Msanii wa filamu, aliyebeba mapenzi makubwa ya Watanzania, Waafrika na dunia kwa jumla, Steven Charles Kanumba aliyefikwa na mauti ghafla Aprili 7, 2012, atazikwa kesho Makaburi ya Kinondoni, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Mazishi ya Kanumba, yamepangwa na kuratibiwa kwa kuzingatia heshima, umaarufu, mapenzi yake kwa watu na hadhi ya kimataifa aliyonayo, hivyo imetolewa fursa ya wengi kumuaga msanii huyo ambaye ni mwanamapinduzi wa tasnia ya filamu ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati.

Mpangilio wa ratiba na nafasi itatolewa kwa kila mtu mwenye kuhitaji kushiriki mazishi ya Kanumba, kufanya hivyo katika tukio la kihistoria la kumsindikiza ndugu yetu huyo kwenye maisha ya milele. Hivyo, wito unatolewa kwa kila mtu kujitokeza kwenye shughuli nzima.

RATIBA
Mwili wa marehemu Steven Kanumba utachukuliwa kwa msafara kutoka Hospitali ya Taifa, Muhimbili saa 2:30 asubuhi. Utapitishwa Barabara ya Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni ambako Misa ya kumuombea itasomwa pamoja na salamu mbalimbali kabla ya watu wote kumuaga.

Wito unatolewa kwa watu kujitokeza kwa wingi kuanzia saa 2:00 asubuhi, wakijipanga kando ya Barabara za Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi ili wautolee heshima mwili wa Kanumba wakati ukitolewa Muhimbili kwenda Leaders Club.

Saa 3:30 asubuhi, mwili wa Kanumba utapokelewa Viwanja vya Leaders, ukitanguliwa na mapokezi ya wazazi wake, viongozi mbalimbali wa serikali ambao juu yao kabisa atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal.

Saa 4:00, itakuwa ni muda wa kusoma Misa ambayo itachukua dakika 60, saa 5:00 kitakuwa kipindi cha salamu kutoka kwa watu mbalimbali.
Saa 6:00 mchana, ratiba ya kumuaga Kanumba itaanza mpaka saa 9:00 alasiri na baada ya hapo, utakuwa wakati wa kuusafirisha mwili kwa msafara kutoka Leaders Club mpaka Makaburi ya Kinondoni, msafara ukipita Barabara ya Tunisia, utakatisha Barabara ya Kinondoni kuelekea makaburini.
Saa 10:00 alasiri, mazishi yatafanyika kwa kufuata utaratibu wa imani ya marehemu.

Kamati ya Mazishi inatoa wito kwa watu watakaohudhuria shughuli ya kumzika ndugu yetu Kanumba, kuja na maua ili kumuaga kwa heshima.
Utulivu, unyenyekevu na ustahimilivu ni mambo muhimu yanayohitajika katika kipindi chote cha kumuaga mpendwa wetu Kanumba.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Sisi wote tulimpenda kwa dhati na tulitamani aendelee kuwa nasi siku zote ila Mungu aliyemleta kwa mapenzi yake ameamua kumchukua. Jina lake lihimidiwe.

                                            K.N.Y GABRIEL MTITU
                                   MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Mlioko Dar tunaomba mtuwakilishe kwa kumsindikiza ndugu yetu Steven Kanumba, lala kwa amani kaka yangu. Mungu kakupenda zaidi Kanumba hatuna cha kufanya zaidi ya kushukuru na kulitukuza jina lake.

    ReplyDelete
  2. ishallah Mola awaongoze katika hilo

    ReplyDelete
  3. Hili ni somo tosha kwa wasanii wote katika tasnia ya filamu wafahamu uzito na unyeti wa kazi yao ya uigizaji filamu katika jamii.Iwe chachu kwa wote waongeze bidii na ubunifu zaidi katika kazi yao bila ya kusubiri kusaidiwa bali jitihada binafsi,maarifa,kipaji na kujituma ndiko kulikomfikisha Kanumba hapo alipofikia.Basi waige mazuri yote aliyofanya Kanumba,ya kujitoa,kuwa mnyenyekevu kwa wote,kucheka na wote,kuheshimu kazi hata iwe duni kiasi gani,kulinda heshima na nidhamu ya taaluma,nk nk.,na zaidi kujitahadhari ya maisha yaliyozidi mipaka,"overindulgence in non-essentials of basic life",Kanumba alikuwa mfano na nyota iliyozimika ghafla,lakini,kaacha kumbukumbuku nzito itakayo dumu milele mioyoni mwa wapenda filamu nchini,bara la afrika na duniani kote.Muendelezo huo na taasisi nyingine duniani katika fani ya uigizaji filamu uendelezwe daima. Sote tusameheane kwa yote yaliyopita,tuwe na subira na uvumilivu mkubwa kwa mapungufu ya wenzetu,tumshukuru Mungu kwa ukarimu na upendo wake,na katika kifo cha Kanumba,lipo jambo Mungu alilotaka kutukumbusha na kutufundisha,lazima tutafakari,tusikimbilie kuhukumu,tuombe kwa utukufu wake Mungu, yote yaende salama,amina!

    ReplyDelete
  4. Upi ni uandishi sahihi kati ya hizi mbili:

    K.N.Y GABRIEL MTITU
    MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI

    AU

    GABRIEL MTITU
    K.N.Y MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI

    ReplyDelete
  5. Hapa duniani sote ndiko tunakoelekea,tangulia kaka yetu mpendwa kipenzi cha watanzania na watu wote duniani lakini ni pengo kubwa sana umetuachia na hakuna wa kuliziba ila tutafanyaje mungu amekupenda zaidi yetu.Umefanya mengi mazuri mungu atakulipa poleni sana watanzania wenzangu tumwombe mungu katika kipindi hiki kigumu.SOTE TUTAREJEA KWAKE(MUNGU) ILA NDUGU YETU AMETANGULIA TU.INNAL-LILLAH WA-INNAL LILLAH WAJIGHUN.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...