Na Mwandishi maalum
Nongwa na mgomo baridi unaofanywa na wachezaji wazalendo wa Simba inatokana na uwiano usio sawa wa mishahara baina yao na wachezaji  wageni, kiasi hata  timu hiyo kuboronga katika mechi zake za ligi kuu ya Tanzania Bara.
 
Uchunguzi umebaini kuwa, baadhi ya wanasoka wazalendo hawafurahii wenzao wa kigeni kulipwa mishahara minono wakati mchango wao katika timu ni mdogo.
 
Uchunguzi huo umegundua kuwa, hali hiyo imewafanya wachezaji hao wacheze chini ya kiwango kwa lengo la kuushinikiza uongozi kuweka uwiano mzuri wa mishahara.
Mchezaji mmoja mwandamizi wa timu hiyo, alitoa mfano wa wachezaji kama Komabil Keita na Paschal Ochieng, ambao alidai wanalipwa mshahara wa shilingi milioni 1.5 kwa mwezi, lakini wamecheza idadi ndogo ya mechi hadi sasa.

Mchezaji huyo alisema kuwa, viwango vya mishahara kwa wachezaji wazalendo ni kati ya shilingi laki tano na milioni moja wakati kiwango cha juu kwa wanasoka wageni ni shilingi milioni tatu. Felix Sunzu, raia wa Zambia ndiye mchezaji ghali kuliko wote katika klabu ya Simba akiwa analipwa mshahara wa shilingi milioni tatu wakati Mganda Emmanuel Okwi naye amekuwa akishinikiza kuongezwa mshahara katika mkataba wake mpya.
 
Kwa sasa, Okwi anaramba shilingi milioni 1.5. Wachezaji, ambao wamekuwa wakitajwa kulipwa kiwango kidogo cha mshahara wakati mchango wao ni mkubwa katika timu ni pamoja na Shomari Kapombe, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Nassor Masoud 'Cholo'. Mrisho Ngasa, ambaye amesajiliwa na Simba akitokea Azam, analipwa mshahara wa shilingi milioni mbili wakati Kapombe anakunja shilingi laki saba baada ya kupandishiwa hivi karibuni kutoka shilingi laki tano.
 
Kwa mujibu wa chanzo chetu hicho, mgomo huo ndio uliosababisha Simba ilazimishwe kutoka sare ya bao 1-1 na Polisi Morogoro kabla ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar, na juzi Jumamosi kulala kwa bao 1-0 dhidi ya Toto African katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam .
 
Alipoulizwa, kiongozi mmoja wa Simba alikiri kutambua kuwepo kwa mgomo huo na kuongeza kuwa, wanatarajia kukutana hivi karibuni kujadili hatua za kuwachukulia wachezaji wanaowashawishi wenzao kucheza chini ya kiwango.
 
Simba, ilianza ligi kuu kwa kishindo na ushindi wa mfululizo, lakini katika siku za hivi karibuni imekuwa ikidorora na kujikuta ikimaliza mzunguko wa kwanza ikishika nafasi ya tatu nyuma ya Azam na Yanga, na kuchafua rekodi yake kwa kupoteza michezo miwili, dhidi ya Mtibwa na Toto African.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. Kwani ligi ilipoanza walikuwa wanalipwa sawa? Na mikataba waliyosaini, haikuwa na kiasi cha mishahara?

    ReplyDelete
  2. Poa sana wachezaji wazawa wa Simba komaeni hadi kieleweke na kikieleweka ndiyo mwali kashachukuliwa na Yanga.Kilio cha kuku ni furaha ya kunguru ,Yanga wanachekelea tu ,mtajiju.

    ReplyDelete
  3. kumbe mikataba mibovu si kwa wanasiasa tu bali hata wachezaji wazawa huwa wanasaini mikataba mibovu halafu mwisho wa siku wanalalamika.

    ReplyDelete
  4. Huu ni ushamba tu; hamuwezi wote kulipwa sawa - hii siyo siasa ya ujamaa bali ni mpira wa kisasa na biashara papo hapo. Acheni ujinga wachezaji wa kitanzania ambao miaka 50 sasa hamjachukua hata kombe moja barani Afrika. Hovyooo!

    ReplyDelete
  5. Mtakoga Mabao mapaka mwisho na KOMBE MOJA KWA MOJA NI JANGWANI !

    YANGA BINGWA 2012-2013.

    ReplyDelete
  6. Mikataba mibovu Wachezaji wa Kibongo ni kuwa hamjui Kiingereza!

    Mmeona umuhimu wa Elimu sasa?

    ReplyDelete
  7. Mimi si mpenzi wa Simba lakini naweza kuchangia kwa ujumla.Wachezaji wageni kulipwa zaidi ya wazawa si kitu cha ajabu.Ni sawa na kazi zingine duniani(fani zingine).Kuna watu wanafanya kazi kama Expats(expatriates) sina kiswahili chake kizuri lakini kwa lugha rahisi ni kwenda kufanya kazi nje ya nchi yako.Mara nyingi mishahara ya expats iko juu kuliko wazawa..LAKINI....Lazima Expat uwe na kitu cha ziada ambacho wazawa hawana.Na hapo ndipo ugomvi ulipo nadhani.Vile vile unaweza kuwa expat ukajikuta bado unalipwa kidogo kuliko wazawa-Hapo kuna kitu kinaitwa SALARY NEGOTIATION POWER(Maelewano ya mshahara kabla ya kusaini mkataba),hapo ndipo wachezaji wa Simba wanapopigwa bao(ELIMU).MSHAHARA ni siri sana kati ya mwajiri na mwajiriwa-Uongozi wa Simba unawajibika kwa hili.

    David V

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...