LOS ANGELES na NAIROBI (Juni 14, 2012) – Buni TV (www.buni.tv) Jukwaa la Kiafrika lililozinduliwa majuzi kuhusu matumizi ya video mtandaoni na katika simu ya mkononi/rununu, linatangaza leo kuwa limechagua filamu fupi ya “Who Killed Me”, ya mtayarishaji filamu wa Tanzania, Amil Shivji ili iweze kusambazwa kwa watazamaji Waafrika kote barani.Filamu hiyo ya “Who Killed Me” (tengenezwa na York University) inaangazia maisha ya hali ya chini ya mhamiaji wa Congo mjini Toronto, kabla na baada ya kupigwa risasi na kuuawa nje ya sehemu anapofanyia kazi. Kuanzia dada yake hadi kwa mfanyakazi mwenzake ambaye pia ni mhamiaji na kwa polisi ambao wanampata, ‘Who Killed Me” inaonyesha jinsi maisha tofauti katika jiji moja yanaathiriwa na tukio moja.
Amil Shivji mwenye umri wa miaka 22, aliwahi kuwa mwanahabari na mtangazaji wa redio, amehitimu majuzi katika kozi ya utayarishaji filamu, aliyofanyia Chuo Kikuu cha York, Toronto. Anaamini kuwa utayarishaji filamu ndio njia inayofaa zaidi ya kuleta mabadiliko ya kijamii kwa kukabiliana na ukosefu wa haki za kijamii na kisiasa, hata ingawaje usambazaji wake barani ndio changamoto kuu.
“Kuna wasambazaji wachache sana katika bara lote, hii ndio sababu filamu nzuri za Waafrika zinaishia kuonyeshwa katika tamasha za filamu za Cannes ama Sundance ilhali hakuna mtu atapata kuziona Afrika,” Shivji alisema.
“Filamu za Afrika zinafaa kutazamwa na Waafrika wenyewe. Buni TV ni jukwaa linalofaa la maonyesho kwa sababu ni mtandao unaondeshwa na Waafrika na unaoweza kufikiwa na watu wote bila vikwazo.”
Buni TV ni mtandao mbunifu (www.buni.tv) na simu ya mkononi (m.buni.tv) ni jukwaa za kusambaza video za Afrika.
Kwa kuonyesha zile bora, zenye ubunifu na kunasa yanayotayarishwa sasa Afrika ama kuhusu Afrika na kusambazwa kwa watazamaji wapya barani na ng’ambo, Buni TV inanuia kuleta mageuzi katika mandhari ya vyombo vya habari Afrika.
“Tunajivunia kuweza kuonyesha filamu ya Amil katika Buni TV na kuifanya iweze kupatikana kwa watazamaji Waafrika kote barani. Amil ni mwakilishi wa wimbi jipya la watayarishaji filamu Waafrika ambalo linajitokeza sasa, na tunasubiri kwa hamu kile atakachofanya baadaye,” Mkurugenzi Mtendaji wa Buni TV, Marie Lora-Mungai, alisema.
Buni TV imeelezea kupokewa vyema na watazamaji wake tangu ilipozinduliwa Aprili mwaka huu, na watu waliotembelea jukwaa zake wakifikia 90,000 katika muda usiozidi miezi miwili. Waliotembelea jukwaa hizo walichukua saa zaidi ya 2,000 wakitazama video.
Ingawaje jukwaa nyingine za video za Afrika zinaonekana kuleta tu soko la nje, Buni TV inataka kuonyesha zake kwa watazamaji barani ambao hawajapata fursa hiyo. Ikiwa inatarajia video kwa simu za mkononi kushika kasi, Buni TV iliunda jukwaa linaloweza kutumika kwa urahisi hasa katika simu zenye uwezo wa kufanya shughuli nyingi na huduma hiyo inaweza kupatikana kwa m.buni.tv.
Mwanzoni video zinazoingia kwa Buni TV huwa bila malipo pamoja na matangazo. Katika siku zijazo, jukwaa hilo litaunda sehemu ya kutozwa ada ili kuweza kufikia yaliyomo muhimu.
Habari zaidi kuhusu Buni TV:
Buni TV ni huduma ya Buni Media (www.bunimedia.com), kampuni ya vyombo kadha vya habari, Kenya na Los Angeles, California. Buni Media hutayarisha kipindi cha XYZ, kipindi cha kwanza Afrika kinachoonyesha dhihaka katika siasa na hutumia watu waliovalia kama vikaragosi. Shoo ya XYZ (www.xyzshow.com) hufikia watazamaji zaidi ya milioni nane kila mwezi kupitia jukwaa tofauti.
Kwa habari zaidi, wasiliana na press@bunimedia.com.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...