Wachezaji wa timu ya Asante Kotoko wakiwasili nchini tayari kwa mchezo wao wa kesho dhidi ya timu ya Simba kwenye uwanja wa Taifa. Mchezo huo umeandaliwa kwa ajili ya sherehe ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru.
TIMU ya soka ya Kumasi Asante Kotoko iliwasili jana kwa ajili ya mechi maalum dhidi ya Simba iliyopangwa kufanyika kesho kwenye uwanja wa Uhuru huku ikitoa tambo kibao dhidi ya wapinzani wao hao.
Kocha msadizi wa timu hiyo, Isaac Sarfo alisema kuwa wamekuja na kikosi cha wachezaji wanaofanya vyema katika ligi ya Ghana na kuwataka mashabiki kufika kwa wingi ili kuona mchezo huo.
Alisema kuwa kwa sasa wamekujikusanyia jumla ya pointi 21 na wachezaji wake wamekuja kuendeleza wimbi la ushindi kwa timu yao na si vinginevyo.
“ Hakuna sababu ya kushindwa katika mchezo huo, tumejiandaa vilivyo na bila shaka tutaibuka na matokeo mazuri, ” alisema Sarfo.
Alisema kuwa wamefurahia sana kuwepo katika maadhimisho ya miaka 50 yaUhuru wa Tanzania kwani waasisi wa mataifa yao Marehemu Kwame Nkurumah na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wameacha historia kubwa hapa duniani.
“Hatujasita kuja mara baada ya kuambiwa madhumuni ya mchezo huu, tutaomba chama chetu cha soka kuahirisha mechi zetu ili kuja kujumuika na watanzania, nao walikubali ombi letu huku tukiwa tumebakiza mechi nne za ligi, hii ni mechi muhumu na ya kihistoria,” alisema.
Nahodha wa timu hiyo, Danielnii Adjei alisema kuwa Simba wasitarajie mteremko kutoka kwao kwani wamedhamilia kushinda kwa mabao mengi.
“Nashukuru kwa kupewa heshima hii, ni faraja kwetu kushiriki katika mechi kubwa ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru, tumekuja kamili na tunashinda tu,” alisema Adjei.
Mwenyekiti wa Kampuni ya Future Century, Hellen Masanja alisema kuwa maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika na kabla ya mchezo huo, timu ya soka ya waandishi wa habari za michezo nchini, Taswa FC itacheza na mechi ya utangulizi kwa kupambana na timu ya kombaini ya wanawake wa mkoa wa Dar es Salaam, Mzizima Queen United.
Masanja alisema kuwa mchezo huo utaanza saa 8.30 na mashabiki wanaombwa kufika kwa wengi ili kuona vipaji vya wachezaji wa timu ya Kotoko na Simba.
Wachezaji wetu waige jinsi ya kuvaa sio kila siku wanavaa mijezi sababu ni wachezaji.Angalia hawa walivyo jirepresent.
ReplyDeleteKweli kabisa, kumbe wachezaji si lazima wavae mitisheti mikubwa na majeans na yebo yebo na waya za simu masikioni..
ReplyDelete