Kwa miaka kadhaa nimekuwa nikisikia neno China China, hili linamaanisha kila kitu, siku za hivi karibuni neno hili limehusishwa sana na ufake,kutodumu nk. Binafsi nikiwa fans wa made in China, iwe kwa kukosa njia nyingine au urahisi ninaweza kusema machache ambayo nadhani yatakuwa na msaada kwa wengine. Nikiwa Mtanzania niliyeishi China kwa miaka zaidi ya sita, ninapenda kushare nawe mambo machache ambayo wafanyabiashara hawawezi kukuambia kuhusu Made In China.

1. Kuna Vitu China ni Ghali kuliko hata Tanzania

Unaweza kusema kivipi, ila ni kweli, ukiwa Uchina na unataka kupata kitu chenye ubora mzuri, ni dhahiri unatakiwa kulipia zaidi. Binafsi nimekuwa nikipokea simu nyingi mno toka nyumbani wakitaka kunitumia pesa niwanunulia komputa nk. Ukienda sokoni kompyuta ya kawaida ambayo ni bora inaanzia yuan 2000, tena hiyo ni ile ya kiwango cha chiiini kabisa, ila ukiipeleka kwenye dola ni kama mia tatu kadhaa, ukijumlisha na utumaji mpaka inafika nyumbani ni kama dola mia tatu na nusu au mia nne. Hapo ndio unapata kompyuta ya kawaida mno kitu ambacho kwa mtanzania wa kawaida lazima aone ghali kwani akienda sokoni anaona DELL kibao kwa laki tanotano.

2. China kuna bei tatu

 Kama umewahi kufika Uchina ni dhahiri utakubaliana nami, ukienda dukani unaulizwa unataka ipi, Hao(nzuri), Yiban(Ya kawaida) Shuihuo(Dump aka fake). Kwenye kila kundi ubora ni tofauti,ingawa kwa macho zote zinaonekana sawa. Pindi ununuapo ni lazima uhakikishe unapata kulingana na mapenzi yako. Hongera kwa wafanyabiashara WENGI wa Kichina ni kuwa, atakuambia. Hii ni nzuri na hii ni mbaya. Pia hata kwenye hiyo nzuri nayo kuna makundi yake humo ndani.hehe. Hivyo kabla hujanunua ni lazima ujue nini unataka na lazima muelewani na muuzaji.

3.Kitu cha 100Yuan si cha 80Yuan.

  Kwa wale waliowahi kukutana na Watanzania au wageni kadhaa walioishi Uchina kwa miaka mingi watakubaliana nami, jinsi muda uliokaa China unavyooongezeka ndivyo uwezo na ari ya kupatana bei inavyokwisha. Binafsi ni mara chache mno ukaniona ninapatana bei. Hii ni kwa sababu tayari wanafahamu hili. Kuna siku niliambatana na dada mmoja kununua simu, alipofika kule simu aliyopewa ilikuwa ni ya mia nane, akazidi kupatana (pianyipianyipianyi) basi mwisho yule mchina akakubali, yule dada akasema nachukua hii, mchina aliwaka kama kawekwa petroli. Akibwabwaja "haiwezekani,hii ni ghali nk) mwisho ikabidi mdadaa aongeze pesa.

4. Kuna maduka yanayojulikana kwa ufeki na ubora.

 Kila sehemu wana mila na tamaduni zao, ukiwa China, kama unataka kupata kitu chenye hadhi na ubora mzuri basi unashauriwa ukanunue kwenye maduka makubwa, kwa mfano unataka kununua TV ya nyumbani basi nenda kwenye maduka kama ya Sunning, Gomao,carrefour nk kwani mengi ya maduka haya yana mkataba wa ubora na bei na serikali. Kuna kipindi Carrefour walipandisha bei kiholela kwa baadhi ya vifaa vyao, walipigwa faini na ikawacost mno. Binafsi  mwaka jana nilinunua simu ya mkononi "Nokia", wiki iliyopita kilitokea kitendo kilichonisukuma kuandika makala hii. 
Nikiwa barabarani kwenye pikipiki simu yangu ilidondoka, nikasikia mchina akiita "simu imedondoka" nikasimama na kuangalia kumbe ni simu  yangu. Kwa bahati mbaya ilikuwa katikati ya barabara hivyo sikuwa na cha kufanya zaidi ya kuiangalia ikikanyagwa na basi la abiria, baada ya lile basi kupita taa nyekundu ikawaka na nikakimbia kuangalia masalio ya simu, nikaona kioo kimevunjika, nilipoishika nikaona ukiondoa kioo hakuna kingine. Niakajaribu kupiga simu ikawa inaita bila matatizo. Kesho yake nikaipeleka kwa wenyewe Nokia, wakaiangalia wakasema ukiondoa kioo hakuna tatizo. Ni kweli nimebadirisha kioo na sasa inadunda  bila wasi.

5. Nokia si sawa na NokIa, pia Smsung si Sunsung.

  NImekuwa nikisikia na kuona watu wengi wa nyumbani wakitumia simu wanazoziita Nokia ya Mchina, au Sumsung ya Mchina, hakuna kitu kama hicho huku. Wengi wanaotengeneza hizo simu ni viwanda vidogovidogo ambazo ubora wake ni hafifu mno. Wengi wamekuwa wakiongopewa kuwa inaitwa hivyo kwakuwa imetengenezwa China. Wafanyabiashara wengi wamekuwa wakijilimbikizia faida kwa kununua simu hizo kwa bei ya chee halafu kuwaongopea Watanzania. Chukulia mfano simu ya Nokia E72i inauzwa kuanzia 1800 hadi 2000yuan. Ila kwa zile mbofumbofu aka NoCia(NokIa) inauzwa kwa 500Yuan. Simu hizo sio tu hazina ubora bali pia ni hatari kwa afya yako kwani wakati wowote inaweza kukulipukia, inakulisha mionzi ya ajabuajabu nk.  

 Hayo ni machache tu ambayo leo ninapenda kushare nanyi, kama una maoni, upinzani na mengineyo karibu kwa maoni. BOFYA HAPA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 24 mpaka sasa

  1. SAWA KABISA , TUMEKUPATA.

    ReplyDelete
  2. mie hata sijaelewa unamaanisha nini manake umeongelea vitu feki vya kichina na ukaishia kusifia sifia,lakini hata hivyo mimi situmii vitu vya kichina,na nijuavyo mimi kama kuna vitu vya kichina bora basi ni vichache mno vingine vyote ni uchafu,ila hata hivyo nakushukuru kwa kuweza kuweka wazi kwamba simu nyingi za kichina zina madhara kwa afya ya wanadamu,simu moja sipika tano,mziki mnene,ya chuma,kubwa ,sio tu double line zingine unaweza weka hata line kumi,zina bia,soda,sipea za baiskeli,kuna brututh,kamera nne,vipaza sauti,visheti ,pilao n.k.,china china china ovyoooo!!!!

    ReplyDelete
  3. Ni kweli kabisa Mdau wa China.

    Kwa sasa ni vigumu sana kuagiza kitu kutoka Marekani au Ulaya ukakuta hicho kitu ni made in US ,Made in Canada/ Fabrique Du Canadien au Made in Italy, Made in Switzerland, Made in Germany,Made in France.

    Hivi sasa nchi za Magharibi karibu bidhaa zote zinazalishwa nchini China!

    Isipokuwa Magharibi wanadhibiti sana Ubora wa bidhaa kwa daraja kama ulizosema hapo juu.

    ReplyDelete
  4. Wacina Noomaaaaaa!! hadi MAKALIO fyeki!

    Wachina watatumaliza wallah!

    ReplyDelete
  5. Inaelimisha!

    ReplyDelete
  6. Asante mdau..Vipi kuhusu nguo..kufua mara moja tu rangi hiyoo.Swali..Kwa hiyo serikali ya CHINA inawaruhusu hawa wenye viwanda visivyokidhi hadhi na wanalipa kodi?

    David V

    ReplyDelete
  7. Mdau unayesema hujaelwa anachosema hujui China kabisa!. Dunia nzima inatumia China,yaani ni hela yako tu.Kama wewe ni Mtz na huna hela ya kununua vilivyo bora kutoka China na wala huna uwezo wa kudhibiti quality utapata unavyostahili.Ila ukiwa Mmarekani au Mswede na ukiwa na uwezo wa kununua vilivyo bora na ukiwa na uwezo wa kudhibiti quality wakati wa uingizaji, utapata quality kutoka China. Ni wewe tu kama nchi/mwananchi. Wewe upo kundi lipi?

    ReplyDelete
  8. @anonymous 2 , kama hujaelewa anachozungumza. rudi shuleni.... Asante mdau kwa kutupa habari muhimu

    ReplyDelete
  9. NASHUKURU TBS KWA KUANZISHA MKAKATI WA (PVOC) UTAKAOANZA KUTUMIKA FEBRUARY MOSI. MUAGIZAJI WA BIDHAA ATAKIWA KUWA NA CERTIFICATE KUTOKA SGS AU INTERTEK AU BEARAU VERITAS AMBAO NI WAKAGUZI WA BIDHAA ILI KUJUA UBORA.
    UTARATIBU HUU UPO KENYA, NA BAADHI YA NCHI ZA AFRICA. LABDA ITASAIDIA TANZANIA KUTOKUWA DAMPO LA FEKI GOODS FROM CHINA.

    ReplyDelete
  10. mdau umenena.
    Mimi nimetumia simu feki na nzuri za china. Mfano, moja la laini mbili niliambiwa ahaiwezekani kutumia majira ya baridi ya ulaya, ilidumu miezi sita, baadae, ikatapika! haya sasa ninayo yenye laini nne, inazima kila wakati..lakini la zaidi ni kuwa kama unataka cha quality nzuri unapata ila utalipa hela zaidi.Kuna duka la bei mbaya London, Harrods' kuna vitu vya mchina. Mimi niliagiza in-car video za wanangu kwa gari ya mjerumani, zilipifika ni made in china..kwa hiyo vya quality nzuri na mbaya utapata, ila bei ndio tofauti..kwa maneno mengine, mdaualiyekandia atikali hii, hakuelewa uliposea, kitu chayuan 100 sio cha yuan 80, lipa mia upate quality nzuri, 80, ukadolole!
    ahsante sana mdau..

    ReplyDelete
  11. Ukweli yaliyoelezwa ni sahihi. Mimi nipo China mwaka wa tatu sasa. China kuna vitu kwa kila daraja. Wewe kama pesa yako ni kiduchu utapata kwa thamani ya fedha yako. Na hivyo vya bei poa ndiyo wanachukua wafanyabiashara wa Tanzania na kuja uza kwa bei kubwa. Huyo mdau anyesema kuna simu ina laini 10 huyo anaongea kwa jazba mimi sijaona simu yenye laini 10, zina bia n.k. Inaonyesha huyo hata ABC za elektroniki ni sifuri. Huwezi kuweka kitu cha maji maji kwenye simu ikabaki nzima wakati ikitumbukia kwenye maji unashauriwa kuizima haraka na kutoa betri mpaka itakapokauka. Ni vyema kama huna hoja ukakaa kimya badala ya kuandika maneno ambayo yanakuonyesha kuwa una uelewa mdogo. Huyo mdau ni vyema akajua kuwa hivyo anavyotumia eti vimetengenezwa UK, USA n.k. vinatengenezewa China. China hivi sasa ni kiwanda cha dunia. Nchi za Ulaya na Marekani wana viwango vya ubora na wana watu wao kwenye viwanda hivyo wanaosimamia ubora tofauti na nchi zetu kama Tanzania. Wao huruhusu tu vitu viingie hata kama havifai kwa afya ya binadamu sababu ya rushwa na kutowajibika kwa wanaohusika na kuangalia ubora. Hivyo usilaumu vitu vya China laumu nchi zetu kutokuwa na watu waaminifu wanaosimamia ubora wa vitu vinavyoingia. Hapo ndiyo ujue rushwa ni mbaya na adui wa haki. Mdau wa Beijing.

    ReplyDelete
  12. WALE NI WAAMINIFU SI KAMA WASWAHILI. wafnaya biashara wa kiswahili anataka shida zake zoooote ziishe kwa kuuza kitu kimoja hata kama ni feki. Anasahau kuwa akishauza na biashara inakuwa imeishia hapo

    ReplyDelete
  13. Ukweli ndiyo huo mdau. UK wanatumia made in China, halafu mbongo unaenda kariakoo unataka kitu made in UK, au Original! Ubaya wa Bongo ni kwamba utatakchoambiwa feki, ni kweli feki na utakachoambiwa Oringinal nacho ni feki!...Fekifekifeki, tena sio lazima iwe SØNY, hata kama ni SONY hivyohivyo!

    ReplyDelete
  14. Kwa ufupi wafanyabiashara wetu wananunua hivyo vya bei ndogo wanatuuzia kwa bei kubwa. Bongo hata makampuni ya simu wanauzia watu simu feki. Hapa UK unapewa simu bure ya iPhone na Blackberry isipokuwa tu ulipie kwa mwezi bill yako. Bongo bandwidth TTCL wanatuibia na ndiyo kampuni ya serikali!!

    ReplyDelete
  15. Ni kweli kabisa kwa sasa kila kitu ni made in china ila vinatofautiana ubora ila china mpo juu chezea tchin chon tchu china weee

    ReplyDelete
  16. Tatizo watanzania wengi tunapenda vya dezo kuliko uhalisia wake.Wachina ni wabunifu hakuna mfano,wamewapata waafrika kufanya biashara zao na vile vile waingereza wanafanya biashara nao na kote huko biashara inaenda isipokuwa Afrika viwango hakuna kwa sababu ya bei ndogo.Mimi nipo naishi uk vitu vingi sana vya nyumbani,Tv,radio,jokofu,pasi,mashine za kuoshea nguo na vyombo,na matoy ya watoto na wakubwa vyote vinatoka china.Tofauti ni kwamba uk ubora ni mbele wakati Tanzania ni bora kinafanya kazi na bei cheee.Hupo hapo.Wachina nawapenda sana ukiwajua utafaidi na ni wachapa kazi hakuna mfano.

    ReplyDelete
  17. OK BWANA HABARI ZA U-CHINA. SASA TUSHAJUA ULIENDA CHINA UMERUDI UNATUTAMBIA...THETETETETEHHHHHHH
    MMATUMBI BWANA ASIPANDE NDEGE, KOSA. MPAKA SISIMIZI ATAMWAMBIA

    GEORGE LUCAS

    ReplyDelete
  18. Mwandishi wa habari hii atakua anafanya biashara ya kuuza vitu vya kichina china!

    ReplyDelete
  19. Mdau namba mbili uliyesema hujaelwa nazani we ni bonge la kiazi, hujui bidhaa karibia zote za electonics na nguo zinatoka china ila zinatofautiana ktk grade ya utumwaji kutoka bara moja hadi jingine.. Kwa taarifa yako hata hiyo Apple inatengenezwa huko sema kwalite ya product inategemea bara gani inaenda..

    ReplyDelete
  20. wadau kwa sisi tuliopo marekani asilimia kubwa ya vitu tunavyonunua hapa ni madeni china. vitu hivi vyote vinaubora wa juu kwani viwanda vinamilikiwa na wamarekani wenyewe waliovipeleka china kwa chipu leba. hivyo ukinunua computa na electronics karibu zote ni kutoka china. kwa kifupi ukitaka kununua kitu bora nunua hapa usa hata kama kilitengenezewa china usiwe na magutu ili mradi ununua katika maduka yanayo kubalika kama vile office depot, Best buy, home depot, sams club nk.
    -Kiongozi

    ReplyDelete
  21. Nadhani watu wengi mnakosea sana kudhania dhania mimi naona cha msingi ni unanunua bidhaa ya kampuni gani na sio imetengenezwa wapi. Mfano Apple Ipod imeandikwa made in China hiyo ina maana assembling imefanyika China na sio kwamba Ipod ni bidhaa ya China. Ipod ni bidhaa ya Aple Computer ya USA. Design ya bidhaa za USA an UK wanafanya wenyewe ila production au assembling ndio inafanyika China kwa usimamizi wa viwango vyao ili kushusha gharama za uzalishaji. Kibaya ni kwamba China kuna "sido" nyingi sana huiga bidhaa halisi na ndio hizo zinazonunuliwa wafanyabiashara wa Bongo na kuuziwa madukani.

    Mzozaji

    ReplyDelete
  22. Mdau umenena na unaifahamu Vyema sector ya bidhaa za Cina. Bidhaa ni kwa uwezo wako wa fedha ndio mfumo wa Cina. Hata ukitaka za America, Euro,na kwengine hapo Cina utavipata kwa viwango bora na kuzalishwa Cina.

    ReplyDelete
  23. USHINDANI WA M CHINA USIO NA MPINZANI
    -------------------------------------
    MABEPARI WA DUNIA WAMESHINDANA SANA KATIKA BIASHARA LAKINI MCHINA AMEKOSA MPINZANI KWA HAYA HAPA CHINI:

    1.DAWA YA KUKUZA MAKALIO;
    Mtumiaji akijichanganya wakati wa kupaka dawa ikizidi upande mmoja basi kalio moja litakuwa kubwa kuliko lingine!

    Wapo wanaotumia dawa wakabaki hivyo hivyo, na wengine inawakataa wanaporomoka baada ya miezi kadhaa wanarudi wembambaaa vimbau mbau kama mwanzo!

    2.Simu ya MCHINA ina mlio (Ring ton ya makelele saana, haina siri ,wakati wa kuizima nibalaaa tupu kwala kachaa pwiiii....
    Baadhi ya watu wanadai ndio SIMU ya kuchukua unapoenda kuposa shamba maana ilivyo kubwa na manjonjo watakuona ni Bosi huko ukweni!

    3.VIJANA MABAUNSA (WATUNISHA MISULI) M CHINA HAKUWATUPA:
    Wengine dawa hukubali na wengine huwakataa ,unakuta mtu anavimba kifua kama TONGWA NA MATAKO YANABAKI KAMA AMEPIGWA PASI!, UTAFIKIRI DEREVA WA TREKITA AU TRENI!

    ReplyDelete
  24. hwang ho balaa,,,hata bamia watakutengenezea ukitoa oda!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...