![]() |
MATHIAS CHIKAWE (MB.) WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS–UTAWALA BORA |
Ndugu wanahabari, nimewaita ili nizungumze nanyi juu ya Mpango wa Ubia katika Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa uwazi (Open Government Partnership - OGP).
Mpango huu ambao ni juhudi mpya za kimataifa katika kuendesha Serikali kwa uwazi na ushirikishwaji mkubwa wa wananchi, ulizinduliwa rasmi na Viongozi wa nchi za Marekani, Brazil, Indonesia, Mexico, Norway, Philippines, Afrika ya Kusini na Uingereza mnamo tarehe 20 Septemba 2010 wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani.
Nchi hizi waanzilishi kwa pamoja zilipitisha Azimio la kuendesha Serikali kwa uwazi na uwajibikaji kwa kuweka bayana Mipango ya utekelezaji katika nchi zao.
Kwa kutambua umuhimu wa mpango huu, Tanzania imeridhia kujiunga na mpango huo. Hadi sasa nchi nyingine 37 zimeridhia kujiunga na mpango huo zikiwemo nchi nyingine nne kutoka Bara la Afrika ambazo ni Afrika ya Kusini, Ghana, Kenya na Liberia.
Ndugu wanahabari, msisitizo mkubwa wa mpango huu ni kuongeza uwazi na uwajibikaji katika Serikali, kuwawezesha wananchi kupata taarifa sahihi na kuzitumia kwa maendeleo yao, kuzuia na kupambana na rushwa na kusisitiza matumizi ya teknolojia na ubunifu katika kuimarisha utawala bora.
Ili kuwa mwanachama wa mpango huo, nchi zinatakiwa kuunga mkono Azimio la Uwazi katika Kuendesha Serikali; kuandaa Mpango Kazi kwa kushirikiana na wananchi na kuweka utaratibu wa uwazi wa kutoa taarifa za utekelezaji wa mpango kazi huo.
Ndugu wanahabari, hatua ya kwanza ya kuchukua baada ya nchi kuridhia kujiunga na mpango huo muhimu ni kuandaa mpango kazi unaoshirikisha wadau mbalimbali zikiwemo asasi za kiraia, Sekta Binafsi na Umma kwa ujumla.
Mpango huu unatakiwa kuandaliwa kwa uwazi, na kwa kuanzia utahusisha vipaumbele vichache vitakavyotekelezeka. Mpango utaendelea kuongeza maeneo mengine ya utekelezaji kadri uzoefu utakavyopatikana.
Vipaumbele vya awali vitahusu kuimarisha uwazi, uadilifu na uwajibikaji katika utoaji wa huduma kwenye sekta tatu za Afya, Elimu na Maji.
Napenda kupitia kwenu kuwataarifu Watanzania wote kwamba, Serikali imeanza rasmi mchakato shirikishi wa kuandaa Mpango Kazi wa Uwazi katika kuendesha shughuli za Serikali. Maandalizi ya mpango huu yatashirikisha wadau niliowataja awali, na tutatumia njia mbalimbali zitakazowawezesha wananchi kutoa maoni yao kuhusu maeneo mahsusi ambayo yakiboreshwa, utoaji wa huduma utaimarika.
Kutakuwa na mikutano ya wazi ambapo Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi, Vyombo vya Habari na Wananchi kwa ujumla watapata fursa ya kujadiliana na Serikali ili kupata mwafaka wa pamoja wa yale ambayo yatawekwa kwenye mpango unaoandaliwa.
Aidha, Tovuti ya www.mwananchi.go.tz, barua za kawaida kupitia posta (Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Ikulu, S.L.P. 9120, Dar es Salaam), ujumbe kupitia simu ya mkononi (SMS) namba 0658-999222, barua pepe: ogp@ikulu.go.tz na blogu: www.ogptz.com zitatumika kukusanya maoni ya wananchi. Mawazo yote yatakayotolewa yatafanyiwa kazi na kwa uwazi mkubwa.
Ndugu wanahabari, rasimu ya mpango unaoandaliwa itajadiliwa katika kikao cha Mawaziri wa nchi zinazohusika na mpango huu. Kikao hicho kitafanyika tarehe 7 – 8 Desemba, 2011 huko Brasilia - Brazil.
Katika kikao hicho, nchi zitabadilishana uzoefu wa maandalizi ya mipango kazi ili hatimaye kuwa na rasimu itakayowasilishwa kwenye kikao cha Wakuu wa Nchi wanachama kitakachofanyika Brazil, mwezi Machi 2012. Baada ya Mpango huu kupitishwa na Mkutano wa Wakuu wa Nchi, kila nchi mwanachma itaanza utekelezaji.
Napenda niwakaribishe kwa dhati kabisa Wananchi kushiriki kutoa maoni yenu yatakayosaidia kuandaa mpango wa kitaifa wa kuongeza uwajibikaji, uwazi na uadilifu katika utendaji wa kazi za Serikali. Waandishi wa habari mna dhamana na wajibu mkubwa wa kuelimisha umma kushiriki kutoa maoni yao ili mpango unaoandaliwa ukamilike kwa wakati.
Hatuna muda mrefu sana kati ya sasa na tarehe ya kukamilisha rasimu ya kwanza ya mpango huo ambayo ni tarehe 7 Desemba, 2011. Nina imani kwa kushirikiana kipindi hiki kinatosha kukamilisha kazi hii. Ni vyema vyombo vyote vya habari vikaubeba ujumbe huu mzuri na kuufikisha kwa wananchi kwa nia ya kuwaelimisha na kuwahamasisha kushiriki kutoa maoni.
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza!
MATHIAS CHIKAWE (MB.)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS–UTAWALA BORA
IKULU
DAR ES SALAAM.
Tarehe 14 NOVEMBA, 2011
Ni mpango mzuri sana kama utatumiwa vizuri utaleta maendeleo. Kusije tu kukawa na unafiki kama ambavyo kumekuwepo katika mipango mingine ya maendeleo.
ReplyDelete