Ankal akiwa na Ndesanji Macha kwenye
ukurasa wa kwanza wa Globu ya Jamii
kuuona BOFYA HAPA

Mnamo Septemba 8, 2005 katika ukumbi wa mikutano wa Finlandia Hall , hususan katika chumba maalumu cha habari ambapo wanahabari  walitengewa kukitumia kwa ajili ya kuripoti mkutano wa Helsinki Process, mimi nilikuwa bize katika kompyuta yangu nikiandaa picha na habari za siku hiyo tayari kutuma nyumbani.

Mara akaingia kijana mmoja mtanashati, maji ya kunde, mfupi kiasi na mwenye sharafu na rasta. Nilistuka aliponisalimia kwa Kiswahili fasaha, na alinishangaza zaidi aliposema yeye ni Mtanzania, kwani pamoja na mavazi yake suti simpo ya kitenge rangi ya hudhurungi, nilidhania ni Mjamaica ama Mmarekani mweusi.

“Najua wewe unafahamiana zaidi na kaka yangu Freddy Macha na mimi hunifahamu kwani hatyujabahatika kuonana. Naitwa Ndesanjo Macha”, aliniambia kwa sauti yake yenye upole lakini yenye uthabiti wa mtu anayejiamini na aliyezoea kuongea na watu wa aina mbalimbali.
Ndesanjo akanikataza nisijitambulishe kwani ananifahamu siku nyingi kutokana na kazi zangu katika gazeti la Daily News, na kwamba kutoonana kwetu ni kwa sababu yeye anaishi na kufanya shughuli zake Marekani. “Nimefurahi sana kukuona….” Aliongezea kwa tabasamu kubwa.

Baada ya maongezi haya nay ale, na kwa kuwa yeye tayari alikuwa anafahamu mimi nafanyia chombo gani cha habari, ikaja zamu yangu kumhoji yeye anafayia chombo gani.  Hapo akanipiga butwa la tatu kwa kusema yeye hafanyii chombo chochote ila ni bloga wa libebeneke la www.jikombe.blogspot.com na pia ni mwandishi na mhariri wa libeneke la kimataifa la mijadala mtandaoni la globalvoicesonline.org.

Ni kweli kwamba toka wakati huo nilikuwa najua blogu ni nini, ila si uwongo kwamba sikuwahi kumaizi kwamba mtu anaweza akajiajiri mwenyewe na kuweza hata kupata mialiko ya kuhudhuria mikutano na shughuli za kimataifa bila kuwa mwakilishi wa chombo rasmi cha habari kama vile TV, redio na magazeti.

Wakati nikiendelea kutafakuri hayo, Ndesanjo akanihoji endapo kama nina blogu yangu. Nilipomwambia sina akashangaa sana. Na si kushangaa pekee bali alinicharura kwa utani kwa nini wanahabari wa Tanzania hatutumii mitandao kutuma habari za nyumbani kama wanavyofanya mataifa mengine. Nikapepesa macho tu; sikuwa na jibu.

Ndipo akanifungulia blogu zake za jikomboe na globalvoices, nikabaki mdomo wazi kwani humo mlikuwa na habari kedekede ambazo alisema siku hizi tunakoelekea ni kwenye mtandano. Haraka haraka nikamuuliza kama na mimi naweza kufungua blogu ya kwangu. Akasema sio tu naweza bali atanifungulia. Akakaa chini na kunielekeza nini cha kufanya, hatua kwa hatua. Kufumba na kufumbua issamichuzi.blogpot.com ikazaliwa.

Nikamshukuru san asana na tukamuomba dada mmoja wa kizungu atupige picha, ambayo ndiyo nikaitumia kufungulia ukurasa wa kwanza wa Libeneke la Michuzi Blog, kama ambavyo picha hiyo ya huo ukurasa na maneno yake unavyothibitisha. 
 Siku hiyo ilikuwa Septemba 8, 2005 siku ya Alhamisi – Yaani siku ya Hepi Besdei ya Globu ya Jamii, ambayo tayari imetimiza miaka minane na siku nane leo. 
Najua kuna wataohoji kwa nini sikufanya sherehe ya siku hii. Ukweli ni kwamba nimeamua kuwa panapo majaaliwa nitafanya sherehe kubwa Globu ya Jamii itapotimiza miaka 10, ambayo ni Septemba 8, 2014 Mola akinijaalia uhai.
Leo naandika haya yote ikiwa ni kuonesha heshima na furaha yangu kwa Ndesanjo Macha, ambaye kwangu ni lulu iliyoniwezesha kufika hapa nilipo katika mambo ya libeneke. Awali nilikuwa namwita Mwana Mfalme wa Blogu, lakini leo, kwa ruhusa yako Ndesanjo, naomba nikuite Mfalme wa Blogu barani Afrika, baada ya kutunukiwa tuzo hiyo jana.

Najisikia fahari kubwa sana kuona mwalimu wangu wa kublogu ametunukiwa tuzo hiyo, ambapo hata na eye pia nahisi anajisikia hivyo kwani mwalimu hujisikia rah asana anapoona mwanafunzi wake anafuata yote aliyomfundisha bila kukoma. Nina imani hata kaka yangu Fidelis Tungaraza 'Mti Mkubwa' huko Helsinki aliko anakubaliana na mimi, maana yeye Fide ndiye alikuwa shuhuda wa kwanza wa mimi kuanzisha blogu kwa msaada wa Ndesanjo. Na hadi leo Fide amebaki kuwa mshauri wangu mkuu, akisaidiana na wanalibeneke wengine wenzangu wa mwanzo akina Jeff Msangi, Boniface Makene, John Mwaipopo, Freddy Macha, Asimwe Kabuga, Chemi Che-Mponda, Da'Mija na wengineo wengi.

Baadhi ya mambo mengi ambayo Ndesanjo alinifundisha wakati naanzisha Blogu ni uvumuilivu, kuwajua na kuwaheshimu wasomaji wako, na juu ya yote kukataa kulala bila kuposti yapo habari moja kwa siku.  “Huwezi kukosa habari japo moja kwa siku, na wasomaji wako kila siku watarudi kwenye blogu yako endapo kama utakuwa na kitu kipya kila siku ama kila mara”, aliniasa.

Nakumbuka usia mwingine mkubwa alioniachia ni kutoruhusu watu ama mtu kuchafua hali ya hewa ama kujeruhi nafsi ya mtu ama za watu, hasa linapokuja swala la kuhariri maoni ya watu wanayoyatuma kwa kila posti. Alinitahadharisha pia uhariri wa maoni ni kazi nzito inayohitaji umahiri wa hali ya juu pamoja na uvumilivu, kwani bila kufanya hivyo hadhi ama heshima ya blogu huporomoka haraka sana. Hayo yote nimeyafuata na naendelea kuyafuata, japo ni kweli kazi ni nzito sana, ikizingatiwa kwa siku inakubidi kupitia maoni kiasi hata cha 2,000 kwa siku na kuangalia kama yanakidhi ama la. Pia alinikumbusha kuwa si rahisi kumridhisha kila mtu katika hili, hivyo ujasiri na kuiamini unachokifanya ni muhimu. Yaani 'What's good for the goose is bad for a hen'

Nami sijutii  kutii ushauri wa Ndesanjo kwa hili, japo baadhi ya wadau ambao hupenda kupoza  hasira zao binafsi kwa kutoa maoni yanayojeruhi hisis za watu ama kuchafua hali ya hewa hawafurahii sana.

Somo lingine ambalo nalizingatia sana ni kusaidia bloga wengine kwa namna yoyote ile bila uchoyo. Hili nadhani wadau mnaona wenyewe ninavyotambulisha ma-Libeneke ya wadau wengine bila kusita kila wanaponiomba nifanye hivyo. Najisikia fahari kubwa kutekeleza mafunzo ya Ndesanjo kwa vitendo kiasi hata asilimia kubwa ya blogu kubwa hapa Tanzania, na hata nje ya nchi, zina mkono wangu wa msaada. Si ustaarabu kuzitaja blogu hizo kwani Ndesanjo hajawahi hata siku moja kusema hadharani kuwa ni yeye aliyenisaidia kuanzisha blogu.  Nadhani mabloga wengine pia watafuata ushauri huu ambao kwa kweli umetunufaisha wengi.

Kunradhi kwa kuchukua muda wenu mwingi na kuwanyima safu ya upigaji picha ya kila Jumapili ambayo leo imebidi ikae kando kumpisha Mfalme wa Blogu Afrika, Ndesanjo Macha.

Naomba kuwasilisha
-ANKAL


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. Kwanza kabisa ningependa kuipongeza blog kwa kusherehekea kuzaliwa kwake,Happy Birthday.Ila ningeomba kukusahihisha kuhusu umri unaosheherekewa.Kama ilianzishwa 8.9.2005.basi leo itakuwa ni miaka saba na siku nane,na siyo nane.Na mwakani 2013 itatimiza miaka tisa na siyo kumi.Ninavyoelewa huwa tunaaza kuuhesabu mwaka baada ya mwaka mmoja tokea tukio lifanyike.Sipendi kuchafua hali ya hewa ila naona hii shida inayojitokeza mara kwa mara.Ni majuzi tu mliturushia picha za jubilee ya miaka 50 ya ndoa ya Che-Mponda's ambao walifunga ndoa mwaka 1961,kwa hiyo ilipaswa iwe ni miaka 51 ya ndoa na siyo 50.Mwaka jana 2011 ndiyo walitimiza miaka 50 ya ndoa yao,labda kama haikuwezekana kusherehekea jubilee yao kwa sababu zisizozuilika wakafanya mwaka huu,basi ilibidi ielezwe lakini kimahesabu ni kama nilivyoeleza hapo juu.
    Anyway narudia tena kuomba msamaha na kuwatakia wana blog hii Happy Birthday ya miaka saba(7)na pia wanandoa Che-Mponda's jubilee njema ya miaka 51 ya ndoa yao.Mungu awape wote maisha marefu ya afya njema na kazi njema.

    ReplyDelete
  2. Absolutely fantastic story. Nimejifunza mengi saana ANKAL. lamaana-tu, ni kwamba umefunzwa ukafunzika, na sasa umekuwa mkufunzi aliye kubuu, ndio maana huja sahau ulikotoka.

    ReplyDelete
  3. Kaka Michuzi,
    Hongera saaana, mimi blogu yako ni kama chai na chapati, na maharage (zege) bila hiyo kazi haifanyiki ofisini.
    Pili, nakupongeza kwa kushukuru, tunapaswa kutoa shukrani kwa watu wanakutendea makuu. udumu kwa kuwa mtu wa shukrani.

    Mama G.
    Kijitonyama

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...