Eid Mubarak Ankal!
Aisee nipe lau nafasi nipate kusema kidogo ooo Ankal, moyoni
naugua.
Ni kuhusu hii dhana ya maadili ya Mtanzania. Aghalab
utasikia kitendo Fulani ni kinyume cha maadili yetu, ama kuvaa aina Fulani ya
kivazi (mfano vichupi kwenye umiss ama umodo) tunaambiwa ni kinyume cha
maadili. Wakati nakubali kwamba kuna maadili na yana umuhimu mkubwa katika
jamii, lakini nababaika na kupepesa sana macho na hii dhana nzima ya kuwepo ama kutokuwepo na
maadili rasmi ya Mtanzania, maana sijayaona pahala popote zaidi ya kusikia
yakitamkwa. Je, ni dhana ya kufikirika ama ni nini?
Yaani hata kwenye katiba ya nchi hayamo (labda yaletwe
kwenye hii Katiba mpya ijayo). Sasa moyoni huwa naugua sana nikisikia mtu
anasema kitu fulani ni kinyume na maadili yetu. Je, ni maadili gani hayo katika
nchi yenye makabila takriban 120, dini tofauti kibao pamoja na itikadi za
kisiasa zinazotofautiana? Aidha hayo maadili, pamoja na kuuliza yako wapi, na ni
nani katunga, kwa nini dhana hii ipo? Na kama maadili yapo mtunzi alimlenga nani na lini? Samahani
kama lugha gongana katika hili, ila nahisi nimeeleweka.
YAANI MAADILI YA MTANZANIA NI YEPI, KATUNGA NANI, LINI, NA
NANI ANAYAHIFADHI KWA MAANA YA KJUCHUKUA HATUA DHIDI YA WAENDAO KINYUME??
Kwa kifupi Ankal naomba uniulizie kwa wadau kuhusu dhana hii
ya maadili. Sina nia ya kuchafua hali ya hewa wala hamu ya kujeruhi hisia ya
mtu kama yalivyo maudhui ya Blogu hii ya Jamii. Nami nategemea michango
itayoletwa hapa ijadiliwe kwa kuzingatia hayo maudhui. Pia izingatiwe hapa mie siongelei
sheria ama kanuni rasmi za mamlaka ya nchi ambazo zimo vitabuni na zinaeleweka.
Naomba Kuwasilisha
Mdau Feri


ASANTE MDAU.SIO WEWE PEKEE MWENYE KUJIULIZA SWALA LA MAADILI YA MTANZANIA. NIONAVYO MIMI LINATUMIWA SANA KWA MANUFAA YA WACHACHE.
ReplyDeleteHOJA HII NI NZITO. ASANTE
Ukweli na uwazi ni kuwa Jamii ya Mtanzania imeanguka mno kimaadili.
ReplyDeleteKwa sasa hivi taswira kuu ni kama hii,
1.Kusikia neno 'shikamoo' mdogo akimpa mkubwa ni mara chache mno.
2.Imekuwa ni fasheni lugha kutokuwa na staha miongoni mwa watu, mfano matusi kutumika zaidi kwenye lugha na kutumika kama msisitizo ktk kauli za watu.
3.Mavazi ndio usiseme jamii hapa imeanguka mno si kwa vijana wavulana kwa wasichana usishange ukamkuta mtoto wa kuome akavaa suruali karibia makalio yote yako wazi wanaita kata-k.
4.Hakuna heshima baina ya familia mke kwa mume, watoto kwa wazazi.
5.Heshima imekuwa ni kitu adimu sana miongoni mwa watu ktk jamii kiasi kwamba anayeonekena anajiheshimu anachukuliwa kama amepitwa na wakati.
Maadili ya mtanzania yapo ndugu.Tuna makabila zaidi ya 100 lakini tuna vitu ambavyo ni COMMON kwa kila kabila(vinafanafana-na ndiyo maadili hayo),mfano kama walivyosema wadau hapo juu-Mtoto kutoa shikamoo..kila kabila,hakuna binti anaruhusiwa kuvaa vimini(Kabila gani linaruhusu),Mvulana kusuka nywele,kuvaa hel/reni ;Kijana kupita barabarani amekumbatiana na binti...sema hapo?Wanawake walioolewa kutembea usiku peke yao (hee hee),wasichana kuolewa bila Bikra.......ngoja niishie hapa Ankal
ReplyDeleteNaona huyu mdau hamjamwelewa vizuri swala lake.Ni swala la muhimu na la kufikiri kwa kina sio la kirahisi kihivyo. Hata mimi niliwahi kulifikiria sana. Kwanza kuhusu hiyo shikamoo waheshimiwa mnaijua historia yake na utumikaji wake.Pwani kwenye kiswahili kilipoanzia wala haitumiki tokea Kenya mpaka Tanzania,je wajua kwanini?Je wajua tuna makabira mengi wanaume wanatoboa masikio na kuvaa hereni,tena makabira mengi tu na ni utamaduni wetu kabla hata mkoloni hajaja kutufundisha sisi wasomi ustaarabu wa kuvaa suti nzito na tai kwenye joto la Dar es Salaam. Je unajua tuna makabira yetu wanaume wanafunga rasta(dreads),usukumani ukimwona rasta basi ujue ishara ya mganga wa kienyeji,wamasai wanasuka tena wote hawajaanza leo.Ndugu zangu hamjaangalia makabira yetu kuhusu mavazi na kuacha sehemu wazi sio uhuni ni utaratibu tu wa mila na desturi za jamii ndio maana unaona binti wa kihindi wa miaka 7 na bibi wa miaka 70 wamevalia vizuri lakini tumbo na mgongo wanaancha wazi na ndugu zetu kule kusini kwenye ngoma zao kina dada na mama vifua wazi na jamii wanaona kawaida tu kama vile mmasai anapokatisha mjini na lubega wakati kakuachia paja toka juu mpaka chini wazi tena kasuka na bangili kibao mwanaume wa shoka.Haya sasa turudi kwenye swali la msingi la maadili na mtanzania na tuisome vizuri tena message ya mdau wa kwanza.
ReplyDeleteMdau wa 01:00 pm na mdau wa kwanza nawaunga mkono kwa kumuelewa vizuri sana mtoa hoja na kujaribu kufafanua.Ukweli ni kwamba sisi tumekuwa tunaburuzwa tu na tunafuata bila hata kujua asili ya yote tunayofikiri kuwa ni(maadili)mazuri.Walipokuja wakoloni walitukuta na tamaduni zetu nzuri mavazi ikiwa ni moja wapo,(aidha kujifunika sehemu nyeti au nusu ya mwili inategemea na sehemu kwa sehemu)basi wao walivyokuja na dini zao wazungu na ukristo wao na waarabu na uislamu wao wakaanza kutubadilisha siyo tu kiimani ila mpaka mila na tamaduni zetu na mavazi,salamu/kusalimiana vikiwa baadhi ya orodha ndefu.Shikamoo haikuwepo katika salamu zetu kwa makabila yote na kitu cha kusikitisha unakuta mtu akiwa na uwezo au madaraka hata kama kiumri ni mdogo wakati mwingine hupewa hiyo shikamoo ambayo ni salamu ya kitumwa.Makabila mengi yana salamu maalum kwa watu wa tabaka au umri fulani na ambaye hayupo katika hilo kundi hastahili hata awe tajiri au mwenye madaraka fulani,lakini kwa hii shikamoo una kuta mzee wa umri wa kukuzaa anamuamkia mtu mdogo.Kuhusu hayo mavazi ndiyo hata hii blog nzima naweza kuijaza kwa maelezo.Walipokuja wakakuta jinsi tunavyovaa walisema hatujastarabika wakatufundisha kuvaa kikwao "kimagharibi/ulaya au kijangwani/kiarabu.Waulaya walihitaji kuvaa nguo kwa ajili ya kujikinga na baridi ya ulaya na waarabu pia walijifunikiza kutoka kichwa hadi miguuni kujikinga na jua kali la jangwani wasiunguze miili yao,sasa sisi wa bara la afrika hali yetu ya hewa ni nzuri kiasi kwambaa tulisitiri tu sehemu nyeti.Kwa nini nasema tunaburuzwa?walitufundisha kuvaa kikwao,walikataza wanaume wasisuke nywele,rasta au kuvaa hel/reni shanga na bangili.Kutoboa ndonya kwa makabila mengine,kuchanja chale mwilini n.k.sasa hivi wanafanya hivi vitu vyote tena kwa gharama na fahari kubwa,wanatembea nusu uchi kabisa yale ambayo walisema si ustaarabu.Sasa sisi tumebaki kuhukumiana kwa kutoa kasoro nani kavaa nguo gani au hakujifunika sehemu gani,katoboa pua,sikio au sijui nini,kasuka nywele gani au rasta,sijui kachora tatoo ooh hawana maadili sijui hawana adabu...Jamani kweli maadili ni nini/yapi?Basi tunavurugwa tu na sisi tunavurugana kwa kuhukumiana,ooh nguo fupi hana heshima,wakati miaka ya nyuma tuliona mama/dada zetu wakivaa nguo zilizo juu ya magoti na walihesimika na kuheshimiwa bila ya kusakamwa leo hii utaitwa 'malaya' kumbe hata ukijifunika kutoka kichwani mpaka miguuni unaweza ukaufunika huo U-'malaya'na wakasema ooh fulani ana heshima sana tazama anavyovaa nguo za heshima!!?Usipovaa suti na kufunga tai basi utasemwa hujavaa kwa heshima hivi jamani joto la Dar kujinyonga kwa suti na tai wapi na wapi?unaona kabisa mtu anateseka kwa joto lakini yumo tu.Na haya yote ndiyo yanatufikisha pia kwenye kaugonjwa ka 'TITLES'mtu kuitwa sijui nanihii...,lakini walala hoi wao hawastahili hizo'TITLES'ukienda mfano hosp.utasikia walala hoi wanaitwa labda kuingia kwa daktari."Sofia Jonh,Ashura Ramadhani,Juma Abdallah,Kalubandika Kijakazi" n.k.hawapaswi kuitwa Mr/Bw.Mrs/Bibi,Miss/Bi na kubwa ya yote Mheshimiwa n.k.Ndiyo maana Nyerere alisama wote tuitane Ndugu .. ilikuwa safi sana.Samahanini kwa maelezo marefu lakini siwezi kumaliza.Hebu tuyafanyie kazi mawazo ya mtoa hoja ametoa hoja muhimu sana katika wakati huu tulipo wa kutojua uelekeo wetu.Shu krani na samahani kwa maelezo marefu.
ReplyDeleteKuna mambo ambayo ukiangalia katika makabila yote nchini yanafanana. Hayo naweza kusema ni maadili yetu. Mojawapo ni suala la heshima ya mtu kutokana na utu. Mtu mzima ana namna ya heshima anayompa mtoto hali kadhalika mtoto ana namna ya heshima anayompa mtu mzima. Kwa mfano, kama mtu mzima anaongea mtoto anasubiri mpaka mtu mzima amalize ndipo naye kama ana la kusema analisema. Makabila yote nchini yana hali kama hiyo. Heshima yetu ya asili haikuwa inatokana na wingi wa mali.
ReplyDeleteSalamu ya shikamoo marahaba sio suala la maadili ya Mtanzania. Asili ya salamu hii ni Waarabu na maana ya shikamoo ni 'nipo chini ya miguu yako'. Ukiangalia lugha zetu za makabila, kuna makabila yana mgawanyiko wa salamu na kuna makabila ambayo salamu ya mtoto kwa mkubwa ni sawa na salamu ya mkubwa kwa mtoto. Kwa mfano, Wakinga husalimiana "Mapembelo!" "Va vene!". Iwe ni mtoto au mkubwa anayesalimia, salamu ni ile ile. Heshima ya Watanzania haitokani na hela.
Kuna suala la kusaidiana katika matatizo. Jirani akifiwa kila jirani anashiriki kadri anavyoweza. Kwenye mataifa ya magharibi kuna makampuni yanafanya kazi ya shughuli za mazishi. Kitu hicho hakipo katika utamaduni wetu.
Kadhalika kwenye sherehe majirani hualikana. Huu utamaduni mpya wa kuchangishana kwa mfano michango ya harusi halafu hupati mwaliko bila kuchangia ni mambo ya kigeni.
Hili siwezi kulisemea kwa uhakika lakini kuna heshima maalumu kwa baba na mama mkwe. Hii ni mifano michache. Wengine wataongezea.
WADAU KAKAKUONA NA HUYO HAPO JUU MMEIPATA MADA HASWAA NA MAELEZO YENU NI SAHIHI. UTAMADUNI WA MTANZANIA NI KUHESHIMIANA, KUJALIANA. UKIINGIA KWENYE DALA DALA UNAMJULIA HALI ALIYEKAA KARIBU NAWE NDUGU HABARI YA LEO? UGHAIBUNI HAKUNA HILO. UKIMWONA MTOTO ANASHANGAA BARABARANI UNAMUULIZA JE KUNA TATIZO? WATOTO WAKIPIGANA MKUBWA UNAAMUA NA KUHAKIKISHA AMANI INAPATIKANA KWA SABABU WATOTO NI JUKUMU LA JAMII. ULAYA MGUSE MTOTO WA MTU KAMA HUJAKUWA ARRESTED AU KUCHOMWA KISU. BASI HAYA NI MIONGONI MWA MAADILI YETU, KUJALIANA, KUSHIRIKIANA NA KUTOONGELEA MAMBO YA NDANI YA BINAFSI ADHARANI.
ReplyDelete
ReplyDeleteMaadili ya m TZ Genarally hutayapata. Kama wachangiaji wengi walivyokwisha kueleza.
Makabila ndio yanawakilisha hili, ambapo mengi yanaingiliana na makabila mengine pamoja na wa afrika wenzetu hasa wabantu wenzetu.
Kwani wewe kabila gani? kaanzie huko.
Walitunga wahenga, ambao pia walitunga misemo, nahau, methali na kadhalika.
Tudumishe mila na utamaduni wetu, ambao kwa kifupi LENGO ni kudumisha:
HESHIMA.
ADABU.
NIDHAMU.
KUCHAPA KAZI.
KUWA NA HAYA/AIBU.
KUSAIDIA WAZEE, WATOTO, WANAWAKE.
KUTOKUWACHEKA WALEMAVU.
KUTOKUKEJELI MTU MWENYE MATATIZO.
-Mtu 'akifulia' isiwe ndio subject ya kutuchekeshea
UKARIMU.
KUCHUKIA/KUACHA UCHOYO.
KUKANYA WATOTO WANAPOKOSEA HATA KAMA SIO WA KWAKO.
KUKUBALI WATOTO WAKO KUKANYWA/KUKARIPIWA NA MTU MWINGINE.
KUOGOPA WAKE/WAUME ZA WATU.
KUEPUKA ZINAA.
Na mengine mengi ambayo yamehifadhiwa kwenye hadithi za bibi au babu kwa wajukuu zao kabla ya kulala usiku, methali, nahau, misemo na kadhalika.