![]() |
Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Alfonso E. Lenhardt |
Na Balozi Alfonso E. Lenhardt
Ushirikiano imara kati ya Marekani na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliojengeka katika misingi ya kuheshimiana na ubia katika maendeleo, ulianza zaidi ya miaka 50 iliyopita kwa urafiki kati ya Marais John F. Kennedy na Mwalimu Julius Nyerere.
Ushirikiano wetu umeendelea kukua na kuimarika hadi hivi leo. Matokeo ya msaada wa Marekani hayapimwi na fedha pekee bali Maisha yanayobadilishwa na kuokolewa kutokana na programu zetu za maendeleo.
Mwaka 2011, watu wa Marekani walichangia zaidi ya Shilingi za Kitanzania bilioni 850 (sawa na Dola za Kimarekani milioni 700) kama msaada rasmi wa kiserikali. Msaada wa Marekani kwa Tanzania unalenga katika shughuli za maendeleo na kujenga uwezo na si katika kuchangia moja kwa moja bajeti za wizara.
Programu zetu zinalenga katika kukuza uwazi, kushughulikia masuala ya afya na elimu na viashiria vingine vya maendeleo. Kama ilivyosisitizwa wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje Bi Hillary Rodham Clinton kwamba, Tanzania ipo katika wakati sahihi wa kihistoria wa kupiga hatua kubwa ya maendeleo na ukuaji wa kiuchumi, ilimradi viongozi wake wanaendelea kuchagua mwelekeo sahihi wa maendeleo.
Jitihada zetu za maendeleo ni kubwa na zinazogusa nyanja nyingi. Mathalan, katika mwaka 2011, watu wa Marekani kwa kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) wametoa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 240 ili kuboresha afya ya umma, ubora wa elimu ya msingi, uhifadhi wa bayoanuai na usimamizi wa maliasili.
Mpango wa kuendeleza kilimo ili kujitosheleza kwa chakula uitwao "Feed the Future" uliozinduliwa na Bi. Clinton hapo mwezi Juni mwaka huu umetoa Dola za Kimarekani 61.5 milioni katika mwaka 2011 ili kuinua maendeleo ya kilimo, kukuza uzalishaji wa mazao ya kilimo, kukuza masoko na biashara ya mazao ya kilimo, kuwekeza katika tafiti na ubunifu katika masuala ya kilimo, kuchochea ukuaji sawia (equitable) wa maendeleo vijijini na kushughulikia tatizo la lishe duni kwa mama na watoto nchini Tanzania.
Mfuko huu umedhamiria kuwezesha ukuaji wa haraka na endelevu wa sekta ya kilimo - huku wanufaika wakubwa wakiwa ni wakulima wadogo wadogo na jamii za vijijini.
Marekani imeweza kushirikiana vyema na Tanzania katika kuboresha afya ya watu wake.
Mpango wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na UKIMWI (PEPFAR) ni mfuko mkubwa zaidi uliowahi kutengwa kimataifa na taifa moja katika kushughulikia ugonjwa wa aina moja.
Toka mwaka 2004, zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 1.8 zilizotolewa na PEPFAR zimesaidia taasisi za kitaifa na kimataifa na asasi zisizo za kiserikali katika kutekeleza shughuli zao zinazolenga kukabiliana na janga la VVU/UKIMWI ikiwa ni pamoja na utoaji wa matunzo na matibabu, kuzuia maambukizi, kukabiliana na athari za janga hili na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya.
Kutokana na msaada huo, zaidi ya Watanzania 300,000 wanaoishi na VVU wanapatiwa dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo. Aidha, mamilioni ya Watanzania wameweza kupatiwa huduma za upimaji wa VVU na ushauri nasaha na kunufaika kutokana na taarifa zinazotolewa kuhusu namna ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU.
Kila mwaka, mamia ya maelfu ya akina mama wajawazito hupata huduma za upimaji wa VVU wakati wa ujauzito na iwapo wanagundulika kuwa na VVU; wanapatiwa dawa za kuzuia mambukizi kwenda kwa watoto wao.
Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Malaria ulioanzishwa mwaka 2005, ni mpango ulioandaliwa na Serikali ya Marekani ili kuzisaidia nchi 17 za Kiafrika kukabiliana na mzigo mkubwa wa Malaria na kupunguza umasikini.
Toka mwaka 2006, mfuko huu umetoa Dola za Kimarekani milioni 210 ili kusaidia jitihada za kukabiliana na malaria nchini Tanzania.
Fedha hizi zimesaidia shughuli mbalimbali nchini kote ambazo zimewezesha kupungua kwa kiwango cha malaria hadi chini ya asilimia 1 na kusaidia ugawaji wa vyandarua kwa wote Tanzania bara.
Kituo cha Marekani cha Udhibiti wa Maradhi (CDC) kinashirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na hatari mbalimbali za kiafya na milipuko ya maradhi ya kuambukiza kama vile mafua makali ya H1N1, Homa ya Bonde la Ufa, na Surua.
Kwa kupitia CDC vituo vya kisasa vya upimaji wa VVU,ushauri nasaha na matibabu zaidi ya 80 vimefunguliwa nchini kote vikitoa huduma za bure za matibabu, maabara na ushauri nasaha zinaotolewa na wataalamu wa afya wenye ujuzi wa hali ya juu.
Ili kukabiliana na mahitaji makubwa ya miundombinu ya usafirishaji, nishati na maji, taasisi ya Millennium Challenge Corporation (MCC) chini ya mkataba uliosainiwa hapo mwaka 2008, inaipatia Tanzania msaada wa Dola za Kimarekani milioni 698 , huuukiwa ni msaada mkubwa zaidi katika historia ya MCC.
Kabla ya hapo MCC iliipatia Tanzania Dola za Kimarekani milioni 11.15 kwa ajili ya program ya awali kusaidia katika kukabiliana na rushwa katika manunuzi ya umma, kuimarisha utawala wa sheria kwa ajili ya utawala bora, kutoa mafunzo ya uandishi wa habari za uchunguzi kwa zaidi ya waandishi wa habari 300 na kusaidia vyombo huru vya habari kama kipengele muhimu katika kukuza demokrasia na uwazi.
Mabadilishano na uhusiano kati ya watu wa mataifa haya mawili umeendelea kuwa msingi muhimu wa maelewano yetu. Tanzania ilikuwa ni nchi ya kwanza kupokea wafanyakazi wa kujitolea wa Peace Corps volunteers hapo mwaka 1962.
Zaidi ya wafanyakazi wa kujitolea 2,000 wamefanya na wanaendelea kufanya kazi nchini Tanzania wakihudumu kama walimu wa sayansi na teknolojia ya mawasiliano katika shule za sekondari na vyuo vya ualimu.
Aidha, wafanyakazi hawa wa kujitolea wamehudumu katika miradi ya elimu ya afya inayolenga kuongeza uelewa kuhusu masuala ya afya na kubadili tabia pamoja na miradi ya mazingira inayoshughulikia uendelezaji wa maliasili katika ngazi za vijiji.
Tuna fahari kubwa kwamba toka mwaka 1965 hadi 1968 Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika Bw. Johnnie Carson alihudumu kamba mfanyakazi wa kujitolea nchini Tanzania katika maeneo ya nyanda za juu kusini kutoka.
Hali kadhalika, watu wa Marekani wanafadhili programu mbalimbali za mabadilishano zinazowawezesha Watanzania wengi kwenda Marekani kila mwaka. Programu hizo ni pamoja na programu za kielimu za Fulbright, Humphrey na programu ya Mafunzo ya Kingereza kwa ngazi ya shahada ya pili na zaidi.
Pia kuna programu za mabadilishano kwa ajili ya kusaidia kuinua viwango vya wasanii, waandishi wa habari, watumishi wa umma, viongozi vijana, wanamuziki na wanafunzi. Huko Zanzibar, Marekani imefadhili programu za mafunzo ya Kiingereza na kutoa zaidi ya vitabu vya sayansi 600,000 kwa wanafunzi wa shule za sekondari.
Katika kuheshimu na kuthamini urithi wa kipekee wa utamaduni, toka mwaka 2002 Mfuko wa Balozi wa Hifadhi ya Utamaduni umetoa zaidi ya Dola za Kimarekani 870,579 ili kusaidia miradi kadhaa ya ukarabati majengo ya kihistoria, ikiwa ni pamoja na Dola za Kimarekani 700,000 kwa ajili ya kukarabati magofu ya kihistoria ya Kilwa Kisiwani.
Misaada yote ya maendeleo ya Marekani inatolewa kwa kupitia taasisi za kiserikali, asasi zisizo za kiserikali au wabia wa humu nchini. Tunafahari kubwa kutambua mchango muhimu wa wabia wetu hawa na ni matumaini yetu tutaendelea kupata fursa ya kufanya kazi pamoja ili kuimarisha ushirikiano wetu na kuboresha maisha na matumaini mema ya siku za baadaye ya watu wa Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...