Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja (wa pili
kushoto) akibadilishana nyaraka na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Water
Resources Corporation ya Korea Kusini, Bw. Woo Kyu, Kang jijini Dar es
Salaam. Kampuni hiyo ya Korea itafanya
upembuzi yakinifu wa mradi wa uzalishaji wa nishati ya umeme na maji kwa
matumizi mbalimbali katika Bonde la Mto Ruaha mdogo. Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa bodi ya
RUBADA, Prof. Raphael Mwalyosi (kushoto) na afisa mwandamizi wa kampuni hiyo,
Bw. Jaemin NAM (katikati).
==================
|
Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la
Mto Rufiji (RUBADA) imesaini makubaliano na Water Resources Corporation (K
Water) ya Korea Kusini kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa uzalishaji wa
nishati ya umeme na maji kwa matumizi mbalimbali katika Bonde la Mto Ruaha
mdogo.
“Tumekuatana hapa leo kufikia
makubaliano na wenzetu wa Kampuni hii ya Korea Kusini kuanza kufanya upembuzi
yakinifu wa kuzalisha nishati ya umeme, kupata maji kwa ajili ya Manispaa ya
Iringa na maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji kwa wananchi wa maeneo
hayo,”alisema Mkurugenzi Mkuu wa RUBADA, Bw. Aloyce Masanja mbele ya waandishi
wa habari jana jijini Dar es Salaam.
Alisema Mkoa wa Iringa umepata bahati
ya kuwa na mvua za kutosha na kwamba mto huo unaweza kuwa chanzo kizuri cha
kuzalisha umeme, matumizi bora ya maji kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kwa ajili
ya kilimo cha umwagiliaji.
Maeneo ambayo yana uwezekano wa
kuzalisha umeme katika bonde hilo ni pamoja na maanguko ya Tosamaganga,
Manyandamonda, Ibosana Nginayo.
Alisema kampuni hiyo itafanya kazi
hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja ili kuona kama kuna uwezekano wa kupata huduma
zote za umeme, matumizi ya kawaida na umwagiliaji au kupata mojawapo.
Alisema mwaka 1984 Shirika la Kimataifa
la Maendeleo la Norway NORAD lilifanya upembuzi yakinifu katika eneo hilo na kubaini
kuwa linauwezo wa kuzalisha Megawati 87.
“Umeshapita muda mrefu, sasa tunataka
kuangalia kama bado uwezo ni huo la mambo yamebadilika,” alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
RUBADA, Profesa Raphael Mwalyosi alisema mto Ruaha mdogo una maji kwa kipindi
chote cha mwaka kutokana na mazingira mazuri ya mvua za kutosha.
“Tukifanikiwa katika hili itakua ni
kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa sababu Iringa inakua kwa kasi, kuna viwanda
na huduma za maji zinahitajika,”alisema Profesa Mwalyosi.
Alisema maji hayo yanaweza kutumika
katika matumizi mseto ikiwa ni pamoja na kuzalisha nishati ya umeme, kilimo,
mifugo na matumizi ya watu na hivyo kuwa chachu ya maendeleo.
Alisema ni muhimu kuhakikisha vyanzo
vya maji vinalindwa ili kuwa ma matumizi yanayoendana na mabadiliko ya tabia
nchi kwa ajili ya kuwa na mazingira endelevu.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya
Water Resources Corporation ya Korea Kusini, Bw. Woo Kyu, Kang alisema kampuni
yao ni kongwe na yenye uzoefu mkubwa.
Ilianzishwa mwaka 1967 na imejihusisha
na miradi mikubwa ya uzalishaji umeme ikiwemo ya nchini Philipines na Pakistan.
Alisema mradi wa Iringa katika Bara
la Afrika wanauchukulia umuhimu mkubwa kwa faida ya pande zote mbili.
“Tunashukuru kwa serikali ya Tanzania
kuonyesha uaminifu kwetu,” alisema.
Alisema wanategemea ushirikiano
mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali hapa nchini ili kukamilisha kazi
watakayoanza kufanya na kuahidi kuifanya kwa uaminifu na ufanisi mkubwa.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...