Jumapili iliyopita niliongelea kero anazopata mpiga picha wa kulipwa kwenye harusi, hasa zile za kupigana vipepsi na wadau wanaofika harusini na kamera zao za mfukoni, kamera za simu ama iPad na Samsung Galaxy tablets, na kushauri kila upande uangalie jinsi ambavyo maharusi watakavyoweza kupata picha nzuri za tukio hilo kubwa maishani mwao.
Leo naomba mniruhusu nigusie mada ya maandalizi ya harusi na wapiga picha, tukianzia kwenye mikutano ya kamati za maandalizi ambazo pamoja na kupanga bajeti, huamua nani watakaohudumu katika harusi hiyo. Aghalabu wahudumu hao kama vile watu wa chakula, wapambaji na hata wapiga picha huitwa kujieleza na kutetea nafasi zao kabla ya kupewa tenda.
Kwa uzoefu wangu wa miongo takriban mitatu ya upigaji picha za harusi na matukio mengine, mara nyingi nimeshuhudia kamati ya maandalizi kuweka kipengele cha picha mwishoni kabisa mwa ajenda za kikao, na kama mpiga picha umeitwa kuhudhuria unajikuta unakaa masaa kibao na kusikia hata yale yasiyokuhusu.
Na hata kama ajenda ya picha itakuja juu, lakini mara kwa mara bajeti huwa inakuwa ishu, ikizingatiwa kwamba wanakamati wengi hutoa  kipaumbele kwa vitu kama keki, mapambo na mengineyo, kiasi kwamba utakuta bajeti yote imeishia hapo, na ya  picha hubaki kuwa finyu hata wakati mwingine maharusi hulazimika kupiga mbizi mifukoni mwao na kusawazisha mambo.
Ikumbukwe kwamba hii ni siku muhimu katika maisha ya maharusi, na kumbukumbu ya picha ina umuhimu mkubwa sana, hivyo kuweka bajeti kiduchu kwa ajili ya picha, na bajeti kubwa kwa ajili ya mapambo na keki pekee sio vyema sana – japo vyote vina umuhimu wake.
Nahisi kuna wataodhani najifagilia ili niweze kula tenda nono. La, hasha. Huo ndio ukweli wenyewe. Wakati ni kweli kabisa kwamba “Cheap is expensive”, pia si uwongo kwamba kama utabeza umuhimu wa picha nzuri, subiri harusi ikiisha kisha anza kuweka kumbukumbu ya mapambo na keki kwenye albamu kama zilivyo, ndipo utaelewa namaanisha nini.
Kwa kawaida ya mpiga picha za kulipwa anayeifahamu vyema kazi yake, wa kukutana naye si kamati nzima, bali maharusi wenyewe na kupanga nao aina gani ya picha wanazohitaji na mahali pa kupigia, ukiondoa sehemu inapofungiwa ndoa na ukumbini. Hapo mpiga picha, kwa uzoefu wake, hupata ama hupewa fursa kutoa maoni yake, na maharusi wenye hekima huzingatia maoni hayo.
Picha za mahali panapofungiwa ndoa na ukumbini aghalabu huwa zinafanana karibu katika kila harusi, ukiondoa ratiba ya sherehe, ila zile za nje ya sehemu hizo hutofautiana. Kuna maharusi wanaopenda kwenda studio kupata picha za portrait na za makundi, wengine hupendelea sehemu za nje zenye mvuto kama vile bustanini ama ufukweni mwa ziwa ama bahari.
Kwa maharusi wanaochagua kwenda studio sina maneno nao, maana huko hukuta kila kitu kipo tayari, ikiwa ni pamoja na mataa, background, viti na kadhalika. Kwa wanaokwenda kupiga picha zao nje, hapo nina ushauri wa kuzingatia muda. Kama ndoa imefungwa mapema, muda huwa sio tatizo. Ila wanaochelewa kutoka hadi zaidi ya saa 12 unusu za jioni, hapo pana tatizo, maana mandhari wanayoitegemea huwa giza tupu na hata maana ya mwenda ufukweni wakati jua limeshazama inakuwa kazi bure. Ni vyema mpiga picha akakubaliwa ushauri wake kwamba hizo zikapigwe ukumbini.
Kubwa cha kukumbuka katika picha zote hizo za baada ya ndoa ni taswira za maharusi na wala sio mahali penyewe (background) ambapo japo kuna umuhimu wake katika kunohesha muonekano, lakini kuonesha bustani ama bahari zaidi ya maharusi hakuleti tija sana.
Mwisho kuna hii tabia ya kumtaka mpiga picha awepo saluni anakopambiwa Bi harusi (hapo anakojipunia Bw. Harusi husahaulika) tokea anaingia hadi anatoka. Kwa upande wangu hii ni kazi ya ziada ambayo inastahili iwe na malipo yake tofauti. Maana kufika saluni toka saa saba na kusubiri hadi avae na kurembwa masaa manne baadaye, nayo ni ishu.
Ufumbuzi wa hili, kwa maoni yangu, iko haja ya saluni kuwa na wapiga picha maalumu kwa kazi hiyo, ili kumpa wasaa mpiga picha wa siku muda wa kutosha kujiandaa kwenda mahali inapofungiwa ndoa na hatimaye ukumbini. Na ikibidi, kwa maoni yangu, malipo ya saluni yawe ya ziada kama ilivyo kazi yenyewe.
Jumapili ijayo nitazungumzia namna nzuri ya mpiga picha anavyotakiwa kujiandaa na kufanya kazi ya kupiga picha za harusi, huku nikimalizia tena kwamba kamati za maandalizi zisiache kutoa kipaumbele kwa kipengele cha picha. Si vibaya hata bajeti yake ikafikiriwa kwa herufi kubwa ili maharusi wapate picha nzuri na za kutosha.
Naomba kuwasilisha
-Ankal


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. duh !! Michu, kumbe una mchuma wa majuuu ?? ndiyo maana VISA hazikusumbui.Zebedayo msema kweli.

    ReplyDelete
  2. Naona umefunguka mzee

    ReplyDelete
  3. Tumekusoma ANKAL, safi sana.

    ReplyDelete
  4. Michuzi,
    Nimefurahi na makala zako za wiki kuhusu upigaji picha. Makala ya wiki hii imenigusa kidogo na nimeona nichangie.

    Kama mpigaji picha za harusi huku majuu naona kama makala zako zimeegemea zaidi mila na desturi za upigaji picha za harusi wa kibongo. Nisamehe kama nitakuwa nimevamia mkenge.

    Sijui Africa lakini kwa wapigaji wengi wa picha za harusi huku majuu uchaguliwa na bwana na bibi harusi. Hii inawezekana ikawa kutokana na bei yako au kuwa umepiga picha za marafiki, ndugu za maharusi siku za nyuma.

    Unapozungumzia suala la vikao na upigaji picha saloon, naona kama unagusia zaidi mila za kibongo. Suala la harusi ni jukumu la bwana na biharusi kwa mila nyingi na Kama una bahati nzuri litajumuisha wazazi (baba na mama).

    Maharusi katika utamaduni wa huku magharibi hupambwa majumbani na jukumu zima la mpangilio/siku nzima ya uchukuaji kumbukumbu hii liko mikononi mwa mpiga picha. Hivyo basi ni busara uwe na mkataba ambao ni uwazi na kuwasliana na kuweka bayana kwa mteja katika mzungumzo ya awali. Kama hutaweza kupiga picha saloon/nyumbani basi uweke wazi kwenye mkataba na pia ni njia ya kujiongezea kipato kwa kushawishi mpiga picha msaidizi kuweza kupiga picha hizi.

    Muhimu zaidi ni kuwa na upendo wa kazi hii. Upigaji picha za harusi ni usanii na mteja mara nyingi anakuchagua kutokana na ubunifu na utundu wa kazi zako. Kazi nyingi nilizoshuhudia nifinyo mno katika kuleta mvutio wa taswira. Hili linatokana na wapiga picha kutumia vifaa(kamera,lensi) ambavyo ni vya hali ya chini.

    -Mdau

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...