Usiku wa tarehe 13 (kuamkia tarehe 14) Agosti 2012 mtu mmoja jangili ambaye jina halijapatikana aliuwawa katika Pori la Akiba la Burigi Mkoani Kagera baada ya mapambano kati ya genge la majangili na askari wa Wanyamapori waliokuwa wakifanya doria ndani ya pori hilo.
Siku hiyo mnamo saa 7 usiku askari wanyamapori walisikia milio ya risasi katika eneo la Nyungwe Kilomita 5 ndani ya Pori la Burigi. Askari walifika katika eneo la tukio maana walikuwa wakifanya doria karibu na eneo hilo na kukuta majangili ambao walikuwa wamemulika tochi zenye mwanga mkali.
Majangili walianza kurusha risasi walipobaini kuwa askari wamewakaribia. Askari Wanyamapori walijibu mapigo na mapigano hayo yaliendelea kwa muda wa takriban saa moja kabla ya majangili kukimbia.
Ilipofika saa moja asubuhi, wakati walipokuwa wanakagua eneo la tukio, askari wa Wanyamapori waligundua kuwepo kwa maiti akiwa na bunduki aina ya gobore na baruti. Askari Wanyamapori walitoa taarifa katika kituo cha Polisi Biharamulo ambapo Polisi waliuchukua mwili wa Marehemu na kuupeleka katika hospitali ya Biharamulo ambako mwili umehifadhiwa hadi sasa.
Hadi leo hakuna mtu aliyejitokeza kudai kupotelewa na ndugu. Hata hivyo uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20 hadi 28 anaweza akawa ni raia wa nchi jirani.
Uchunguzi unaendelea.
[MWISHO]
George Matiko
MSEMAJI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
16th Agosti 2012
Simu: +255 784 468047
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...