Kwa jina la Rahmani, Mola aso na mfano,
Naingia uwanjani, kwa beti kumi na tano,
Lengo langu si utani, wala mengi malumbano,
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Wakati wa kampeni,viwanja vya Tangamano,
Tulipokea ugeni, wa ‘bosi’ wa Muungano,
Akatutoa huzuni, Tanga mambo ni ‘mswano’,
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Viwanda kama Amboni, vilikuwepo zamani,
Mabasi na matreni, sambamba kuwa njiani,
Leo katiza relini, hata husikii honi,
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Tulikuwa na ‘Mbolea’, njia ya Raskazoni,
Wazazi waliponea, mkono kwenda kinywani,
Wapi kimepotelea, kiwanda hiki jamani?
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Mji watoa matunda, mkonge hata korosho,
Vipi ukose viwanda, ewe mwana wa Mrisho?
Muagize japo Pinda, afanye matayarisho,
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Tanga tunayo bandari, nzuri na ya kuvutia,
Meli zije kwa fahari, tupate pa kushibia,
Ukitupatia feri, Unguja twaenda pia,
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Bandari kuu ni Dar, ya Tanga imedorora,
Meli huko zimejaa, hadi yatia hasira,
Zinachelewa bidhaa, kuzitoa ni hasara,
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Reli ya kwenda Uganda, nayo naikumbushia,
Mbao huko zinakwenda, tatizo ni hiyo njia,
Vipi na mama Makinda, bungeni aigusia?
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Mazuri nayasifia, msiseme tu ni kero,
Mradi wa Milenia, Tanga kwenda Horohoro,
Bara bara yanyinyia, yashinda hata ya Moro,
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Na wale wawekezaji, nawakaribisha Tanga,
Mji wetu una maji, yeyote hawezi pinga,
Mzuri kwa ufugaji, uvuvi hata wa tenga,
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Tuna mawe kiomoni, na samaki baharini,
Machui na Maforoni, fukwe nzuri kama nini!,
Tafadhali wekezeni, Tanga ni nambari wani!,
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Tanga pia kuna chumvi, kaoneni Kisosora,
Twatengeneza majamvi, ila soko ladorora,
Twavua hata uduvi , na kuuza Makorora,
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Ninakuomba Kikwete, Rais wa Tanzania,
Ahadi zisiwe tete, Tanga tutakulilia,
Najua huwezi zote, japo mbili kazania,
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Tanga ni maendeleo, si kuja kurudi leo,
Tupatieni koleo, tufyatue pembejeo,
Kamwe hatutaki vyeo, ukoloni mambo-leo!
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Beti ninakamilisha, nisije nikawachosha,
Ujumbe nimefikisha, Mtanga nimejikosha,
Wakuu wasijebisha, eti sikuwakumbusha,
Nakumbushia ahadi, za viwanda kwetu Tanga.
Mwamgongo,
Mwenyeji wa Tanga
2 / Machi / 2012
This is good advise only if he knows... Good job for the author
ReplyDeleteSafi sana nimellipenda shairi hilo ujumbe wake muafaka
ReplyDeleteAMIIIIIN SWADAKTA!
ReplyDeleteMistari imetulia haswaa, TANGA ndio ingefaa iwe juu kimaendeleo zaidi ya Dar kwanza Bandari yake ni Natural na ina kina kirefu kuliko ya Dar.
Tanga ni ya Wajanja usisikie angalia Wazee wa Tanu ktk kupigania Uhuru Tanga imo iweje sasa ikawa Kisiwa cha Huzuni?
Duh Mwamgongo unatisha.Asante mkuu.Vina..mizani umenikumbusha mbali sana.Ujumbe umekaa vizuri mkuu.Somo la kiswahili linakuwa gumu kweli mashuleni sijui ni ufundishajia au vipi.Kidato cha nne mimi masomo ya Sayansi nilifaulu vizuri lakini kiswahili kikanipiga mweleka kiasi,mambo ya fasihi haya..fasihi simulizi
ReplyDeleteDavid V
nilisoma masiwani darasa la sita nikaondoka tanga sikurudi ndani ya miaka 15 niliporudi sikuhitaji mtu kunionyesha uchochoro nilokua napita kwenda shule yaani hakujajengeka kabisaaa,ni tofauti na nilipoondoka dar na kurudi baada ya miezi sita nikakuta pori limekua mlimani city
ReplyDeletenimepata hasira jamani, TANGA kunani???
ReplyDeleteUjumbe maridhawa, sasa sijui huyo mheshimiwa ataupata ili atekeleze japo mawili???
ReplyDeleteMuda wa kutoka hili shairi na uendaji wa chadema tanga unatia shaka!
ReplyDeleteIt does not matter kama ni chadema au ni nani lakini Habari Ndiyo hiyo...ahadi zilitolewa...zitekelezwe alah! Chadema...Chadema kivuli chenu mtakikimbia mpaka lini?
ReplyDeleteTanga kuna wachawi wa kurusha mapepo ya msukule.
ReplyDeleteWenyeji acheni mambo ya ulozi au wivu usio na maendeleo NA tanga itaendelea. Tanga kwetu mimi mdigo lakini nakuogopa sembuse mgeni. We we ukija na maendeleo wenzio wana kupiga vita kwa nini ana uwezo huu sasa kutaendelea kweli?
ReplyDeleteUliyenena kwa tungo, hongera nnakwambia,
ReplyDeleteYote kweli si uongo, ujumbe tawafikia,
Wamezidi 'longolongo', kura kianza lilia,
Wazitimize ahadi, mana ahadi ni deni!
Kwanza ahadi ni deni, ni wajibu timizia,
Kesho kwa MOLA MANANI, pia taziulizia,
Kuahidi mtihani, kuupasi timizia,
Wazitimize ahadi, mana ahadi ni deni!
Ahadi zao ni 'feki', kura zetu kivizia,
Ahidi tupiga jeki, ikulu wakiingia,
Kija 'wini' hawataki, madhila yetu sikia,
Wazitimize ahadi, mana ahadi ni deni!
Viwanda lihanikiza, kila unamopitia,
Mkoa ulipendeza, kwa shida hatukulia,
Wapi leo telekeza, au fika khatamia?
Wazitimize ahadi, mana ahadi ni deni!
Hao wote lao moja, mjengoni kiingia,
Kila kitu wanafuja, wakishajikusanyia,
Wakumbusha ipo haja, ahadi tutimizia,
Wazitimize ahadi, mana ahadi ni deni!
aisee umenifurahishaje maana shauri zuri sana yani na tamu haswaaaa hongera kwa kufikiria hichi kitu ila sasa ikiwezekana tafuta email ya mkuu i mean kikwete au box yake umtumie ili akae chini alisome lisiishie hapa kwenye blog sawa ndugu ubarikiwe snaaa
ReplyDelete