Na Nafisa Madai Maelezo Zanzibar

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ipo mbioni katika kuhakikisha inajenga Bandari mpya katika eneo la Mpiga Duri kutokana na uhaba uliopo kwenye bandari inayotumika hivi ya Mlaindi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Issa Haji Ussi mara baada ya kumaliza kwa ziara yake katika maeneo ya kuwekea makontena bandarini na Bwawani.

Amesema kuwa katika ziara yake hiyo ameona kuwa Shirika la Bandari Zanzibar linakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa eneo la kuwekea makontena pamoja na gati ya kufungia meli kubwa za mizigo.

Alisema kuwa hii inatokana na eneo hilo kuwa dogo la kuwekea makontena hayo na biashara mbali mbali ambazo zinatoka nje ya Zanzibar zinapitishwa hapo kwa ajili ya kuwafikia wananchi.

“Bandari ya Zanzibar inakabiliwa na changamoto kubwa sana ya uhaba wa eneo la kuwekea makontena pamoja na gati ya kuegeshea meli kubwa zinazobeba mizigo,”alisema.

Naibu Waziri huyo alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar mwaka huu imeshuhudia ongezeko kubwa la makontena katika bandari ya Zanzibar ukilinganisha na miaka iliyopita.

Alisema kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu jumla ya makontena 11,430 yaliingia katika bandari ya Zanzibar,ambapo pia alisema kuwa meli za makontena hivi sasa zinabeba kati ya makontena 400 hadi 800 kwa ajili ya Bandari ya Zanzibar ikilinganishwa na Makontena 100 hado 500 miaka ya nyuma.

Aidha Gavu alitoa mfano wa meli ya MV Lara Rickmers ambayo iliwasili visiwani humu Mei 19 mwaka huu ikiwa na makontena 668 ya kuteremesha,ililazimika kufunga gati Mei 20 baada ya Shirika kuandaa nafasi kwa kuyahamisha makontena 334 yaliokuwa matupu.

Alieleza kuwa meli hiyo ilianza kazi ya kushusha makontena hayo siku ya pili na mpaka jana tayari ilikuwa imweshashusha makontena 284 na inatarajiwa kumaliza kazi ya ushushaji Jumatano jioni ikiwa ni pamoja na kupakia makontena 500 matupu ya kampuni hiyo yaliokuwepo katika bandari ya Zanzibar.

“Hii inaonesha wazi kuwa wafanyakazi wa Shirika la Bandari wanafanya kazi kwa ufanishi wa hali ya juu na wanafanya ipasavyo isipokuwa nafasi ya kuwekea makontena na gati ndio tatizo kubwa,”alieleza.

Aidha Gavu alifahamisha kuwa kutokana na uhaba wa gati ya kufungia meli,iwapo meli mbili au tatu za makontena zitawasili siku moja au kukaribiana sana,ni lazima meli nyengine zibakie zimetia nanga zikisubiri nafasi.

Alieleza kuwa jumla ya meli tisa za mizigo kutoka nchi mbali mbali zinashusha mzigo katika bandari ya Zanzibar kila mwezi,ambapo alisema kuwa inasaidia kuingiza fedha nyingi ambazo hutumika katika kuleta maendeleo mbali mbali katika nchi.


Hata hivyo Naibu Waziri huyo alifahamisha kuwa bandari mpya ambayo inatarajiwa kujengwa katika maeneo ya Mpiga Duri itakuwa na ukubwa wa kilo mita tano ambayo itaweza kufunga gati kwa meli nne za mizigo tofauti na sasa ambapo meli moja tu ya mizigo ndio inayofunga gati.

Kuhusu bandari ya Pemba,Naibu Waziri huyo alisema kuwa bandari ya hiyo mpaka hivi sasa haina matatizo ambayo yaweza kuathiri utendaji wa kazi za Shirika hilo.

Alifahamisha kuwa matatizo yaliyopo kwenye bandari ya Mkoani na Wete kisiwani humo ni madogo sana, hivyo alifahamisha kuwa mara baada ya kumalizika kwa ujenzi wa bandari ya Zanzibar,fedha zitakazopatikana ndizo zitakazofanyia matengenezo bandari ya Pemba.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 21, 2012

    Mhe. Naibu Waziri tafadhali sahihisha kauli yako.Hebu kuwa mkweli.Si sahihi kawamba bandari ya Mkoani haina matatizo. Toa taarifa sahihi kwa umma.Bandari ya mkoani haina sifa ya kuitwa bandari bali ni tuta. Mhe.Shein tafadhali chagua Mawaziri wenye dira. Leo bandari ya Mkoani ina mapungufu makubwa mabayo ile sifa ya kuitwa Gati haipo. Inabidi wataalam wakae chni waifanyie mabadiliko yakiwemo ya kupakia abiria na kupakua mizigo na sio hali kama ilivyo sasa. Pili bandari aya Wete.Lazima ukweli usemwe kwamba bandari hii ndio ilikuwa bandari kuu tangu baada ya Mapinduzi matukufu.Leo imebakiwa na baraza licha ya kuwa na uwezo kukuza biashara na Tanzania Bara(Tanga) na jirani zetu Mombasa(Kenya). Serikali lazima iwe na mkakati wa kuangalia upande wa pili.Unakusudia kujenga bandari yenye maili tano urefu wake kisha unaacha kisiwa cha Pemba kikiwa hakina huduma hata ya kawaida tu si sahihi. Serikali ya umoja wa kitaifa ionyeshe kwa udhati Umoja wa Kitaifa.Na hilo tunamuachia Mhe.Shein alirekebishe.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...