Mfuko wa maendeleo ya watu wenye ulemavu wa ngozi BADEF ambao ni taasisi isiyo ya kiserikali (NGO) uliasisiwa na mbunge wa Lindi mjini Mhe. Salum Kalfan Barwany umezindua kampeni maalum ya kutunisha mfuko utakao tumika kuelimisha umma wa watanzania ili kubadilisha dhana potofu dhidi ya jamii hiyo na hivyo kuondokana na vitendo vya kikatili dhidi yao vinavyodaiwa kuitendwa kwa misingi ya imani ya kishirikina.

Kampeni hio inayoitwa ‘Nifahamu’ inalenga kuelimisha umma juu ya madhila yanayowapata watu wenye ulemavu wa ngozi na hivyo kuiomba jamii kukusanya jumla ya shilingi milioni 500,000,000 za kitanzania kwa ajili ya kazi hiyo muhimu. ‘mimi (Barwany) nikiwa mtu mwenye ulemavu wa ngozi, naelewa fika madhira yanayowakabili watu wa aina yangu nchini. 

Kwa msingi huo, nimeazimia kuendesha kampeni hii ya ‘Nifahamu’ ili kuleta mabadiliko stahili kwenye baadhi ya sekta ambazo zimewaacha kando watu wenye ulemavu wa ngozi nchini. Kwa kuanzia, BADEF italenga maeneo ya elimu, afya na ufahamu kuhusu dhana ya ulemavu wa ngozi. Sekta hizi zikikaa vizuri zitasaidia, kwa kiasi kikubwa, kukomesha vitendo viovu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi na kuondoa unyanyapaa ambao ni tatizo sugu dhidi ya jamii hii nchini.’

Aidha, kampeni inalenga kupunguza kama siyo kuondoa kabisa tatizo la vifo vya utotoni vya watu wenye ulemavu wa ngozi vinavyotokana na janga linaloweza kuzuilika la maradhi ya saratani ya ngozi. Madaktari wanathibitisha kwamba saratani ya ngozi inatibika na kupona kabisa lakini lazima kulielewa tatizo na kuanza tiba sahihi mapema.

BADEF inalenga kufanikisha kampeni hii ya kitaifa ya kuleta mabadiliko chanya kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kupitia mpango kabambe wa elimu kwa umma yaani ‘Nifahamu’ nakudhamini kiraslimali miradi mbalimbali yenye malengo ya kukomesha ubaguzi na unyanyapaa na hivyo, kuleta usawa wa ushiriki wa watu wenye ulemavu wa ngozi katika maswala yote yahusuyo jamii ya waTanzania. 

Wakati huu tunaadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania, nchi yetu, ambayo inajulikana kwa jina zuri la kisiwa cha amani duniani imegubikwa na doa chafu la mauaji, unyofolewaji viungo na manyanyaso dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Ndani ya kipindi hiki cha miaka 50 ya uhuru, bado kundi la watu wenye ulemavu wa ngozi limekabiliwa na vifo vya ujanani vya saratani ya ngozi, mazingira yasiyo rafiki ya kielimu, umaskini uliokidhiri, unyanyapaa na mengineyo. Tuna wajibu wa kuonyesha njia, tuna wajibu wa kuandaa mazingira rafiki na kuiomba jamii ituunge mkono ili kufanikisha kampeni hii.

BADEF iliyo sajiliwa kwa namba 4266, inazindua kampeni hii leo kupitia vyombo vya Habari na imo katika maandalizi kabambe ya utunishaji mfuko kupitia chakula cha hisani, tukio hilo linatarajiwa kufanyika Februari 2012, ambapo wadau na wahisani wa ndani na nje ya nchi yetu watakaribishwa kuchangia kwa hali na mali.

BADEF inawakaribisha watu wote (watanzania na wageni) wenye nia njema kuchangia kampeni hii. Inakaribisha watu binafsi, mashirika ya dini, makampuni, idara/wizara za serikali, wanataaluma, wanamichezo, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyama vya siasa, mashirika ya kimataifa, vyama visivyo vya kiserikali, balozi za nje na wengineo kushiriki katika kampeni hii kwa hali na mali kukomesha unyanyasaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...