Leo nimesoma katika gazeti moja la Kiswahili kuwa timu ya Azam (Azam FC) wamemfukuza kocha wao baada ya sare mbili mfululizo zikifuatiwa na kufungwa na Simba. Kilichonishtua ni kwamba habari hii nimeiona kama ya kawaida sana. Ufukuzwaji wa makocha umekuwa jambo la kawaida mno, hata nadiriki kusema kuwa umekuwa utamaduni mpya wa klabu zetu za soka. Kwa kweli siamini kuwa hili jambo ni sawa hata kidogo kutokana na hoja zifuatazo:

1. Kocha ni sehemu moja tu ya timu. Katika timu pia kuna wachezaji, viongozi (ambao humtafuta/humsaili kocha), mashabiki, vyama vya soka, n.k. Pia kuna vitu vingine kama uwanja, waamuzi, n.k. Ni kweli kuwa hizi timu zetu zikifungwa ama kutoka sare kosa huwa ni la kocha pekee? Uamuzi wa kumfukuza kocha hutokana na uchunguzi ili kubaini tatizo katika mfumo mzima ama hasira kwa vile kocha ndiye mwalimu? Kwamba muumini wa dini akienda kinyume na maandiko basi dhambi huwa ni ya kiongozi wa dini? Je, mtoto wa umri wa chini ya miaka 18 akilewa pombe kosa ni lake binafsi, la wazazi/walezi wake, la mmiliki/meneja wa baa, la kampuni ya bia, la sheria za nchi, ama la nani? Kila leo tunasisitizana kuwa "tucheze kama timu", "sisi wote ni kitu kimoja" n.k. kwa maana gani hasa, kwamba tunacheza kama timu ila tukifungwa kosa ni la kocha? 

2. Ni timu gani mnazozijua hapa duniani ambazo huwa hazifungwi? Ninachokijua mimi kila timu hufungwa, hata iwe kubwa namna gani? Achilia mbali Azam kufungwa na Simba (timu kubwa nyezie), Simba hiyo hiyo inaweza kufungwa ama kudroo na timu iliyo daraja la tatu. Hivi mmeshawahi kutafakari kwa kina hali hiyo husababishwa na nini hasa ama ni suala la ushabiki na kasumba tu kuwa kosa ni la kocha? Huwezi kumuadhibu mwanao eti tu kwa sababu amefeli mitihani, ni lazima utafiti kujua kwanza vitu gani huchangia kumfanya mtoto afaulu kisha upime kama alivipata. Pengine hana muda wa kutosha wa kusoma kwa vile anapaswa kufanya kazi kusaidia maisha ya nyumbani, ama kuna wakati akiwa anajiandaa na mitihani alikumbwa na tatizo ambalo lilimuathiri kisaikolojia na kimorali, ama hapati chakula awapo shuleni, n.k. Je, akifeli basi aadhibiwe tu ama apewe pole na msaada anaouhitaji ili afanikiwe kimasomo? Iwe ManU, Brazil, Kagera Sugar, Matikiti maji FC, n.k., zote ni lazima zifungwe tu, zitake zisitake! Ni lazima tutafakari upya badada ya kugeuza ufukuzwaji wa makocha kuwa tabia yetu mpya. Tunawaharibia hawa makocha CV zao walizozijenga kwa bidii na muda mrefu kwa ajili ya uvivu wetu wa kufikiria na ushabiki usio na mantiki ya kimaendeleo. 

Ni hayo tu kwa sasa.

Mdau, Canada.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Azam bana walibugi stepu! Stewart Hall hakustahili kufukuzwa hapo awali. Isitoshe, akaenda Kenya na kubwabwaja hovyo kuhusu soka la tanzania na sasa wanataka kumrudisha tena.

    Walipomfukuza tuu nikasema ndio mwanzo wa mwisho wa Azam kuelekea kuwa timu ya kawaida tuu!!!

    ReplyDelete
  2. Timu ikifungwa lazima kufanyike mabadiliko. Moja katika hayo ni kocha. Kocha ndiye mwenye kupanga timu, kutafuta wachezaji, kufundisha wachezaji. Sasa timu inapofungwa itakuwa kocha hakufanya wajibu wake.

    ReplyDelete
  3. Kama kocha hawezi kazi mkae nae wa nini? timua haraka. Mfano mzuri ni yule kocha wa Chelsea, angalia mafanikio yaliyopatikana baada ya yeye kutimuliwa!

    ReplyDelete
  4. Sasa unataka tufanyeje? Timu ifungwe mpaka zishuke daraja? Washabiki waache kuzi-support financially? Na washabiki wakipungua na hata sponsors kujitoa maana yake timu haitoweza ku-generate pesa za kulipa wachezaji/viongozi. Ndio maana kocha anakuwa wa kwanza kuwajibishwa.

    Unajua mchezo wa soka ni results oriented sport na kama timu inafungwa basi kosa linakuwa kwa kocha, na hii inaeleweka hata na wazungu ambao wao pia hufukuza makocha ktk timu zao kama mbwa mwitu. Kama unafuatilia soka utagundua kwamba mara tu kocha mpya anapoichukua timu matokeo yake huwa mazuri, na hii inathibitisha kwamba kosa kubwa linakuwa la kocha kutokana na mambo makuu matatu ambayo ni:

    1. Kutoweza kuwamotivate wachezaji wake
    2. Tactics zake zimefail.
    3. Kusajili wachezaji kwa pesa nyingi ili wafiti system aitakayo halafu wachezaji wanashindwa kudeliver.

    Unajua timu ikifungwa sana inakuwa haiwavutii washabiki wake matokeo yake wanakaa nayo mbali maana wanajua wakienda uwanjani kuishangilia wanarudi nyumbani na huzuni baada ya kuona timu yao kuchapwa. Sasa hapa utaona kuna swala la uchumi wa timu lina kipaumbele sana ndio maana kocha, kama mhusika mkuu wa tactics/kununua wachezaji/kumotivate na ku-implements his playing system inabidi aachie ngazi ili kuvutia na ku-winn more fans ili waongeze pato la timu.

    Sioni umuhimu wa article yako, maana hakuna geni hata moja ndani yake maana hata Serie A, Bundesliga e.t.c. zinafukuza makocha, tena wengi kwa msimu kuliko hata Bongo.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...