Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha-Rose Migiro akifungua mkutano wa siku moja ambapo uliwakutanisha wadau kutoka Umoja wa Mataifa, na Taasisi za Kimataifa, kwa lengo la kubadilishana mawazo ya namba bora ya kushirikiana ili kuibua vyanzo vya ajira rasmi na zisizo rasmi kwa vijana hususani wale ambao nchi zao zimetoka kwenye migogoro ya vita.

Na Mwandishi Maalum

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha-Rose Migiro amesisitia haja na umuhimu kwa wadau mbalimbali kushirikiana ili kuibua vyanzo vya ajira kwa vijana hususani wale ambao nchi zao zimetoka kwenye machafuko na vita.

Ametoa msisitizo huo mwanzoni mwa wiki wakati alipokuwa akifungua mkutano wa siku moja wa Kamisheni ya Ujenzi wa Amani ( PCB), ambapo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwamo taasisi za kimataifa walijadiliana na kubadilishana mawazo ya namna bora ya kuibua vyanzo vya ajira kwa vijana walio katika mazingira magumu.

Migiro akasema ushirikiano wa wadau mbalimbali nje ya mfumo wa Umoja wa Mataifa ni muhimu sana katika katika kuibua mbinu mpya na kujenga mifumo bora ya kuwapatia ajira rasmi na zisizo rasmi vijana.

“ Nimefurahi kualikiwa kujumuika nanyi katika mkutano huu muhimu, ni jambo lililodhahiri kwamba duniani kote vijana wanakosa elimu, uzoefu, mafunzo na ujuzi unaoweza kuwapatia ajira. Lakini changamoto kubwa zaidi ni kwa vijana walio katika nchi ambazo zimetoka katika vita na ambako hakuna taasisi madhubuti, uwekezaji na miundombinu inayoweza kuwapatia ajira vijana” akasisitiza Migiro.

Na kuongeza kwamba, mataifa yote yawe ni yale ambayo yametoka katika vita au ambayo yako katika hali ya amani na utulivu, yanahitaji kujiwekea misingi bora na sera zitakazoweza kuibua ajira kwa vijana.

“ Tunahitaji kufanya kazi kwa pamoja na kwa kushirikiana miongoni mwetu na kwa haraka zaidi katika kushughulikia tatizo la ajira kwa vijana ambao wanaendelea kukata tama ya maisha na kujingiza katika vitendo vya uvunjifu wa amani na vurugu kama ambavyo tumeshuhudia katika siku za hivi karibu” akatahadharisha Migiro.

Akaongeza kwamba ushiriki wa sekta binafsi ni muhimu sana na kwamba sera zinapaswa kuhimiza mipango ya ujasiliamali. Na halikadhalika waajiri binafsi wanaweza pia kusaidia katika kuhakikisha kuwa sera na mafunzo yanayotolewa yanakidhi mahitaji ya soko la ajira.

Akasisisita kwamba juhudi za pamoja kati ya Umoja wa Mataifa, Mashirika ya fedha ya Kimataifa, Sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali zinaweza kuwa msingi wa kuleta mabadiliko ya kweli katika kupanua na kujenga amani ya kudumu katika nchi zinazoibukia kutoka katika vita.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya Ujenzi wa Amani ( PCB) Bw. Abulkalama Abdul Momen yeye amesema kwamba, uibuaji wa vyanzo vya ajira hususani kwa vijana walio katika mazingira magumu ni jambo la muhimu sana ili kuzuia vijana kurejea katika vitendo vya uvunjifu wa amani.

Akabinisha kwamba vijana katika nchi zilizotoka katika vita wanakuwa na matumaini makubwa sana ya kuwa na maisha bora zikiwamo ajira, na kwamba ni rahisi sana kwao kutumbukia au kurejea katika machafuko kwa kukosa jambo la maana la kufanya.

Akasema kuwa ajira kwa vijana ni jambo linalopewa kipaumbele sana katika PCB. Hata hivyo akasema wanakabiliwa na changomoto kubwa sana katika utoaji wa fursa za kiuchumi na kijamii kwa vijana ambao kiwango chao cha elimu ni duni na wasiokuwa na ujuzi wowote.

Akachagiza kauli iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu Asha- Rose Migiro ya kutaka kuwapo kwa ushirikiano na juhudi za pamoja katika kukuza ajira huku akitoa wito kwa serikali, washirika wa maendeleo, sekta za umma na binafsi na taasisi za kifedha , biashara na asasi zisizo za kiserikali kushirikiana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...