![]() |
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein |
Na Faki Mjaka Maelezo Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein amesema kuwa Jengo la Zamani la iliyokuwa Sauti ya Tanzania Zanzibar lazima lirejeshwe katika hadhi yake ya zamani ili liweze kutumika katika maswala mbalimbali ya Sanaa.
Amesema kuwa Jengo hilo lina historia kubwa sana kwa upande wa Zanzibar na Jengo ambalo ni madhubuti na lipo katika sehemu nzuri hivyo kurejeshwa kufanya kazi kama zamani ya kuonesha michezo ya kuigiza na kutumika kwa maonesho ya Vikundi vya Taarabu litarejesha hadhi na haiba katika Zanzibar.
Dk. Shein ameyasema hayo hivi leo wakati alipolitembelea Jengo hilo ili kuona juu ya matumizi yake ya hivi sasa na hali lilivyo kutokana na historia kubwa ya Jengo hilo kwa Zanzibar.
Amesema kuwa Shirika la Gazeti la Serikali Zanzibar linalochapisha Gazeti la Zanzibar Leo katika Jengo hilo litatafutiwa sehemu nyingine nzuri na kubwa ili kuweza kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi na Jengo hilo kuacha kutumika kwa ajili ya sanaa.
Akizungumzia juu ya suala la iliyokuwa Sauti ya Tanzania Zanzibar amesema kuwa imefika wakati kwa uongozi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kuandika historia ya kuanzishwa Redio hiyo ambayo ni ya mwanzo katika Afrika Mashariki.
Dk. Shein amesema kuwa si vizuri kwa Redio hiyo kuwa ya mwanzo kuanzishwa wakati historia yake haionekani wala haipo hivyo ni wajibu viongozi wa Shirika hilo kuchukua kila juhudi kuona kuwa wanaindaika historia ya kuanzishwa kwa Redio hiyo pamoja na viongozi wake kuwekewa kumbukumbu za picha wakiwemo watangazaji wake.
Aidha Dk.shein ameutaka uongozi wa Wizara ya Habari Utamaduni Utalii na Michezo kulienzi na kulidumisha Jengo hilo kwa kulifanyia matengenezo kwani amesema kuwa hivi sasa huwezi kupata jengo madhubuti na lenye haiba yake hilo.
Akizungumzia juu ya Habari Maelezo Zanzibar amesema kuwa hatua iliyochukuliwa ya kuanza ujenzi wa sehemu ya Maktaba itasaidia sana katika uwekaji na utunzaji wa kumbukumbu za matukio mbalimbali za Picha,Magazeti na Majarida.
Mapema Mkurugenzi wa Idara Habari Maelezo Zanzibar Yussuf Omar Chunda alimuelezea Rais Shein historia ya Jengo hilo na matumizi yake ya hivi sasa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...