Ewe bwana Mwamgongo, wa kule pwani ya Tanga
Asante kwavyo vigongo, vinavyocheza pachanga
Kana kwamba ni  bolingo, waipendayo waTanga
Zangu mie shukurani, kunogesha  libeneke

      Na weye bwana Mroki, Hakika sijamaizi
Kwamba nawe wajikoki, kunogesha simulizi
Nilidhani husomeki, kwenye zetu anga hizi
Zangu mie shukurani, kunogesha  libeneke

      Zangu mie shukurani, kunogesha  libeneke
Enyi marenga wa Pwani, mwanikosha kwa makeke
Yalosheheni  utani, wa kunifanya nicheke
Zangu mie shukurani, kunogesha  libeneke

    Sina nia na upande, wa kushabikia hapa
Tungo zenu kama kande, zenye mchuzi wa papa
Wa kupenda na apende,  la na aondoke hapa
Zangu Mie shukurani, kwa kunogesha  libeneke

  Katika zama za sasa, kweli adimu kuona
Wadau  wenye hamasa, kwazo hoja zenye vina
Nyie kweli ni vitasa, na mfanowe hamna
Zangu mie shukurani, kunogesha libeneke

      Hoja yangu mie hapa,  kuhamasisha wadau
Muendelee kutupa, tuliyokwisha sahau
    Mashairi ninaapa, wengi tumeyadharau
Zangu mie shukurani, kwa kunogesha libeneke

      Naomba muendelee, kuleta vina na ngeli
Wadau wachekelee, umahiri wa kweli
Ya gubu tuyakemee, kwa hasira na ukali
Zangu mie shukurani, kwa kunogesha libeneke

     Mshindi hapa hakuna, wala mshindwa wa hoja
Twendelee kubishana, bila ugomvi wa haja
Mashairi yatafana, kwa juhudi za pamoja
Zangu mie shukurani, kwa kunogesha libeneke

   Beti hizi zinatosha, Mwamgongo na Mroki
Tuendelee kupasha, bila chuki na hamaki
Kwa we kinachokuwasha, lia chozi la samaki
Zangu mie Shukurani, kwa kunogesha libeneke

Na Ankal













Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Libeneke litanoga, cheka mbavu ziraruke,
    Wengine litawatoga, pepesuka waanguke,
    Mwenye lake siwe mwoga, hapa sasa ndio pake,
    Vina mizani vimwaga, ujumbe pake ufike!

    Mwaweza fahamishana, lolote siharibike,
    Mengi haelimishana, bakora zitumike,
    Mabaya hakosowana, mtu asikasirike,
    Vina mizani vimwaga, ujumbe pake ufike!

    ReplyDelete
  2. AnonymousJune 20, 2012

    Enheee

    Mjomba una fiti kotekote!

    Kumbe Ankal na wewe ni bonge la Malenga wa Mashairi ehhh?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...