mbili; moja inaelekea tunakopita sasa. Kwenye hali ya ’ kujifunga’ na kubaki tulipo bila kupiga hatua za haraka za maendeleo huku baadhi, wakiwamo viongozi, wakiwa na udhibiti mkubwa wa hali ya mambo. Njia nyingine inaelekea kwenye uhuru zaidi wa wananchi na uwezo wa kuwadhibiti na kuwawajibisha viongozi wao. Ni njia inayoelekea kwenye ustawi wa nchi.

Watanzania wengi kwa sasa wana kiu kubwa ya kuianza safari ya kuipita njia ya pili. Njia yenye uhuru zaidi na matumaini ya ustawi wa taifa. Njia itakayotufanya tuondokane kabisa na njia ya kwanza, njia inayotufunga na kutubakisha hapa tulipo. Kwa viongozi watakaochangia kutupitisha kwenye njia ya kwanza, nahofia, kuwa hao watakumbukwa kwa dhamira yao hiyo mbaya kwa Watanzania.

Kwa wale viongozi watakaochangia katika kutupitisha kwenye njia ya pili, basi, hao hawatasahaulika mioyoni mwa Watanzania. Watakuwa ni wanadamu walioamua kuachana na ubinafsi na kutanguliza maslahi ya taifa. Ni imani yetu, kuwa hata Wabunge wengi wa CCM wanaweza kuingia katika kundi la viongozi hao. Kutupitisha kwenye njia ya pili.

Na kama Bunge letu litabariki azma ya Serikali kuendelea kutupitisha katika njia hii ya kwanza kwenye mchakato huu wa Katiba, basi, ni dhahiri, kuwa tuendako kuna giza zaidi kulipo hapa tulipoanzia. Kuna watakaoikumbuka Katiba yetu ya sasa.

Na hiki ni kipindi kigumu sana Nchi yetu inakipitia tangu tupate Uhuru wetu.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.
Maggid Mjengwa,
Iringa
Novemba 14, 2011

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 9 mpaka sasa

  1. rubbish, pumba tupu.

    ReplyDelete
  2. Mwenyekiti Big Up kiswahili chako sio kibaya japo muharubaini sina hakika nayo lkn upo juu tofauti na waandishi wengi hasa ukizingatia kwamba ww ni wa Iringa.

    ReplyDelete
  3. Mjengwa....
    It is toooooo long winded and boring. One gets lost in the contents and intent of your prose!
    Be concise and upto the point.
    Now...... What was it you are talking about?

    ReplyDelete
  4. Jamani wabongo wa karne ya 21 tujaribu kubadilika kidogo. Wewe annony wa Mon Nov 14, 04:35:00 PM 2011 mwenzako ametoa hoja 9maoni yake). Wewe badala ya kutoa hoja yako (maoni yako ambayo hukubaliani naye)unatoa haja!!!! Tujifunze kujibu hoja kwa hoja badala ya kujibu hoja kwa haja!!!!Kwa vile hujatoa hoja yako, sisi tunakubaliana na hoja yake.

    ReplyDelete
  5. Huyo anony wa juu kachafua hali ya hewa tayari.Lugha yetu mama ni bora ikatumika katika kutoa mchango kwa kila mkereketwa.
    Binafsi napenda nimpongeze mtoa hoja huyu kwa muda wake wa kuandika pamoja na kuwafikiria watanzania walio wengi.Ni dhahili tukubaliane kwamba watanzania wanaopenda kuiona katiba mpya inawatetea ni wengi kuliko tunavyofikiri.Endapo tutatoa mwanya kwa watanzania walio wengi hii ndiyo demokrasia.Tukubali tusikubali tuna hata watanzania wasioona umuhimu wa wabunge wao sembuse uwaambie kwamba eti wabunge wameamua kuhusu katiba?
    Kama mtoa ada anavyosema, tujaribu kuwapa nafasi wananchi walio wengi kwanza, alafu matokeo yake ndiyo yajadiliwe bungeni.

    ReplyDelete
  6. Ninakubaliana kwa asilimia mia juu ya dhana ya uhuru wa kuongea (Freedom of Speach);lakini, ninapatwa na shaka na baadhi ya maoni yanayotolewa katika kuendeleza hoja ya msingi ya Ndugu Mjengwa. Mimi binafsi ninafikiri Mjengwa ana hoja za msingi juu ya mtazamo wake katika kuelekea kufanya mabadiliko muhimu sana katika katiba ya Tanzania, ambayo mabadiliko hayo yanatarajiwa kuleta njia sahihi ya kuelekea nchi ya Tanzania na watu wake katika maendeleo na miaka ijayo.
    Mimi ni msomaji mzuri wa blog za Mjengwa na Michuzi, juhudi anazofanya ndugu Mjengwa katika blog yake zinahitaji kuungwa mkono kama msomaji wa maandiko yake atakuwa anauwezo wa kufanya uchambuzi wa maandiko anayoandika (infering by reading between the lines). Suala ambalo ninalipatia shaka ni juu ya wasomaji wengine wa blog hii ya Michuzi au blog nyinginezo, ninachoona hapa ni kuwa, nilitarajia wadau wawe mstari wa mbele kujenga hoja ambayo Mjengwa anajaribu kuiweka katika ubao ya kuchukua na kuzingatia hatua madhubuti ili Tanzania iweze kupata katiba muafaka kwa maendeleo ya Tanzania ijayo. kinachovunja tamaa ni kuwa, baadhi ya wachangiaji bila hata ya kuheshimu muda na mazingatio ya muadishi, wanarukia kuponda maandishi kwa uzembe wa hata kuchangia. Kwa mfano, anonymous aliiandika "rubbish, pumba tupu" kwa ukweli maoni kama hayo ni dalili za uvivu wa kufikiri na ukosefu wa mazingatio ya msomaji na mchangiaji wa hoja hiyo.
    Napenda Wasomaji tuwe makini, ni kweli kuwa si kinachoandikwa ndani ya blog hii ama blog nyingine ni lazima kiwe kina maana, lakini kama msomaji na mchangiaji, ni vema kama utaonyesha baadhi ya hisia za uelewa katika maoni, na kama huelewi kilichoandikwa, basi ni vema pia kueleza hivyo zaidi ya kuandika utumbo.
    Kitu kingine ambacho kinanisikitisha ni kuwa, kwa kiwango kikubwa na ustadi wa hali ya juu, Mjengwa amekuwa akifanya juhudi za makusudi kuelezea na kuamsha ari ya maoni juu ya suala la katiba ndani ya blog yake na hata blog jirani kama michuzi na nyinginezo, haiyumkiniki, sina shaka na idadi na uelewa wa wasomaji wa blog hizi, cha kushangaza zaidi ni idadi ya wasomaji ambao wanatoa maoni, hebu tuwe sahihi ndugu zangu. Hoja aloandika Mjengwa ni makini sana, toa maoni yako yaliyo na mantiki ili jamii nzima ya wasomaji na wachangiaji iweze kupata mtazamo mpana juu ya hoja hii na hoja nyingine muhimu zitakazotolewa. Je ni kweli tunasubiri Mr. Mashaka aandike ndo tuanze kupingana nae? Mimi binafsi nakubaliana na mtazamo wa Mjengwa. Marekebisho ya katiba yatakayofanyika hivi sasa yatakuwa kwa maslahi ya watawala na si maslahi ya Tanzania huru na endelevu ambayo tunaitarajia siku zijazo.

    Mwilima, NYC.

    ReplyDelete
  7. bab hapo juu hayo mawazo yako bab..una haki ya kusema rubbish ila ungesaidia kama ungejibu hoja, unatufanya tukuone wewe ndo rubbish!!

    ReplyDelete
  8. hii ni blog ya ankal michuzi na sio mwenyekiti mjengwa kama wanavyojichanganya wengineo hapo juu

    ReplyDelete
  9. http://mjengwa.blogspot.comNovember 15, 2011

    Kwanza kabisa namshukuru kaka yangu Michuzi kwa kurusha hewani mtazamo wangu. Ndiye Michuzi ninayemfahamu, hana hiyana isipokuwa pale mtu anapotoa mitazamo yenye matusi au kuingilia privacy za watu.

    Aidha, nawashukuru wengine wote kwa mitazamo yenu. Hata mwenzetu aliyesema yote niliyoyaandika ni rubbish tupu naye ametoa mtazamo wake na kutuonyesha aina ya WaTanzania ambao pia tunao.

    Mwisho, nimshukuru kwa dhati Bw. Mwilima kwa kuweka msisitizo juu ya uhuru wa kujieleza na umuhimu kwa sisi kuchangia kwenye mjadala huu muhimu wa Katiba ya Nchi Yetu.
    Maggid,
    Iringa.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...