Waheshimiwa wadau,
Kwa heshima na taadhima chini ya Libeneke lenu pendwa la Globu ya Jamii napenda kutoa salamu za XMAS NA MWAKA MPYA wa 2012 kwa wadau wote na popote mlipo ulimwenguni. Nitakuwa mtovu wa fadhila endapo kama sintosema kwamba bila ninyi Libeneke lisingenoga kama lilivyo hivi sasa.Napenda sema ahsanteni sana na nawashukuru kwa kampani mnayonipa na mliyonipa toka Septemba 5, 2005 nilipozindua rasmi Libeneke hili la Globu ya Jamii kule Helsinki, Finland, chini ya usimizi wa mdau mkuu kaka Ndesanjo Macha.
Leo tunasherehekea sikukuu ya Krismas huku kwenye kona tukiwa tunapiga endiketa ya kuuanza mwaka mpya wa 2012 tukiwa na kila aina ya matumani kwamba Mola atatujaalia si pumzi tu bali pia fanaka katika kila jambo la maendeleo wakati tukianza ngwe huku tukiwa tumetoka kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara hivi majuzi tu.
Nina mengi ya kusema, ila endapo nitathubutu kufanya hivyo nahisi nitajaza ukurasa wote huu lakini bado nisiweze kueleza robo tu ya niliyonayo moyoni. Itoshe tu niseme ahsanteni sana wadau wote kwa kuendelea kuniunga mkono kwenye shida na raha, katika kukubaliana na katika kupingana bila kupigana. Ahsanteni sana, sana, sana wadau wa Globu hii ya Jamii.
Napenda pia kukumbusha sera ya Globu ya Jamii ya kwamba ‘Kilicho chema kwa bata mzinga, si chema kwa kuku’ (what’s good for the goose, is bad for the hen) yaani si rahisi kumridhisha kila mmoja kati ya wadau milioni kumi na nne na ushee wanaotembelea Globu ya Jamii. Hivyo nawataka radhi kabisa wale ambao nitakuwa siwaridhishi kwa namna moja ama nyingine, na kwamba hiyo si kwa makusidi bali ni hali halisi ya maisha. HAKUNA ALIYE MKAMILIFU ILA MOLA PEKEE. Kwa hiyo maoni yako yakitiwa kapuni ujue ni katika hilo. Nia ni ile ile ya kupashana bila kuwa na haja ya kujeruhi mtu ama watu kwa kuchafua hali ya hewa.
Wakati ni kweli kwamba mwaka 2012 una changamoto (challenges) kibao katika tasnia hii ya libeneke, lakini si uwongo kwamba kwa msaada wenu wadau hali inaweza kuboreshwa zaidi. Na hii itawezekana endapo kama sie sote tutatumia teknolijia hii ya habari kwa kuendeleza maendeleo ya nchi na si mtu binafsi ama kikundi Fulani cha dini, siasa ama jamii.
Katika hilo nafurahi na kuona fahari kubwa kwamba Globu ya Jamii imekuwa chachu ya kuanzishwa Libeneke nyingi nchini na nje ya nchi zenye kuwa na msimamo wa kupashana habari kwa njia ya kisasa. Ushahidi ni jinsi ambavyo Globu ya Jamii ilivyo mstari wa mbele katika kutangaza blog mpya zinazoanzishwa kila ikitokea.
Pamoja na yote hayo nina masikitiko makubwa kwamba blogu nyingi zinazoanzishwa zinakuwa ni zile zile tu, kama zetu za akina sie. Yaani kwa mtazamo wa wengi blogu ni kuwa na habari za kila mara ama kila siku, badala ya wanaoanzisha blogu kujikita katika fani ambazo wamebobea. Badala ya wote kujikita katka katika habari, tunahitaji blogu za Nyanja tofauti zaidi ya habari tu.
Kwa mfano tunahitaji blogu za useremala, uashi, urembo ama hata muziki wa mipasho. Si kila aanzishaye blogu ajikite katika habari na kutaka kutunishana misuli na kina sie tulio ndani ya tasnia ya habari. Angalizo hapa ni kwamba copy & paste aghalabu hukimbiza wasomaji.
Mwisho napenda kutoa shukurani kwa wote walioifanya Globu ya Jamii ifike hapa ilipo leo. Ni ngumu kumtaja kila mmoja. Lakini si vibaya nikiwataja baadhi ambao wamenipa msukumo kuendeleza Libeneke.
Naomba nianze na mdau mkuu Ndesanjo Macha aliyenifungua macho na kuanza kublogu, wa pili ni kaka yangu mpendwa aliye huko Helsinki, Finland, Fidelis Tungaraza a.k.a Mti Mkubwa (Fide nashukuru sana kwa ushauri wako wa kila mara) , Jeff Msangi wa Canada, Balozi Peter Kallaghe na Balozi Mwanaidi Maajar Balozi Patrick Tsere, Maggid Mjengwa, Haki Ngowi, Francis Godwin (asante na hongera kwa kuendeleza Libeneke huko Iringa) wadogo zangu Ahmad na Othman Michuzi, Mh. Lazaro Nyalandu, Dk. Emmanuel Nchimbi, Mh. Amos Makalla, kaka Gardol wa Reading, Da'Chemi Che-Mponda, Shamim Mwasha 'Zeze', Zubeir Masabo, Lau Shari wa Arise na juu ya yote mke wangu Ainde na Rais Jakaya Mrisho Kikwete (nashukuru sana mheshimiwa Rais kwa kunipa moyo wa kutembelea kwako blogu zetu mbalimbali kila siku, unatutia moyo sana kwa kweli).
Naomba pia niwashukuru wadhamini wakuu wa Globu ya Jamii wakiongozwa na Vodacom Tanzania, Tanzania Breweries Limited, CRDB,NBC,NMB,DSTV,Giraffe hotel,Mansoon, LUCUS, Hillview Family, TIB,NHC,Precision Air,Air Tanzania, Export Showroom, IOM,Dr. Mkombozi,Mbezi Garden,TravelStart,VOA,EASB,Photo Point,Wedding Bells,Umoja Phone,SilverBoutique,OFL,Safari Recovery na Brillante ambao bila wao tusingekuwa hapa leo.
Mwisho na mwanzo ni MK Computer Tweaks ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba tuna blogu zenye muonekano wa kimataifa, chini ya kaka Christopher Makwaia. Asante sana MK kwa yote uliyoifanyia Globu ya Jamii na unayoendelea kuifanyia. Mola akuzidishie!
HERI YA KRISMANI NA MWAKA MPYA MDAU POPOTE ULIPO
Ankal,
Muhidin Issa Michuzi



Mjomba hii dunia ni ya kibepari yaani mwenye nguvu ndio atakaye ishi zaidi(survival for fittest)kwa hiyo kuhusu kuanzishwa kwa blogu nyingi na yanye lango kama lako hutakiwi kulaani kama una nguvu utaishi zaidi na kama huna utaperish mjomba.ingekuaje kama itv ingezuia star tv, tbc au tv nyingine zisiwepo kisa wao wanatoa habari?na je mbona kuna habari zinatolewa tbc,itv na channel nyingine ni zilezile?acha ubinafsi wewe najua ushaanza kuogopa maana kuna blogu nyingi zinakuja kwa spidi ya ajabu so acha zije nyingi zaidi na huwezi kumuamulia mtu afungue blogu inayohusu vitu vingine.Kwa hiyo acha watu wafanye hivyo usipende ubinafsi na ukumbuke ingekuaje wakina zamogera, mahadhi wangesema watu wengine wasiwe wachezaji?acha hizo wewe.....nana ukae ukijua kabisa kuwa hakuna copy n paste wanaokutumia wewe ndio wanaowatumia na wengine unataka kutumiwa wewe tu? hii ni dunia ya capitalist bwana mwenye nguvu atasurvival na aliye weak ata perish.ni hayo tu
ReplyDeleteAnkal, mbona umenisahau mdau wako wa kujipendekeza Mzee wa ZEZE wa hapa Mikanjuni Tanga kwa kunitaja kwa jina. Hadhi yangu kwenye blogu hii kidoogo anayenikaribia ni Ndesanjo na FIDE TU.
ReplyDeleteTeh ! Teh! Teh!!!!!
Michuzi....naona mimi umenisahau ...kwenye salamu zako...
ReplyDeleteHeri na Wewe Ankali!!!!!.......
ReplyDeleteLIBENEKE OYEEEEEE!!!!!!!!!!!!!
Ndugu nawaomba sana watu waelelewe, kuwa tatizo la maji linaletwa na Magodown and ukuta ndefu zinazojengwa na viwanda katika bonde la msimbazi, kuta hizi zinabana maji , na maji yakimbilia kwa wenyeji. Kuwaamisha wenyeji, mkigawa viwanja kwa magodown na viwanda, mjue miaka ijayo daraja la selander litapotea na maji yataingia nyumba za upanga. Tafakarini vizuri. Tatizo siyo hilo livooonekana
ReplyDeleteNdugu nawaomba sana watu waelelewe, kuwa tatizo la maji linaletwa na Magodown and ukuta ndefu zinazojengwa na viwanda katika bonde la msimbazi, kuta hizi zinabana maji , na maji yakimbilia kwa wenyeji. Kuwaamisha wenyeji, mkigawa viwanja kwa magodown na viwanda, mjue miaka ijayo daraja la selander litapotea na maji yataingia nyumba za upanga. Tafakarini vizuri. Tatizo siyo hilo livooonekana
ReplyDelete