Ndugu wanahabari na wananchi kwa ujumla,

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tumefuatilia kwa makini sana mchakato wa Katiba mpya kuanzia ulipoanza mpaka hapa ulipofikia.

Sote tunafahamu kwamba hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kuteuliwa na kuapishwa kwa wajumbe wa tume ya kukusanya maoni juu ya mchakato mzima wa Katiba mpya na namna ambavyo wananchi wangependa iwe.

Tunapenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Serikali kupitia wizara ya Katiba na Sheria kwa hatua iliyofikiwa mpaka sasa kwenye mchakato mzima. 

Tunatoa pongezi kwa uteuzi wa wajumbe wengi waliobobea katika fani mbalimbali za Sheria, Siasa na Masuala ya kijamii. Tumefurahi kuona kuwa Mheshimiwa Rais amemteua kuwa mwenyekiti wa Tume Jaji Joseph Sinde Warioba ambae tulishaona kazi yake nzuri hususan pale alipoongoza vizuri tume ya Rais iliyohusu masuala ya Rushwa. Tuna imani kuwa ataongoza tume hii kufanya kazi nzuri.

Wajumbe wa Tume hii ni 32 (akiwemo mwenyekiti na makamu) waliapishwa tarehe 13/04/2012.

Wajumbe hao ni kama ifuatavyo; 

Mwenyekiti wa Tume ambaye ni Jaji Sinde Warioba na Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu Agustino Ramadhani.Wajumbe wa tume toka Tanzania Bara ni Prof. Mwesiga L. Baregu, Nd. Riziki Shahari Mngwali, Dr. Edmund Adrian Sengodo Mvungi, Nd. Richard Shadrack Lyimo, Nd. John J. Nkolo, Alhaj Said El- Maamry,Nd. Jesca Sydney Mkuchu, Prof. Palamagamba J. Kabudi, Nd. Humphrey Polepole,Nd. Yahya Msulwa, Nd. Esther P. Mkwizu, Nd. Maria Malingumu Kashonda, Mhe. Al-Shaymaa J. Kwegyir (Mb), Nd. Mwantumu Jasmine Malale Na Nd. Joseph Butiku.

Wajumbe wengine 15 ni kutoka Tanzania Zanzibar. Wajumbe hao ni Dkt. Salim Ahmed Salim, Nd. Fatma Said Ali, Nd. Omar Sheha Mussa, Mhe. Raya Suleiman Hamad, Nd. Awadh Ali Said, Nd. Ussi Khamis Haji, Nd. Salma Maoulidi, Nd. Nassor Khamis Mohammed, Nd. Simai Mohamed Said, Nd. Muhammed Yussuf Mshamba,Nd. Kibibi Mwinyi Hassan, Nd. Suleiman Omar Ali, Nd. Salama Kombo Ahmed, Nd.Abubakar Mohammed Ali na Nd. Ally Abdullah Ally Saleh.

Mapungufu tunayoyaona;
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunaona mapungufu makubwa mawili kwa tume hii

i) Kuwemo kwa mbunge na mjumbe wa baraza la wawakilishi
ii) Uwakilishi finyu wa kijinsia na makundi mengine mfano vijana

Wawakilishi kuwa wajumbe Kituo hakikubaliani kabisa na uteuzi wa wakilishi wa wananchi (Mbunge na Mjumbe wa Baraza la wawakilishi). Wajumbe hawa ni Mhe. Al-Shaymaa J. Kwegyir (Mb) Tanzania Bara na Raya Suleiman Hamada mwakilishi Baraza la Wawakilishi Zanzibar. 

Sababu kubwa za kutokukubaliana na uteuzi wa wajumbe hawa ni kuwa kwanza,hawa watashiriki kama wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (constituent assembly) kwa hiyo kuna ‘mgongano ulio dhahiri wa kimaslahi’. (kwa mujibu wa vifungu cha 6 na 22 (1) (a) na (b) vya sheria Namba 8 ya Mabadiliko ya Katiba,(2011) Pili wananchi wanaowawakilisha watanyimwa haki yao ya kuwakilishwa kwa kipindi chote cha miezi 18 mpaka ishirini ambacho tume itafanya kazi kwa mujibu wa sheria.

Tatu, kuna majina mengi ambayo mheshimiwa Rais alipelekewa yenye sifa za kutosha angeweza kuwateua. Kulimbikiza kazi nyingi kwa watu wale wale si afya kwa demokrasia.

Uwakilishi finyu wa kijinsia na makundi mengine Katika tume hii tumeona kuna uwakilishi finyu sana wa makundi kwa mfano wanawake wako 10 kati ya 32, yaani sawa na asilimia 27% tu! Tungetegemea  asilimia 50% kwa 50% kwani Tanzania imesaini na kuridhia mkataba wa nyongeza wa maendeleo ya kijinsia kusini mwa Afrika yaani SADC Gender Protocol. Pia 3 Tanzania ina asilimia ya 51 ya idadi ya wanawake ambao miongoni mwao wengi wana utaalamu na sifa za kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume.

WITO
I) Tunapenda kutoa wito kwa serikali kuwa mchakato wa Katiba ni wa muhimu sana hautakiwi kuchukuliwa kwa wepesi. Mchakato huu unajenga mustakabali wa Taifa letu kwa miaka mingi ijayo. Hivyo katika maamuzi yote yanayochukuliwa, kuwe na jicho la HAKI ZA BINADAMU na utawala wa sheria.

II) Pia tunapenda kutoa wito kwa WANANCHI wote wa Tanzania, mijini na vijijini, wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara, TUSHIRIKI kwenye mchakato huu. Tunawasihi kuwa Tume ya Katiba itakapokuja kwenye maeneo yetu tuhudhurie mikutano yote na kutoa maoni yetu juu ya Katiba Mpya. 

Wananchi katika makundi au mtu mmojamoja anaweza kupeleka maoni ya maandishi kwenye tume mara anuani itakapojulishwa kwa wananchi.

III) Mwisho tunatoa wito kwa tume kuhakikisha watu wote wanatoa maoni yao bila ubaguzi. Makundi yote ya jamii yafikiwe (Wanawake, wanaume,watu wenye ulemavu na watoto wenye umri wa kutoa maoni).

Asanteni kwa kunisikiliza,
Dr. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi mtendaji- LHRC

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 15 mpaka sasa

  1. Nasilitika sana kwa kuwa na mawazo finyu uwiano wa uwakilishi sio kigezo cha ubora wa ukusanyaji wa maoni. strategy gani zinatumika kufikia kila kundi na analysis for building concepts hivi ndio vitu muhimu kwa ajili ya mchakato mzima wa katiba. TAFADHALI TAFAKARI LENGO KABLA YA KUEXPRESS FEELING YAKO

    ReplyDelete
  2. Ndugu Michuzi, naomba nitoe maoni yangu kuhusu tamko lililotolewa na kituo cha sheria na haki za binadamu.
    Mimi kwa mtazamo wangu hiki kituo kumepoteza mamlaka ya kuwa kituo cha sheria na haki za binadamu kwa sababu nitakazao zieleza ifuatavyo:

    Kuna mambo mengi yanatokea hapa nchi yanayogusa haki za binadamu moja kwa moja hatuwasikia hawa kutoa matamko wala kukemea, nitaanza na matukio ya hivi karibuni:

    Muigizaji Elizabeth ajulikanae kama Lulu ambaye ni mtoto, amekuwa akishutumia na magazeti na vyombo mbali mbali vya habari kabla hajafikishwa mahakamani wala kuhukumiwa na mahakama, wamekakimya wakati jamii inamuhukumu kupitia vyombo vya habari, wao wako wapi?

    Kuna mtoto kapewa ujauzito na dereva wa lori na si mtoto mmoja, vyombo karibu vyote na mablog yamaendika wao kimya.

    Kuna mama alidhalilishwa, kafanyiwa fujo, kavuliwa nguo hadharani na kuburutwa kama mzoga, hatukuwa sikia.

    Wagonjwa wamekufa, wamedhalilishwa, wameteseka kwa mgomo wa madaktari kinyume na kiapo chao na maadili ya ajira yao……….walikuwa upande wa pili kutetea, mradi ni serikali ndio iliokuwa ikigomewa.

    Sasa haki hii wanaoipigania ni ipi na sheria wanazotumia ni zipi? Mimi ninawasikia tu pale serikali inapofanya maamuzi ya kitaifa ndipo watakapo tafuta kipengele kimoja au kingine mradi watie dosari serikali na haswa sauti ya rais.

    Hiyo hoja ya mbunge na muwakilishi kuwa na mgongano wa kimaslahi hii si kweli na hoja ya kuwakilisha wananchi, kwani watakapo kuwa wanachukuwa maoni ya wananchi hii haitakuwa kuwatumikia wananchi, isitoshe hii itawapa upeo mkubwa watakapo kuwa kwenye bunge maalum la katiba (constituent assembly) itawapa uwanja mkubwa wa kupambanua hoja, hili si swala binafsi kwa hiyo mgongano wa kimaslahi hautokuwepo.

    Kisha hii SADC gender protocol ilikuwa inagusia maeneo ya serikali tu au na maeneo mengine, kama ndio hivyo atuambie yeye kwake anawanawake wangapi na wanaume wangapi, je amefanya uwiano wakutosha kwa kuzingatia makundi mbali mbali ya jamii?

    Kwa hakika vituo hivi vinatufanya tufikirie na kudadisi madhumuni yao, kwa muelekeo huu hatuna budi baadhi yetu kuona kuwa ziko ajenda za siri zinazoendelea nyuma ya mapazia.

    Asante Ankal.

    ReplyDelete
  3. yussufu laizaApril 20, 2012

    Dr.hellen wacha hizo.
    Wale wamewakilisha jamii ya watu wenye ulemavu. Kuwa kwao wabunge au wawakilishi hakuwavui haki ya kuwa wajumbe wa kamati ya katiba. Na itakapofika wakati wa bunge maalum la katiba basi kura zao hazitahesabiwa, nazo ni mbili tu hazina madhara. Msianzishe ligi tena subirini kwani ninyi ndio mliokuwa mkitaka katiba mpya

    ReplyDelete
  4. Uteuzi umekamilika hakuna Dosari kwa ''Kundi la Walemavu kuwakilishwa mara mbili''

    HONGERA NA AHSANTE SANA MHE. RAISI J.K KWA KAZI NZURI !

    ReplyDelete
  5. MAMA BISIMBA ACHA KUTAFUTA UMAARUFU KWA NGUVU MAMA WEEE... KUMBUKA USEMI WA KUCHAMBA KWINGI MWISHOOOOO......... SASA HIVI HATA HATUKUELEWI UPO UPANDE GANI, MWANAHARAKATIII??? AU MWANASIASA SHAURIANA KWANZA NA VIJANA WAKO MBONA UNA VIJANA WENYE AKILI SANA TU HAPO KWA OFC YAKO? NI LINI KITUO CHAKO KITAPONGEZA SERIKALI IKIFANYA VIZURI AU RAISI WETU INA MAANA WAO WANAKOSEA TU???JITATHMINI USIJE UKAUA LHRC BURE

    ReplyDelete
  6. Namba mbili umeandika vizuri sana,asante sana mkuu.Kwa sisi ambao hii si fani yetu tumepata 'nondo' za kutosha.

    David V

    ReplyDelete
  7. Bora wamepinga kila kitu hata kama hoja hakuna. VERY FLIMSY ARGUMENTS!! Tuacheni tujenge taifa!!

    ReplyDelete
  8. huyu mama ananichefua kweli kweli, kila jambo linalofanywa na serikali yeye lazima akosoe, hakika kuna yaliyojificha nyuma ya pazia niungane na mdau juu

    ReplyDelete
  9. Haya hayaaaa, kituo cha sheria na haki za binadamu.....??? haki za binadamu gani mnazitetea nyinyi?? tukiamua kuwalipua nyie mmoja mmoja mtalipuka mtabaki majivuuuu....

    ReplyDelete
  10. Acheni hizo nyie wengi hampingi hoja mnamsema mtu. Jibuni hoja kwa hoja, anachosema mama ni kwamba sheria namba 8 ya 2011 mabadiliko ya katiba vifungu vya 6 na 22(1) aa na bee. Iweje sheria brand new ivunjwe tena? Hapo ndo ameegemea. Pili kagusia ugeugeu wa serikali kwenye ishu ya gender balance. Serkali ilikua na nafasi kuonyesha kweli iko committed kwenye usawa wa kijinsia kwa kuchagua wajumbe 50% wanawake, na ametoa mfano wa SADC Gender protocol ambayo TZ ni mwanachama. Sasa kuna ubaya gani hapo? Mbona serikali imetumia kigezo cha kuteua 50% wa bara na 50% wa Zenji, imeandikwa wapi 4% ya population ya waTZ wawakilishwe sawa na the other 96%? Bado hamoni kuna kasoro hapa. Wazanzibari na wabara wote ni sawa. Tuna passport yetu ya green, ya ukweli. Binafsi nadhani vigezo kama ivi vikiendelea kutumika muungano utapotea maana ndo njia rahisi ya kutugawa! Ila kigezo cha 50% wake na 50% waume kimekaa pouwa, maana haiwezekani Tanzania kua ya wanawake pekee. Jibuni hoja sio kumchafua mtu!

    ReplyDelete
  11. AMEN wadau kwa kuliona hili...yani siku hizi kila kitu kupinga. Mama hapa umejiabosha, pumzika na wajukuu...umekaa kutafuta dosari ukaiona hiyo ndio dosari aibu. Wameshaapishwa pole sana kama ulihisi na wewe utakuwa mmoja wao umeula wa chuya.

    ReplyDelete
  12. Yeye mama Hellen tunampinga kama yeye na tunapinga hoja zake, maana uzoefu wa hoja zake za mara mara za aashiria kuwa ni zake binafsi kwa maslahi yake na anaowatumikia. Huyu na mwenzie Annanilea wametuthibitishi angalau sisi wachache kuwa hawa si wanaharakati bali ni wanamikakati.
    Sasa wewe unababaika na hivyo vipengele vya sheria alivyoviandika kwa mafungu, ujue kwanza kwenye sheria kuna kitu kinaitwa tafsira, sisi tunajuaje kama hiyo siyo tafsira yake binafsi, hivi mwanasheria yeye tu peke yake, asilete hizo.
    Na hiyo SADC gender protocol ndio Tanzania ni signatory, haina maana kuwa basi maamuzi yote yazingatie uiwano wa jinsia peke yake bila ya kuangalia, ueledi, uwezo, ufanisi, uzoefu n.k pia na kuzingatia uzito wa kazi yenyewe, basi kwa vile ni jinsia basi hata akina kenge, akina ananikera, akina chausiku wawemo kwa vile wanawake. Mimi ni mwanamke na nina support uwiano wa jinsia, lakini si kiholela kujaza nafasi tu. Hizi hoja za hivyo ndio zinavuruga maadili ya nchi hii, anazungumzia vijana, wepi anaowafikiria yeye, vijana wengi wamepoteza muelekeo, wanaona fujo, matusi, kejeli, utovu wa adabu ndio nguvu ya watu, hao ndio watakaoenda vijijini na kuwalazimisha wazee wasaini maoni yao wenyewe.
    Hawa bwana hawana lolote la kijamii zaidi ya kuipinga serekali na hasa wanaomkusudia ni Rais, huu ndio ukweli waukatae tu.

    ReplyDelete
  13. JAMANI MBONA KITUO CHA HAKI ZA BINADAMU HAMJUI HESABUUUUUUUUUUUUU!
    MMESEMA WAJUMBE 10 KATI YA 32 WALIOCHAGULIWA NI WANAWAKE NA KWAMBA HIYO NI ASILIMIA 27 TU, HIVYO HAITOSHI. UKWELI NI KWAMBA NIYO IDADI NI ASILIMIA 31 NA SIO 27 KAMA MLIVYOPOTOSHA.
    (10/32)*100=31.25 WHICH IS EQUIVALENT TO 31%. KAMA HAMJUI HESABU BASI AJIRINI WATU WA MAHESABU.

    ReplyDelete
  14. Sasa ndio imeonyesha wazi mama bisimba na wenzio ni politicians, tulishuhudia Lissu alikuwa mwanaharakati wa mazingira na sasa yupo mjengoni, hatushangai tumewazoea, ila angalieni wananchi tumeanza kuwapuuza kwa hoja zenu zisizo na msingi. Hongera rais Kikwete kwa kazi nzuri(kwanza huyo mnaemlalamikia kuna double presentation walemavu na wanawake pia)

    ReplyDelete
  15. Hizi Pesa za wafadhili sasa zinawadharirisha kwani wanawake 10 hawatoshi, ina maana wakiwa nusu au sawa kwa sawa na wanaume ndo akili zinaongezeka?

    Huko hakuna kazi za kike wala kiume ni mnyumbulikano wa uzoefu ndo unaotakiwa sio idadi sawa, naona uroho wa kuteuliwa umewazidi. Kama mnataka uwakilishi sawa mbon nyie miradi yenu mingi inasimamiwa na wanawake wengi kuliko wanaume? anzeni kwenu kwanza.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...