Baada ya majibizano ya hapa na pale kuendelea kwa muda mrefu baina ya Serikali, Wanaharakati na Wananchi wa Mikoa ya Kusini sasa inaonekana mgogoro huo kukua zaidi siku hadi siku. Ililipotiwa hapo kabla kuhusu Naibu Waziri wa Nishati kwenda usiku huko Msimbati na kufukuzwa, ingawaje Serikali kwa upande wake ilikanusha habari hiyo na kudai ni maneno ya kizushi na udanganyifu wa watu kujitafutia umaarufu.

Katika kile kinachoonekana kuwa ni hatari, asubuhi ya leo tumepata taarifa kwamba gari lililoenda kwa ajili ya kumbeba Bibi kwenda naye kusikojulikana limechomwa moto. Taarifa zinasema, watu kadhaa akiwemo kijana mmoja mwenye asili ya ukaazi wa kijiji hicho walikamatwa jana usiku na wanakijiji cha Msimbati wakidai wameagizwa kuja kumchukua Bibi huyo ili wakafanye maongezi na Wakubwa ambao pia hawakuweza kuwekwa bayana ni Wakubwa gani hao. Kinachoelezwa ni kwamba, baada ya mtafaruku huo, watu hao walichoropoka na kukimbia kitu kilichowapa hasira Wananchi na kuamua kuchoma gali hilo ambalo walikuja nalo.

Ni hatari, kwasababu mbali na propaganda za viongozi wetu wa Kitaifa kwamba suala la gesi ni la Wanamtwara Mjini tu, eti kwamba wenyewe wa Msimbati na Mtwara Vijijini kwa ujumla wako tayari gesi hiyo kupelekwa Dar es salaam, kumbe si kweli. Leo hii, wale wanaodaiwa kuwa tayari kuruhusu gesi hiyo wameteketeza gari, je wale wasio tayari kwa hilo kesho watafanya nini? Wananchi hao wamesema wako tayari kumlinda Bibi huyo usiku na mchana kwa kuhofia kurubuniwa na Serikali ili abadili simamo wake.

Serikali isidharau wananchi na wale wenye matakwa mema na nchi hii, kwani mbali na mamlaka ambayo serikali imepewa katika kusimamia rasilimali za nchi bado uhalali wa wamiliki asilia wa rasilimali hizo ambao ni wananchi hauwezi kuporwa. Wananchi wanaozungukwa rasilimali husika ndio wamiliki halali wa rasilimali hizo kabla ya Serikali na jamii zingine za nchi. Hivyo wanufaika wa kwanza wa rasilimali husika ni lazima wawe ni wale wenye uhalali wa Ki-asili na si vinginevyo.

Tuache dharau, leo gari limechomwa na kama hii hali itaendelea kuwa hivi tusishangae kuambiwa kunamtu pia kachomwa au kapoteza maisha kwasababu hizihizi zinazofanyiwa masihara na viongozi wetu. Tuweni wazalendo jamani, tutetee maendeleo ya nchi na watu wake kwa vitendo, tuache porojo.

Hassani Samli, Mtwara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. Jamani mimi story hii imeniacha mbali, huyu Bibi anayeongelewa ni nani? ilitakiwa taarifa ianzie nyuma!!

    ReplyDelete
  2. huyo bibi ndi nana na anamamlaka gani tafadhali mdau tujulishe?

    ReplyDelete
  3. Samahani jamani mtu anayeweza nielewesha vizuri kuhusu huyo Bibi, ni nani na ana mamlaka gani kuwa anaweza badilishs msimamo, cjajua huyo bibi authority yake katika eneo hilo

    ReplyDelete
  4. kuna tatizo gani kwa serikali kukaa chini pamoja na wakazi wa Mtwara,kulijadili suala hili kwa mapana na marefu,pande zote mbili zifikie makubaliano,ili mambo mengine yasonge mbele?hizi siasa za Ubabe zimepitwa na wakati!watanzania hivi sasa pamoja na umaskini na ujinga wao,wamezinduka na wanatambua haki zao.Hata wakati ule wa mwanzo wa mjadala wa kuwepo kwa Katiba mpya au La,mambo yalikuwa hivi hivi,serikali ilikuwa haipendi Katiba Mpya iandaliwe kama watanzania wengi walivyo kuwa wakipendekeza.Walivyotaka wao,basi iwe hivyo,hakuna kubadilika!Vutana ikaendelea weee mpaka hatimaye serikali ikalegeza kidogo msimamo wake.Na bado,mambo hayajafikia mwisho,bado tuna safari ndefu.Kisa?Ubabe na Ubishi wa baadhi ya viongozi wa serikali,ambao wanadhani,serikali ni mali yao,ipo mifukoni mwao! mweeeee! ipo siku,nchi itakuwa ndogo hii,nawaambieni......Bubu akijilazimisha kusema,ujue kuna jambo hapo.....kwanini ustaarabu wetu watanzania tunataka kuutia doa? wakazi wa mtwara wasikilizwe kwanza jamani!

    ReplyDelete
  5. habari hii inataja mtu anaitwa "Bibi" aliyechukuliwa na kupelekwa kusikojulikana (!?)....lakini haifafanui huyo bibi ni nani, ni mtu wa jina moja "bibi" au ni bibi kizee fulani au ni kitu gani - ni vizuri maelezo kama hayo yawekwe vizuri kuondoa maswali kwa wasomaji wapya...ni mtazamo wangu (nadhani kwa hili sijachafua hali ya hewa wala kujeruhi hisia za mtu, ahsante)

    ReplyDelete
  6. Eee bibi we tuletee maji badala ya gesi sie wajukuu zako hapa Dar ea salaam hasa wa maeneo mengi ya wilaya ya temeke na kinondoni tunaokunywa maji ya visima tangu serikali ya awamu ya kwanza,tunaoteseka kwa shida ya maji.kila uchao ndoo kichwani, vidumu mkononi kutafuta maji.wakati mwengine hua hatulali kwa kuhofu kuchelewa foleni ya maji ya kisima alfajiri.Bibi maji ndio shida yetu kubwa wajukuu zako sie.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...