Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dkt. Asha-Rose Migiro akizungumza wakati wa uwasilishaji wa Ripoti ya mwaka 2012 ya Maendeleo ya Binadamu Afrika, lipoti hiyo ambayo imeandaliwa na UNDP kanda ya Afrika ni mahususi kwa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Ripoti hiyo inaeleza pamoja na mambo mengine kwamba ingawa uchumi wa Bara la Afrika umeendelea kukua vizuri ikilinganishwa na mabara mengine, lakini ukuaji wa uchumi huo haujaweza kuikabili au kumaliza baa la njaa na shida kubwa ya usalama wa Chakula Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara.
Sehemu ya Mabalozi kutoka nchi za Afrika hapa Umoja wa Mataifa, wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Rose Migiro wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya mwaka 2012 ya Maendeleo ya Binadamu Afrika, hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi za Umoja wa Afrika zilizopo jirani na Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York.
kutoka kushoto ni Naibu Balozi wa Ubalozi wa Zimbabwe Bibi Rofina Chikava, Sheila Mweemba Naibu Balozi Ubalozi wa Zambia UN, Naibu Katibu Mkuu Dkt. Asha-Rose Migiro na Bw. Jerobean Shaanika, Naibu Balozi wa Namibia .
Naibu Katibu Mkuu akiwa na, kutoka kushoto, Balozi wa Benin Bw. Jean- Francis Regis Zinsou ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kundi la Afrika kwa mwezi huu wa Juni, anayefuatia ni Bw Tegegnework Gettu Katibu Mkuu Msaidizi na Mkurugenzi wa UNDP kanda ya Afrika na wa kwanza kulia ni mwakilishi wa Umoja wa Afrika katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tete Antonio.

Na Mwandishi Maalum

Wakati Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiendelea kukabiliwa na baa la njaa na upungufu mkubwa wa chakula. Taarifa zinaonyesha kwamba Afrika inaweza kabisa kuondokana na hali hiyo pale tu viongozi wake watakapoonyesha utashi wa kisiasa na dhamira ya dhati ya kujinasua na baa hilo.

“ ushirikiano wa pamoja wa kitaifa na kimataifa, utashi wa kisiasa, será na mipango mizuri inayolenga kukuza kilimo na kuongeza uzalishaji wa chakula katika Afrika kusini mwa jangwa la Sahara ni jambo ambalo halina mjadala” anasema Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha_Rose Migiro.

Ameyasema hayo wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya mwaka 2012 ya maendeleo ya Binadamu Afrika, ripoti ambayo iliwasilishwa kwa Mabalozi wa Afrika wanaoziwakilisha nchi zao katika Umoja wa Mataifa.

Migiro anasisitiza kama ambavyo viongozi wa Afrika wamekuwa wakishirikiana katika kuzikabili changamoto nyingine, wanaweza pia kushirikiana katika kukuza kilimo na uzalishaji wa chakula na hatimaye kuwa na usalama wa chakula ambao ni wakudumu.

Ripoti hiyo ambayo maudhui yake ni “ kuelekea usalama wa chakula”imetayarishwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa, ( UNDP) kanda ya Afrika, na ni mahususi kwaajili ya Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara.

Ni ripoti ambayo imeelezea kwa nini Afrika imeendelea kuwa ombaomba wa chakula, ikianisha pia na kutoa mapendekezo yakiwamo kama ya uendelezaji wa miundombinu ya vijijini, uwezeshaji wa wakulima wadogo wakiwamo wanawake, uwekezaji katika kilimo na pembejezo za kilimo, uhakika wa chakula hicho kufika mezani na lishe bora.

Akizungumzia ripoti hiyo, ambayo anasema tayari imeibua mijadala katika vyombo vya habari. Migiro anasema ripoti imekuja wakati muafaka ambapo Jimbo la Sahel ya Magharibi likiwa katika shida kubwa ya chakula huku watu milioni 13 wakiwa katika hatari kubwa ikiwa ni pamoja na watoto milioni moja.

Akasema inatia moyo kwamba viongozi wa Afrika wameanza kuchukua hatua mbalimbali za kulikabili janga hilo. Lakini inatia moyo zaidi pale ambapo viongozi wa mataifa tajiri akiwamo Rais Barack Obama wanapojitokeza na kuelezea nia yao ya kusaidia ukuaji wa sekta ya kilimo katika afrika na kuwaondoa watu milioni 50 kutoka katika umaskini katika kipindi cha miaka 10 ijayo.

Akabinisha viongozi hao wa mataifa tajiri zaidi duniani (G8) wamereja tena kauli yao waliyoitoa huko L’ Aquila, ahadi ya kuongeza misaada ya kifedha inayolenga kusaidia mipango ya kitaifa.

“Tumeonyeshwa katika ripoti hii kwamba uongozi wa aina hii ni muhimu sana. Usalama wa chakula haupashwi kuchukuliwa kama ni jukumu la sekta moja au wizara fulani peke yake. Bali linatakiwa kuchukuliwa kama jambo linalopashwa kushughulikiwa na sekta nyingi kwa wakati mmoja na kupewa kipaumbele katika ajenda za maendeleo.

Aidha anasema anaimani kwamba ikiwa mpango wa mapinduzi ya kijani ambao umeandaliwa mahususi kwaajili ya Afrika, mpango ambao yeyé aliusimamia kuwa, kama ukitekelezwa vizuri utatoa mchango mkubwa kwa kuwa na usalama wa chakula.

Kwa upande wake, BW. Tegegnework Gettu ambaye ni Naibu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa UNDP kanda ya Afrika, yeyé alisema Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara haina sababu ya kuendelea kuwa na uhaba mkubwa wa chakula kutokana kwamba ina hazina kubwa ya ardhí inayofaa kwa kilimo, mito na maziwa ya kutosha na raslimali watu.

“Afrika tunakila kitu cha kutuondoa katika hali hii, hatustahili kuendelea kuwa omba omba wa misaada ya chakula wala watoto wetu kuwa na utapia mlo na kudumaa”. akasema Bw. Gettu.

Akabainisha kwamba haiingi katika fikra kwamba ni kwanini licha ya Uchumi wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kuonyesha ukuaji mzuri lakini suala la usalama wa chakula limeendelea kubaki tatizo kubwa.

Akahoji pia kwamba kama nchi za India na Amerika ya Latini ziliweza kuondokana na uhaba wa chakula kwa kutumia mapinduzi ya kijani,( Green Revolution) kwanini hali inakuwa tofauti kwa Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...