Samahani Ankali, kwa kurejea jamvini,
Usiniwie mkali, na kuniweka kapuni,
Mroki si serikali, wajibu walo makini,
Takwimu za dini zetu, wapi zinapatikana?

Nilivyoona Mroki, nikadhani haropoki,
Tungo nilipo hakiki, kuzirudia sitaki,
Vina havieleweki, kajibu kiushabiki,
Takwimu za dini zetu, wapi zinapatikana?

Kama hatuna idadi, za wananchi kidini,
Taifa halina budi, kuwahoji Marekani,
Takwimu wanazonadi, aliyewapa ni nani?
Takwimu za dini zetu, wapi zinapatikana?

Wazi zina walakini, kwa kuwa hazilingani,
Mara hawa thelathini, na mara wako sitini,
Hebu cheki hapo chini, tovuti-kweli ya nani?
Takwimu za dini zetu, wapi zinapatikana?

Kuhesabu si udini, ni ukweli wa takwimu,
Kinachofichwa ni nini, nijibuni kwa nidhamu,
Serikali hesabuni, ni ya kwenu majukumu,
Takwimu za dini zetu, wapi zinapatikana?

Sikusema tuwaige, Wamarekani jamani,
Mroki macho matege, ‘data’ hizo hapo chini,
Huyu bwana kumbe bwege, hata mimi sikudhani,
Takwimu za dini zetu, wapi zinapatikana?

Vipi uwe mkimbizi, kusema wewe Pagani?
Weupe wa Msimbazi, mbona wapo kwa amani?,
Hili twaliweka wazi, hata humo takwimuni,
Takwimu za dini zetu, wapi zinapatikana?

Takwimu za kukisia, haziwi ni endelevu,
Wengine wakisikia, wasema ni uonevu,
Upi ni uhalisia, ewe ‘baba wa Kidevu?
Takwimu za dini zetu, wapi zinapatikana?
  
  1. http://www.state.gov/r/pa/ei/bgn/2843.htm
  2. https://www.cia.gov/library/publications/the-world-factbook/geos/tz.html
  3. http://www.encyclopedia.com/topic/Tanzania.aspx
 Mwamgongo, (Bw.)
Mwenyeji wa Tanga,
 19 /Juni/ 2012

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. AnonymousJune 19, 2012

    Wewe ndo mjuzi wa tungo,,Uko juu saaaana kama mawingu
    Ahlam

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 20, 2012

    Ahsante Bw.Mwamgongo kwa kuendelea kutuelimisha kwa kutupa dalili/uhalisia wa mambo.Nafikiri sasa suala la sensa kuwa na kipengele hakina mjadala, ni vyema kiwepo.Taasisi nyingi za serikali ya Tanzania na za binafsi zilizopo tanzania na taasisi za nje ya nchi wanatumia takwimu ambazo si rasmi. Kila taasisi ina lengo lake la kutoa takwimu hizo hata kama hazijatoka serikalini.Sasa kama hali ndiyo hiyo, kwa nini kunakuwa na ubishi wa kuweka hicho kipengele kwenye sensa? Wanaotetea kutowepo kipengele cha dini kwenye sensa hawana mashiko ya kisayansi, mengi yapo kwa kudhania.Hatuwezi kufika tukiendelea kuwa na tabia ya kudhania dhania.Tufuate uhalisia wa jambo.Nitaje kwa haraka haraka taasisi ambazo zimetoa takwimu za watu kulingana na dini zao: TBC1, Uhamiaji, Kanisa Katoliki Tanzania, CIA (Shirika la Ujasusi la Marekani), U.S Department of State Diplomacy in Action (hili ni la Marekani), n.k. Sasa kama hali iko hivyo kwa nini siye Watanzania tusiwe na data zilizo za kweli kutokana na kazi yetu? Hatuwezi kuendelea kama hatuna "DETERMINATION", tusahau. Ndiyo dhana hii hii ya woga watoto wabunifu wanakamatwa na polisi eti wanasema wanataka kuhatarisha maisha yao,badala ya kuwachukua na kuwauliza mumefanyaje?

    Nawakilisha...

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...