Kutoka kushoto Mbuyu Ali,Shamsa Hamud na Grace Lyon kutoka Vodacom Foundation wakihakiki majina ya wanufaika wa mradi wa MWEI katika shehia ya Nungiwi Mjini Zanzibar tayari kupokea fedha za mikopo kuendeshea biashara ndogondogo. Zaidi ya wanawake 230 wa Nungwi na Kiwengwa mkoa wa Kaskazini Unguja wamepatiwa mikopo nafuu yenye thamani ya shilingi 27 Milioni kutoka mradi wa MWEI ulio chini ya Vodacom Foundation.
Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika ya Zanzibar Asha Ali Abdula akifurahia jambo pamoja na Asha Haji mkazi wa Nungwi kabla ya kumkabidhi fedha za mkopo kutoka mradi wa kuwawezesha wanawake wajasiriamali wadogowadogo kiuchumi (MWEI). Kulia ni Meneja wa Vodacom Foundation Grace Lyon na Meneja Mahusiano ya Nje wa Vodacom Salum Mwalim. Kiasi cha Sh27 Milioni zimetolewa kwa wanawake 233 wa Nungwi na Kiwengwa Mjini Zanzibar.

Serikali ya Zanzibar (SMZ) imeipongeza kampuni ya Vodacom kwa kubuni na kuanzisha mradi maalum wa kuwawezesha kiuchumi wanawake wa M-pesa Women Empowerment Initiatives (MWEI) unaowajengea wanawake uwezo wa kukabiliana na maisha kwa kuwapatia mikopo nafuu ya baishara.

Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika ya Zanzibar Bi Asha Ali Abdula wakati wa hafla ya kukabidhi mikopo nafuu kwa wajasiriamali wanawake 230 wa Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A kupitia mradi wa MWEI ulio chini ya mfuko wa kusaidia jamii – Vodacom Foundation.

Zaidi ya wanawake 330 wa Nungwi na Kiwengwa wamepatiwa mikopo nafuu ya MWEI yenye thamani ya zaidi ya Shilingi 27 Milioni ambapo wastani wa Sh 10,000 hadi laki mbili hutolewa kwa mwombaji.

Bi Asha ameutaja mradi huo kama mkombozi kwa wanawake ambao licha ya kuwa na jitihada mbalimbali za kujikwamua kiuchumi wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali katika kufanikisha juhudi hizo.

Amesema wanawake wengi wa Zanzibar wamekuwa na mwamko wa kujishughulisha na biashara ndogondogo ili kupata fedha za kusaidia matumizi katika familia ikiwemo chakula, ada na vifaa vya shule hivyo kampuni ya aina ya Vodacom yenye kufanya biashara za simu za mkononi kuona umuhimu wa kuwawawezesha kiuchumi wanawake ni jambo linalostahili pongezi.

“Nachukua nafasi hii kwa niaba ya serikali ya Zanzibar kuwapongeza Vodacom kwa mradi huu wa MWEI, hii ni fursa ya kipekee kwa wanawake wa Zanzibar kupata mikopo isiyo na riba wala dhamana ambayo hatuna budi kuipongeza kwa kuwa inaendana na azma ya serikali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.”Alisema.

“Wanawake wenzangu wa Nungwi mikopo ya MWEI imeondoa vikwazo vya kupata mikopo…..mikopo hii haina dhamana na zaidi haina riba na hivyo inaendana hata na misngi ya dini hatuna sababu kushindwa kutumia vema fursa hii kujikwamua huku tukiwashukuru Vodacom.”Aliongeza Bi Asha.

Amesema kumkomboa mwanamke ni kuikomboa familia na jamii na kwamba chini ya uhamasishaji wa kauli mbiu ya Mwanamke akiwezeshwa anaweza ana Imani kubwa wanawake wa Nungwi watakuwa wa mfano wakitambua kuwa hata kikubwa kilianza na kidogo.

“Dhana ya uwezeshaji ni pana inahitaji taaluma ya biashara, mtaji na masoko…MWEI imetatua kikwazo cha mtaji kwa kutuwezesha mikopo nafuu na pia inatupatia elimu ya biashara kinachobaki ni kuwa na ubunifu wa mawazo bora ya biashara na kupata masoko ya bidhaa zenu”. Alisema Bi Asha.

Kwa upande wake Meneja Mahusiano ya Nje wa Vodacom Salum Mwalim amewataka wanawake walionufaika na mikopo hiyo kutambua kuwa suala la mtu kujikwamua kiuchumi huanza na dhamira sahihi na ya dhati ya mhusika.

“Mafanikio yenu yapo mikononi mwenu kila mmoja anapaswa kutambua kuwa kujikwamua kiuchumi kunaanzia ndani ya nafsi yake akiheshimu kila fursa anayopata na kunzia hapo unajifungulia milango ya mafanikio.”Alisema Mwalim.

Ameongeza kuwa “Inchofanya Vodacom kupitia MWEI ni kuwatengenezea wanawake fursa na kuwajengea uwezo kwa kuthamini nafasi yao katika jamii na baada ya hapo ni jukumu la kila mmoja kuheshimu kile MWEI ilichomuwezesha ili kujikwamua na hilo linawezekana na ni imani yangu kwamba ipo siku Nungwi itatoa mwanamke mjasiriamali mwenye mafanikio zaidi ambae historia ya maisha yake imeanza na MWEI.”Aliongeza Mwalim.

Mradi wa MWEI ulioanzishwa mwaka 2010 hadi sasa umeshawanufaisha wanawake zaidi ya 6,000 nchi nzima. Kwa mwaka huu zaidi ya shilingi 450 Milioni zimetengwa kuwafikia wanawake zaidi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...