Usiku wa kuamkia jana
Ijumaa Novemba 23, 2012, Wanareli wote nchini na hasa Wafanyakazi wa Kampuni ya
Reli Tanzania –TRL wamefikwa na msiba mkubwa kabisa kwa kuondokewa na Mpiganaji
asiyekata tamaa katika kutetea maslahi yao NDUGU EMMANUEL JOMOLEMA (pichani) ambaye kiwadhifa katika Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania –TRAWU
alikuwa Makamu Mwenyekiti –Taifa.
Marehemu
ambaye amezaliwa Januari 28, 1967 alijiunga na lililokuwa Shirika la Reli Tanzania
–TRC mnamo Januari mwaka 1989 mara baada ya kumaliza elimu ya Kidato cha 4
katika Shule ya Sekondari ya Shaban
Robert ya jijini Dar es Salaam. Baada ya mafunzo ya miaka 3 ( Januari 1989
–Oktoba 1991) katika Chuo cha Reli Nairobi , Kenya
katika fani ya fundi Stadi wa Mitambo alihamishiwa katika
Chuo cha Reli –Ratco Tawi la Morogoro na kuendelea na mafunzo hayo hadi Oktoba
1992.
Baada ya kuhitimu mafunzo hayo
Marehemu akaanza kulitumikia Shirika akiwa Fundi Mitambo Stadi hadi pale Oktoba
mwaka 2007 alipohamishiwa katika Kampuni ya Reli Tanzania –TRL na kuendelea na
utumishi wake hadi mauti yalipomkuta. Kuhusu harakati za kutetea haki za
wafanyakazi Marehemu Jomolema alizianza bila ya kuwa na wadhifa rasmi wa Trawu
kuanzia 1999 hadi 2002. Mwaka 2002 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Trawu tawi
la Karakana Dar es Salaam hadi mwaka 2011.
Halikadhalika
mnamo mwaka 2005 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Dar es Salaam Trawu ,
wadhifa alioushikilia hadi mwaka 2011 alipochaguliwa katika Wadhifa wa juu wa Makamu wa Mwenyekiti Trawu.-Taifa. Marehemu
akifahamu umuhimu wa kushirikisha wanaharakati wengine katika uongozi wa chama
kwa hiyari mwenyewe alijiuzulu nyadhifa za Uenyekiti wa tawi la Karakana Dar na Kanda ya Dar
Trawu.
Kimaisha Marehemu alijaaliwa kuoa na ameacha
watoto wawili. Marehemu Jomolema alilazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuanzia
Oktoba 16, 2012 akiwa anasumbuliwa na maradhi ya TB ya Mifupa.
Kwa mujibu wa Ndugu wa
Marehemu msiba uko nyumbani kwa Baba wa Marehemu Mzee
Jomolema maeneo ya Mwembe Yanga Temeke jijini Dar es Salaam.
Ratiba ya
Mazishi inaonesha shughuli za
mazishi zitaanza kesho Novemba 25, 2012
, mnamo saa 4 asubuhi mara baada ya kuwasilii
mwili wa Marehemu nyumbani. Kwa mujibu wa ratiba kuanzia saa 6 adhuhuri hadi 7:30 waombolezaji watapatiwa
chakula na kuanzia saa 7:30 hadi 8:30
utakuwa ni muda wa Ibada.
Ndugu, jamaa
na marafiki watapata fursa ya kumuaga marehemu kuanzia saa 8:30 mchana hadi saa
9 alasiri. Msafara wa mazishi utaondoka Mwembe yanga kuelekea makaburi ya Kinondoni
kuanzia saa 9 alasiri na mazishi yamepangwa kufanyika saa 10 jioni katika
makaburi ya Kinondoni ambako marehemu
atapumzishwa katika nyumba yake ya milele ! Bwana Ametoa , Bwana Ametwaa, Jina lake Lihimidiwe- Amina!
Imetolewa na
Afisi ya Uhusiano
Kwa niaba ya
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Reli
Tanzania
Mhandisi Kipallo
Amani Kisamfu
Dar es Salaaam
Novemba 24, 2012


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...