Na Mwandishi Maalum
New York
Tanzania imeishauri Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kuboresha uhusiano wake na Afrika kama inataka kufanikiwa katika uendeshaji wa shughuli zake.
Ushauri huo umetolea na Mhe. Ombeni Sefue, Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa alipozungumza wakati wa mkutano wa Kumi wa nchi wanachama wa ICC. Mkutano huo unafanyika hapa Makao Makuu ya Umoja ya Mataifa ukiambatana pia na uchaguzi wa majaji sita watakaochukua nafasi zitakazoachwa wazi na majaji watakaomaliza muda wao mwakani.
“ Bila ya kuingilia utendaji wenu wa kazi, tunaamini uhusiano wa karibu kati ya mahakama hii na nchi za Afrika ni jambo la muhimu sana katika kuifanya mahakama itekeleze majukumu kikamilifu” akasisitiza Balozi Sefue.
Ushauri wa Tanzania wakuitaka Mahakama hiyo kuboresha uhusiano wake na Afrika, unatokana na ukweli kwamba. kumekuwapo na sintofahamu kati ya makama hiyo ya makosa ya jinai na Afrika, kwa kile ambacho Afrika ambayo ndiyo yenye idadi kubwa ya wanachama ikiamini kwamba mahakama hiyo imekuwa haitendei haki Afrika.
Akisisitiza umuhimu wa ICC kuboresha mahusiano yake na Afrika na kuboresha utendaji kazi wake. Balozi anasema licha ya kuwa idadi kubwa ya wanachama ni kutoka Afrika, lakini hata kesi ambazo hadi sasa zimo katika mahakama hiyo ambazo ni sita zinaihusu Afrika.
Akizungumzia utendaji kazi wa Mahakama hiyo, Balozi Sefue anasema kwa ujumla imekuwa ikifanya kazi vizuri hususani ya kusimamia utawala wa sheria na haki, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba wale wote wanaotuhumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu wanafikishwa mbele ya mkono wa sheria.
Akabainisha kuwa, mahakama hiyo imekuwa chombo muhimu katika kuzuia uhalifu mkubwa dhidi ya binadamu, kuzuia ukiukwaji wa haki za binadamu, kusimamia utawala wa sheria na haki na pia kuhakikisha kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria.
Kuhusu raslimali fedha. Mwakilishi huyo wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, amesema, ili mahakama hiyo iweze kutenda haki ni lazima iwe na bajeti ya kutosha vinginevyo itashindwa kabisa kutekeleza wajibu wake.
Kutokana na mtikisiko wa uchumi kumekuwapo na taarifa za kupunguzwa kwa bajeti ya mahakama hiyo hatua inayoelezwa na wanadiplomasia na asasi za kiraia kwamba itakwaza utendaji wa mahakama hiyo.
Makahama hiyo ambayo nchi kadhaa ziliridhia kuanzishwa kwake miaka 13 iliyopita hivi sasa ina wanachama wapatao 120. Kati yao 33 ni kutoka Afrika, 18 ni nchi za Asia na Pacifiki, 18 ni kutoka Ulaya Mashariki, 26 ni nchi za Amerika ya Latini na Visiwa vya Karibian na 25 ni kutoka nchi za Ulaya Magharibi na nyinginezo.
Wakati huo huo,majaji sita kati ya 19 waliojitokeza kuwania nafasi za ujaji katika ICC wamechaguliwa kufanya kazi katika Mahakama hiyo kwa kipindi cha miaka tisa.
Katika uchaguzi huo uliokuwa na ushindani mkubwa na kura kupigwa hadi raudi ya 15 walioshinda na nchi zao kwenye mabanoniCarmonaAnthonyThomasAquinas(Trinidad&Tobago),Defensor_Santiago Miriam ( Philippines), Fremr, Robert (Czech Republic),Herrera Carbuccia Olga Venecia ( Dominica), Chile Eboe-Osuji ( Nigeria) na Howard Marrison Qc (Uingereza).
Pamoja na kuwachagua majaji hao, nchi wanachama wa ICC wiki iliyopita zilimpitisha kwa kauli moja, Bibi. Fatou Bensounda kuwa Prosecutor mpya akichukua nafasi ya Bw. Lois Moreno-Ocampo anayemaliza muda wake mwakani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...