Uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) unafuraha kuwatangazia kuwa huduma za safari za abiria kwenda Kigoma kutoka Dare s Salaam zitaanza tena hapo siku ya Ijumaa Februari 10, 2012 saa 11 jioni kama kawaida. Uamuzi hu umechukuliwa baada ya kuwa na uhakika eneo korofi kati ya Godegode na Gulwe mkoani Dodoma katika reli ya kati limeimarika kwa sasa.

Hivyo basi wananchi kwa ujumla wanaarifiwa kufika katika stesheni husika za reli ya kati kuanzia leo Februari 7, 2012 kukata tiketi kwa safari ya kutoka Dar hadi Kigoma moja kwa moja.

Kuanzia Januari 24, 2012 huduma hiyo ya usafiri wa treni ya abiria ilikuwa inaanzia Dodoma ambapo abiria wa kutoka Dar es Salaam na mikoa ya jirani walibidi kusafiri kwa mabasi hadi mjini Dodoma ili kuendelea na safari kwa treni hadi Kigoma.

Halikadhalika Uongozi wa TRL unawaarifu wasafiri na wananchi kwa ujumla kuwa treni ya leo Februari 07, 2012 kutoka Dodoma kwenda Kigoma imesogezwa mbele kwa siku moja hadi kesho Jumatano Februari 08, 2012 saa moja usiku. Hali hiyo imetokana na ratiba ya usafiri huo kuvurugika baada ya kutokea ajali ya treni ya mizigo katika eneo la stesheni ya Kigwe mkoani Dodoma usiku wa kuamkia Jumamosi Februari 05, 2012.

Kutokana na kazi ya kuondosha mabehewa na kukarabati njia kuchukua muda mrefu, treni ya abiria ya Jumamosi kwenda Kigoma iliahirishwa hadi usiku wa Jumapili Februari 06, 2012.

Uongozi unawashukuru abiria na wananchi kwa ujumla kwa uvumilivu wanaouonesha pindipo huduma zetu zinapokwazika kwa sababu zilizo nje ya uwezo wetu!

Imetolewa na Ofisi ya Uhusiano kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi K.A.M Kisamfu
Imesainiwa na:
MIDLADJY MAEZ
MENEJA UHUSIANO- TRL
DAR ES SALAAM
FEBRUARI 07, 2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Kwani mkitumia picha ya mzawa??? Acheni ushamba!

    ReplyDelete
  2. wacha ubaguzi wewe mdau kumbuka tupo 2012 sasa

    huku ughaibuni kuna matangazo mengi sana wameweka picha za watu tofauti wakiwemo watu weusi

    tutabakia na hela za madafu kwa ujinga wetu roho mbaya chuki ubinafsi ubaguzi ulimbukeni na ushirikina tuachane na kubagua watu

    kila siku utasikia ooh mwarabu mara ooh muhindi hivi mbona tunaongoza kwa ubaguzi?

    mbona wajomba zenu wamekimbilia ughaibuni na hawabaguliwi kama mfanyavyo nyinyi?

    mtu kazaliwa tanzania ni mtanzania acheni mambo ya ukabila kila siku jambo la muhindi au mwarabu lazima liongelewe kumbukeni hao ndio waliowafungua macho kabla ya mzungu

    hao ndio waliowawekea maduka tokea enzi hizo mkapata huduma mpaka mmekuwa wakubwa sasa mnajuwa internet ndio mnajifanya mmefunguka macho.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...