Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali yake itahakikisha kuwa mikataba ya uzalishaji gesi asilia iliyogunduliwa na makampuni binafsi nchini inawanufaisha ipasavyo wananchi wa Tanzania.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ambako gesi asilia imegunduliwa ama inatafutwa katika Bahari ya Hindi dhidi ya tishio ya uharamia wa Kisomalia.

Rais Kikwete amesema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Kampuni ya British Gas International (BGI) ukiongozwa na Sir Robert Wilson ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya British Gas (BG) Group ya Uingereza ambayo ni kampuni mama ya BGI.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jioni ya jana, Jumatatu, Februari 20, 2012, Ikulu, mjini Dar es Salaam, Rais Kikwete aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa Serikali yake itahakikisha kuwa Mikataba ya Pamoja ya Uzalishaji – Production Sharing Agreement (PSA) ambayo Tanzania itaingia na makampuni binafsi yanayotafuta ama kugundua gesi asilia nchini italenga kunufaisha pande zote mbili, yaani wananchi wa Tanzania na wawekezaji.

“Ninataka kuwahakikishieni kuwa tutahakikisha kuwa mikataba tutakayoingia ya uzalishaji wa pamoja – PSA- itawanufaisha wananchi wa Tanzania na vile vile wawekezaji kwa namna ambayo kila upande utajiona unanufaika, “ amesema Mheshimiwa Rais Kikwete katika mazungumzo hayo yaliyochukua zaidi ya saa moja.

Katika mazungumzo hayo, Sir Robert Wilson alimthibitishia Mheshimiwa Rais kuwa kampuni yake imefanikiwa kugundua kiasi kikubwa cha gesi asilimia katika visima vitatu vilivyochimbwa mwaka juzi na mwaka jana katika Bahari ya Hindi, kikiwamo kisima cha kwanza kabisa katika Tanzania kuchimbwa kwenye kina kirefu zaidi cha maji (deepwater well).

Sir Robert Wilson alimwambia Rais Kikwete kuwa kampuni yake iliwekeza dola za Marekani milioni 500 katika utafutaji gesi nchini Tanzania mwaka jana na kuwa itawekeza kiasi hicho hicho kwa mwaka huu.

Hata hivyo, Sir Robert Wilson ambaye alifuatana na ujumbe wa watu saba akiwamo Balozi wa Uingereza katika Tanzania, Bibi Diane Corner alimwambia Rais Kikwete kuwa katika nusu ya pili ya muongo wa sasa, BGI itaanza kuwekeza kiasi kikubwa zaidi, kiasi cha kati ya dola za Marekani bilioni 10 hadi 20, katika shughuli hiyo na katika uchumi wa Tanzania.

Sir Robert Wilson amesema kuwa kiasi hicho kitakuwa kikubwa mno kiasi cha kwamba Serikali ya Tanzania inatakiwa kuanza kujiandaa sasa kwa ajili ya uchumi wake kupokea kiwango kikubwa kiasi hicho cha fedha kwa wakati mmoja.

Sir Robert Wilson pia aliitaka Serikali ya Tanzania na BGI kuchukua hatua za kukabiliana kwa pamoja na changamoto ambazo zinakabili utafiti, utafutaji na hatimaye uzalishaji wa gesi asilimia katika Bahari ya Hindi.

Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na tishio la uharamia wa Kisomalia, kulazimika kwa makampuni binafsi kutumia walinzi wao kujihami dhidi ya uharamia huo, kiasi kikubwa cha uwekezaji kitakachoingizwa katika uchumi wa Tanzania katika miaka michache ijayo kupitia gesi asilimia na uwezekano wa kutokea mivutano ya kimikataba kama ilivyotokea kwa makampuni ya madini.

Rais Kikwete amemhakikishia Sir Robert Wilson kuwa Serikali yake itachukua hatua stahiki kukabiliana na changamoto hizo. Mazungumzo hayo ya Rais Kikwete na ujumbe huo wa BGI yalihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Mustafa Mkullo na Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa William Njeleja.

BGI iliingia katika Tanzania mwaka jana kwa kununua asilimia 60 ya hisa za kampuni ya Ophir Tanzania Limited ambayo tokea miaka ya 2005 na 2006 iliingia katika mikataba ya PSA na Serikali ya Tanzania na Shirika la Mendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa ajili ya ufatutafuji gesi katika vitalu vitatu katika Bahari ya Hindi.

BG Group ni moja ya makampuni makubwa zaidi katika biashara ya nishati duniani ikiwa na shughuli katika zaidi ya nchi 25 duniani. Ni miongoni mwa makampuni 15 makubwa zaidi katika Uingereza ikiwa na mtaji wa kibiashara unaokadiriwa kuzidi dola za Marekani bilioni 70.

Ingawa Tanzania imepata kugundua gesi katika maeneo ya Songosongo na Mnazi Bay lakini visima hivyo ni visima vya Serikali na BGI inakuwa kampuni binafsi ya kwanza kutafuta na kugundua gesi katika Tanzania.

Mwisho.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
21 Februari, 2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. Hii ndiyo tunaita SIASA kwenye UCHUMI.
    Je kwenye madini hali ikoje????

    ReplyDelete
  2. When have any citizens of any nations, ever benefited from ones country natural resource!!!

    ReplyDelete
  3. ahadi kama hii inapaswa kupongezwa na wabongo wote kwani ukiangalaia NIgeria na Angola, watu wao bado maskini au nchi zenyewe zimeendela na umaskini kwa vile hakuwa na muono kama huo wa Marehemeu Mwalimu, kuwa mali asili ni ya taifa na inufaishe taifa. Bravo JK. mfano wa Equatorial Guinea ni wa kuigwa, kwa wale waliofuatilia World Cup kule,mambo mswano kwa wezenzetu, sababu ya mafuta

    ReplyDelete
  4. asilimia kubwa ya mabilioni hayo ya wawekezaji yataishia kurudi ulaya na marekani kwa kuwa watekelezaji wengi wa mradi huu watakuwa makampuni kutoka nje. Ni ukweli kuwa hakuna makampuni ya kitanzania yaliyokuwa na uwezo wa ku-supply drillers, shafts,heavy duty compressors, rigs, hydocarbon engineers, etc. Alex bura dar

    ReplyDelete
  5. Utahakikishia kutokea wapi? Uingereza au?

    ReplyDelete
  6. Nakubaliana kabisa na mdau wa 4 hapo juu.

    Pia naongeza kuwa mafuta ni shetani katika umbo tofauti. Nawaambia ni bora tungebaki na madini tu. Japo ni ishara ya pesa, mafuta yatatutafuna, watakaotutafuna tutawajua na watajiweka wazi, na hatutaweza kuwafanya chochote (hatima yake sote tunaijua).

    Vile vile, Rais hata aseme nini, wanaodhibiti mafuta ni kikundi cha majitu fulani yaliyo juu ya serikali zote duniani. Hivyo Rais ndiye atakayedhibitiwa kwanza kisha wananchi wake. Wakitaka wanambadilisha fasta fasta tu. Mafuta ni kama nchi inayojitegemea hata kama yakiwa nchini mwako. Yana Rais wake na msululu wa viongozi wengine.

    ReplyDelete
  7. Mangapi yamesemwa na hayajatimizwa

    ReplyDelete
  8. kwanini serikali na watanzania hawawi na shares kwenye hizo shughuli ili wagawane faida kiukweli badala kupewa vijicenti. kwanini haya makampuni ya kigeni wachukuwe mikopo ambayo mara nyingi serikali nchio wanai guarantee wakati serikali na wananchi wanaweza kufanya hivyo pia. i wiwh nyerere angekua around asinge kubali kudanganywa.

    ReplyDelete
  9. Good initiative; I see a big benefit katika ajira as wildcats, madereva, waendesha mashine mbalimbali, wajenzi, etc., na ununuzi wa bidhaa za kiTanzania za kulisha visima/kampuni hizi, mfano, maji, chakula kama kuku, mchele, unga, matunda, etc, na pia industry zingine zinaweza kukomaa na kufaidika e.g. watengeneza mabuti, mafundi stadi mbalimbali, etc.

    Lakini yote hii nio lazima serikali iweke mazingira bomba ya kuwabana hawa wawekezaji walazimike kufanya hivi.

    ReplyDelete
  10. 100% confidence levelFebruary 22, 2012

    Thanks for attending my concern mr moderator.

    ReplyDelete
  11. bravo mr president,i hp we'll be benefited from this natural resource
    found.

    ReplyDelete
  12. AHSANTE RAISI!

    KABLA YA KUFIKIA LENGO HILO KWA GESI ASILIA INGEFAA TUANZIE KTK RASILIMALI ZINGINE AMBAZO FAIDA ZAKE ZIKO MIKONONI MWA WACHACHE AU ZINA VUNWA NA WACHACHE.

    ILI KUFIKIA AZIMIO HILO,

    Tuanzie kwanza mambo haya matatu:

    1.Tupige panga la Mshahara na Mafao ya bure wanayopokea Waheshimiwa Wabunge huku watu wa Kada zingine wakibaki patupu.

    2.Tuhakikishe sheria inakuwa JUU ya kila Mwananchi na Wahalifu wanawajibishwa.

    3.Tuwapige pingi kundi la watu wachache wanaoyumbisha nchi watu hawa wanahesabika kwa uchache pana hawa Vijogoo wanne hapachini
    ED,AC,RA,NK.

    HAO JAMAA WANNE WATAKAPO PIGWA PINI NDIO NCHI ITASONGA NA UWEZEKANO WA ASILIMALI ZINGINE NA GESI ASILIA KUWANUFAISHA WANANCHI UTAPATIKANA!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...