Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe. Ombeni Sefue akizungumza kwa niaba ya Nchi za Afrika wakati wa Mkutano wa Tano wa kilele uliokuwa ukijadili ufadhili wa maendeleo hususani kwa nchi zinazoendelea. katika mkutano huo ambao ulifanyika kwa siku mbili hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, na kufunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa UM Dkt. Asha- Rose Migiro, nchi za Afrika zilisisitiza haja na umuhimu wa nchi zilizoendelea kutimiza ahadi zao za kuzisadia nchi zinazoendelea, huku wafadhili hao nao wakitaka nchi zinazoendelea kuwajibika zaidi kwa kukusanya mapato yao ya ndani, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi wao, kupiga vita rushwa na kusimamia uwajibikaji na kukuza biashara na uwekezaji.

Na Mwandishi Maalum

New York

Wakati utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya kufadhili maendeleo kwa nchi maskini yakiwa yamekwama, huku washirika wa maendeleo wakijipanga kupunguza misaada yao kwa nchi zinazoendelea. Afrika kwa Upande wake imewataka washirika hao kutimizia ahadi zao za huko nyuma na kuacha kusingizia mdodoro wa uchumi.

Akizungumza kwa niaba ya nchi za Afrika ,Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue amesema, nchi zilizoendelea zinawajibu wa kutimiza ahadi zao kwa mujibu wa makubaliano ya Monterrey na Azimio la Doha. Na hasa ikitiliwa maanani kwamba nchi zinazoendelea na hususani za Afrika zimejitahidi kutimiza ahadi zake.

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, walikutana katika mkutano wa Tano wa Kilele ambapo kwa siku mbili, walijadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu suala zima la ufadhili wa maendeleo, utekelezaji wake na mwelekeo wa baadaye. Majadiliano yaliyojikita katika taarifa za makubaliano ya mikutano ya kimataifa Monterrey na Azimio la Doha.

“ Afrika kwa upande wake imejitahidi sana kutimiza karibu mambo yote iliyoahidi katika mikutano hiyo miwili. Mambo hayo tuliyoahidi na ambayo ninapenda kuyarudia tena leo hii, ni pamoja na kumiliki ajenda zetu za maendeleo, ukusanyaji wa mapato yetu ya ndani, sera na mipango mizuri ya kukuza uchumi, utawala bora , utawala wa sheria, amani na utulivu” akasema Balozi Sefue.

Akasema matokeo ya utekelezaji wa ahadi hizo ni ya kutia moyo sana. “ tunaamani tungeweza kufanya vizuri zaidi kama tungepata misaada zaidi tuliyoahidiwa kutoka kwa washirika wetu” akasisitiza Balozi Ombeni Sefue.

Katika hotuba yake hiyo ambayo ilipokelewa vizuri na kupongezwa na baadhi wa wajumbe wa mkutano huo, akiwamo mwakilishi kutoka Ubalozi wa Marekani katika Umoja wa mataifa. Balozi aliongeza pia kwamba hata kwa upande wa ukuaji wa uchumi, Afrika imekuwa ikifanya vizuri licha ya vikwazo mbalimbali vikiwamo vya mifumo pendelevu na baguzi ya uchumi wa soko na biashara.

“Afrika tumejitahidi sana, licha ya kwamba hivi sasa dunia inakabiriwa na mdororo wa uchumi, uchumi wetu kwa baadhi ya nchi unakuwa kwa kiwango kinachoridhisha. Na ukuaji huu ingawa si mkubwa sana unatokana na mahitaji makubwa ya bidhaa kutoka nchi za afrika kwenda katika nchi zinazoinukia kiuchumi” akabainisha mwakilishi huyo wa Tanzania.

Akizungumza utekelezaji wa ahadi ambazo zimetolewa na nchi wa hisani kabla hata ya mdororo wa uchumi na ambazo hadi sasa bado hazijatekelezwa.

Balozi Sefue anasema “ wakati kiwango cha misaada kwenda Afrika kiliongezeka kwa asilimia 4 mwaka 2010, bado kuna changamoto ya kufikia utekelezaji kamili wa ahadi za maendeleo zilizotolewa katika mikutano ya kimataifa ukiwamo ule wa G8. Tunahitaji kuimarisha ubora wa kiwango wa misaada hiyo na uhakika wa upatikanaji wake” anasititiza na kuongeza

“ Mdororo wa uchumi na matatizo ya kifedha yanayozikabilia nchini zilizoendelea kisiwe kisingizio kwenu ( nchi zilizoendelea) cha kuto timiza ahadi zenu mlizoahidi kuzisaidia nchi zinazoendelea, tumetimiza ya kwetu na nyie timizeni yenu. Tunawashukuru wale wote waliotangaza nia zao za kutekeleza ahadi zao na tunawahimiza wengine kufanya hivyo”.

Aidha Balozi Sefue amewaeleza wajumbe wa mkutano huo ambao pia uliwashirikisha baadhi ya mawaziri kutoka nchi kadhaa na ulifunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro.

Anasema nchi nyingi za Afrika zinafanya jitihada kubwa ya kuimarisha uzalishaji na kuhimili ushindaji katika uuzaji wa bidhaa zake .

“ Nchi za afrika zinataka kufanya biashara miongoni mwao ili kujikomboa na umaskini. Lakini wakati misaada ikiongezeka kwa upande wa biashara katika miaka michache ilioyopita, mfumo mzima wa biashara ya kimataifa bado si mzuri. Afrika inaendelea kuumia kiuchumi kutokana na mifumo mibaya na isiyo sawa ya sheria za biashara” akabainisha.

Akasisitiza kwa kusema, kutokana na ubaguzi katika mfumo zima wa biashara ya kimataifa,mchango wa bara la Afrika katika biashara ya kimataifa kwa mwaka 2009 ulikuwa ni asilimia 3.1.

“ Tulitegema mazungumzo ya Doha, yaliyotarajiwa kukamilisha mwezi disemba mwaka 2005 na ambayo yamekwama tangu mwaka 2008 yangeweza kutoa mwelekeo na matokeo mazuri lakini imekuwa kinyume chake.

Katika hatua nyingine, Balozi Ombeni Sefue, amesema Afrika inahitaji kusaidiwa katika kuweka mikakati na mipango bora ya kuimarisha vyanzo vyake vya mapato ili kufidia kile kinachopunguzwa na wahisani.

“Mdororo wa uchumi umeiadhiri Afrika vibaya sana , na hasa katika uwezo wake wa kukusanya mapato yake ya ndani. Na kwa sababu hiyo tunaomba kusaidiwa katika kuimarisha uwezo watu wa kitaifa katika kukusanya mapato ya ndani” akasihi Balozi Sefue kwa niaba ya Afrika.

Aidha akaomba pia kufutiwa madeni kwa nchi zile ambazo hazijanufaika na utaratibu huo. Ili pamoja na mambo mengine ziweze kunufaika na ufutwaji wa deni hilo kwa kuboresha na kuimarisha uchumi wao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. Tatizo ni kwamba hata ninyi wadogo hamtimizi ahadi zenu kwa wananchi wenu, mnatukatisha tamaa sisi wakubwa, Ok! inakuwa kama tunatia maji kwenye gunia.

    ReplyDelete
  2. Na mimi nilitaka kusema hivo hivo; watimize ahadi wana deni na sie? Nyie wanasiasa ndo mtimize ahadi za wapiga kura wenu; hao so called wakubwa hatuwajuhi sie wala hatukuwapa kura. Okay!

    ReplyDelete
  3. Hongera Balozi. Wape maneno yao!

    ReplyDelete
  4. haoni boritu lake anazungumzia vibanzi vya wengine....

    ReplyDelete
  5. Punguzeni rushwa, na Muwe wawajibikaji wakweli mtapewa hiyo misaada. Kwanza misaada ya nini? mi nafikiri tuachane na misaada ya kifedha tuombe misaada ya kiufundi tu kama waalimu na maprofessor kutusaidia elimu yetu na sisi tuweze kutumia mali asili zetu kwa manufaa yetu.

    ReplyDelete
  6. balozi msanii, mabadiliko yaanze chinikwanza. Wao wamewaona corrupted ndio maaana wanasepa. Kwani hawana akili watupe manoti yao watu wazidi kuengeza wake!!

    ReplyDelete
  7. kitu kikubwa uwaeleze viongozi wa Africa wawe na utawala bora,waache rushwa wizi na ub inafsi.Toka tunazaliwa tunaona USAID,DANIDA,nk wakitoa pesa mpaka leo zinaingia mifukoni mwa watu binafsi.Msitafute kisingizio cha kukosha wizi wenu

    ReplyDelete
  8. Hongera mdau wa kwanza na wa pili kwa kuliona hili. Kama hawa wadogo wangetimiza ahadi zao wala wasengihitaji msaada wa wakubwa.

    ReplyDelete
  9. Mdau wa 7 hapo juu, na wengine mliotangulia ni kweli ilikuwa hivyo wahisani wamekuwa wakitoa misaada inaingia matumboni mwa watu, Huyu huyu Balozi wetu Tanzania ktk UN Ombeni Sefue aliliona hilo akafanya jitihada na zimezaa matunda kama mlivyoona Sweden safari hii wametoa msaada kwa TZ lakini kupitia UN ,sio moja kwa moja Serikalini kwa wachakachuaji na hela zimeelekezwa zaidi kukata makali ya umaskini!

    ReplyDelete
  10. Mdau wa 9 hapo juu Unajua raha ya msaada kupitia UN kunakuwa na strict coordination kwa vile wale wana MILLENIUM DEVELOPMENT GOALS (MDG), huwezi hamisha hela za mipango yao ukaingiza ktk siasa au chama fulani, sasa kwa msingi huo hela zao ni za moto hazi chakachuliki kirahisi!

    ReplyDelete
  11. Nafasi hiyo hiyo ya kwenda na UN-Millenium Development Goals (MDG) ndio Rwanda imeitumia na sasa inaelekea kutoka kimaendeleo!

    ReplyDelete
  12. inabidi nasi tuwe na mikakati ya kujitegemea kwani kutegemea misaada kutoka nje ni ishara mojawapo ya udhaifu wa matumiz ya rasilimali zetu,naamini tukijipanga sawasawa tunaweza tukajitegemea huko baadae lakini tuanze mikakati hiyo sasa,na tuhakikishe kinachopatikana kinatumika ipasavyo ktk maendeleo

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...