Waziri Mkuu wa Mstaafu wa Uingereza, Bw. Gordon Brown akizungumza wakati wa mkutano wa Viongozi wa Umoja wa Afrika walipokuta Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa sambamba na majadiliano yanayoendelea ya Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa. Viongozi hao waafrika walikutana kujadiliana Azimio la mpango wa AU kuhusu Ugonjwa wa Ukimwi ambapo pamoja na mambo mengine walikubaliana kuongeza kasi ya utekelezaji wake na uwekezaji ili kuukabili ugonjwa huo. Katika Mchango wake, Bw. Brown ambaye ni Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, aliwahimiza viongozi hao (hawapo pichani) kuhakikisha kwamba wanaipa elimu umuhimu wa pekee kwa sababu ni kwa kupitia elimu ndipo wananchi wanaweza siyo tu kujikinga na maambukizi bali hata kuudhibiti ugonjwa huo. Katika maelezo yake alielezea pia namna alivyotiwa matumaini na mtoto mdogo wa kitanzania alipoitembelea Tanzania mwaka 2005 na kupata fursa ya kumpakata mtoto huyo ambaye alifiwa na wazazi wake wote wawili, ili hali yeye mwenye akiwa ameambukizwa na akiugua kifua kikuu, lakini pamoja na udhaifu wote mtoto huyo alionyesha macho ya matumaini. Ni matumaini aliyoyaona kwa mtoto huyo ndiyo yanayomfanya mpaka leo hii , Gordon Brown kuamini kwamba yapo matumaini ya kuukabili ukimwi kupitia mipango mbalimbali na kubwa zaidi fursa ya kila mtu kupata Elimu.
Wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Rusibamayila na Dk. Mmbado wakifuatilia mkutano wa viongozi wa afrika kuhusu ukimwi.
Mhe. Vita Kawawa akifuatilia mkutano wa wabunge
wanaohudhuria mkutano wa 67 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. mkutano
huo uliandaliwa na Inter-Parliamentary Union ( IPU), katika
mkutano huo wabunge walibadilishana mawazo kuhusu wajibu wa mabunge na
wabunge katika kusimamia utawala wa sheria, kuhakikisha kwamba wananchi
wanapata fursa ya kuzijua sheria zilizopo pamoja na mbinu mbalimbali
zilizolenga kuwajengea uwezo wabunge wa kuzifahamu sheria na kuzijengea
hoja. Aidha wabunge hao walielezwa kwamba mbunge anayechaguliwa kwa
njia halali bila rushwa au sheria kupindishwa anakuwa na nafasi nzuri ya
kusimamia sheria na kuzitetea n akuwatetea wananchi. Kwa upande wake
Mbunge Kawawa akichangia majadiliano hayo aligusia pamoja na mambo
mengine mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili mitatu, nafasi ya bunge
katika kuisimamia serikali pamoja na uundwaji wa taasisi mbalimbali
zinazolenga kumsaidia mwananchi wa kawaida kupata haki zake za kisheria.
Waziri wa Katiba na Masuala ya Sheria kutoka Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar Mhe. Abubakar Khamis Bakari ( Mb) akichangia
majadiliano kuhusu Ujenzi wa Amani: kuelekea amani endelevu na usalama.
Mkutano huo wa Kilele ulikuwa umeandaliwana kamisheni ya Ujenzi wa
Amani. katika mchango wake Waziri Khamis pamoja na mambo mengine alisema
kwamba Tanzania ikiwa nchi Mwanzilishi wa Tume ya Ujenzi wa Amani
ya Umoja wa Mataifa ilikuwa inasisitiza umuhimu wa nchi zinazotoka
katika vita kumiliki yenyewe ajenda zake za maendeleo na ujenzi wa nchi
zao badala ya kupandikiziwa ajenda au nini wanatakiwa kufanya kwa vile
tu wanahitaji kusaidiwa. aidha akasema Tanzania inaamini zaidi katika
vitendo badala ya maneno na ahadi zisizotekelezwa.
Ujumbe uliofuatana na Katibu Mkuu Kiongozi wakati wa
uzinduzi wa Taarifa ya Kamisheni ya Kimataifa ya masuala ya
Uchaguzi, Demokrasia na Usalama hiyo, uzinduzi ambao umefanyika
sambamba na Mkutano wa 67 wa Baraza Kuula Umoja wa Mataifa.
RTaarifa hiyo inasisitiza umuhimu wa uadilifu katika chaguzi mbalimbali,
ambapo nchi zote duniani isipokuwa 11 zimefanya chaguzi katika miaka ya
hivi karibuni. Kutoka kushoto ni Balozi Liberata Mulamula, Mhe. Vita
Kawawa (Mb), Katibu Mkuu Kiongozi na Mhe. Musa Hassan Mussa (Mb).
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue, akichangia
majadiliano wakati wa uwasilishaji wa Taarifa ilyoandaliwa na Kamisheni
ya Kimataifa ya masuala ya Uchaguzi, Demokrasia na Usalama. kamisheni
hiyo inaongozwa na Bw. Kofi Anna, Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa
Mataifa. katika mchango wake, katibu Mkuu Kiongozi alisema misaada au
ufadhili hasa kutoka nje unaleta changamto kubwa hasa ikizingatiwa
kwamba nchi nyingi zinazoendelea hazina mifumo ya udhibiti wa misaada
hiyo. aidha pia akasema nchi nyingi zinachangamoto ya kujenga utamaduni
wa vyama vya upinzani kuheshimu matokeo ya uchaguzi na kutoa
ushirikiano kwa chama tawala ili kitekeleze ilani yake kwa mafanikio
na kwa faida ya wananchi waliowachagua. kama hiyo haitoshi akaongeza
kwamba Tanzania inaheshimu na kuthamini ushiriki na mchango wa makundi
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na makundi ya wanawake na imedhamiria
kufikia ushiriki wa asilimia hamsini kwa asilimia hamsini baina ya
wabunge wanawake na wanaume.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...