Ndugu zangu,
Imekuwa
ni utamaduni wangu kutuma salamu za Mwaka Mpya kwa wanakijiji wa
Mjengwablog, marafiki zangu kwenye FB na wengine walio ndani na nje ya
mitandao ya kijamii.
Nimefanya
hivyo tangu mwaka 2006 ilipoanzishwa Mjengwablog. Na mwaka huu
naendeleza utamaduni huo. Nina mambo makubwa mawili kwenye salamu za
mwaka huu, lakini, nitaanza salamu hizi kwa kukumbushua ahadi muhimu ya
Mwana –TANU; kwamba;
” Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa manufaa ya wote”.
Ndugu zangu,
Siku kama ya leo miaka 30 iliyopita nilikuwa ndani ya garimoshi la Tazara nikielekea Dar kutokea kijijini kwetu Nyeregete.
Nikiwa
Nyeregete kwenye likizo ndefu ya kusubiri matokeo ya Kidato cha Nne,
zilinifikia taarifa kuwa nahitajika haraka Dar es salaam kwenda kufanya
maandalizi ya kuanza Kidato cha Kwanza shule ya Sekondari Tambaza.
Masomo yetu pale Tambaza yalianza Januari 13, 1983.
Siku
kama ya leo miaka 30 iliyopita nilivuka kwa kuogelea korongo la
Lihamile ili kuifikia Rujewa na hatimaye stesheni ya Tazara kule Ihanga.
Korongo hilo lilijaa maji ya mvua ya masika yaliyokuwa yakipita kwa
kasi.
Hakukuwa
na daraja. Baadae likajengwa daraja la magogo wakati wa kipindi cha
Ubunge wa Kanali Mstaafu, Edmund Mjengwa. Daraja hilo sasa limeoza.
Halipitiki. Ahadi nyingi zimetolewa kulijenga upya. Zimebaki kuwa ahadi.
Ni daraja muhimu kiuchumi na kijamii kwa watu wa Nyeregete na wengine
wengi wenye kulitumia. Ni kero kubwa kwa wananchi wa Nyeregete.
Nimeongea
na baadhi ya viongozi wa Nyeregete. Na nimewaambia, kuwa tushirikiane
kuhakikisha, kuwa mwaka 2013 daraja hizo linajengwa hata kama ni kwa
nguvu za wananchi. Tayari tumeshafanya utafiti na kuona inawezekana
likajengwa kwa kiwango cha zege na chini ya shilingi milioni 20.
Hivyo
basi, mwaka 2013 nitashirikiana na wananchi wa Nyeregete na wengine
wote watakaokuwa tayari kusaidia kuhakikisha tunapitisha harambee ya
kujenga daraja hilo. Miaka 30 baada ya mimi kuvuka Lihamile kwa kuogelea
itakuwa ni aibu kubwa kuwaona tena wananchi wa Nyeregete na wengine
wakivuka korongo hilo kwa kuogelea. Ni nini basi maana ya kwenda shule?
Ndugu zangu,
Maji ni kero kubwa kwa wananchi wengi wa Bonde la Usangu, Mbarali Mbeya.
Badala
tu ya kuilalamikia na kuisubiri Serikali iwasaidie wananchi kutatua
kero ya maji, mwaka 2013 nimeazimia nitashirikiana na wanakijiji wa
vijiji vya Magwalisi na Lihamile wilayani Mbarali ili tuweze kuchangisha
fedha za kuchimba visima vya pampu kimoja katika kila kijiji husika.
Nitashiriki
kuchangisha sehemu ya fedha zinazohitajika kugharamia visima hivyo kwa
kupanda Mlima Kilimanjaro, kitu ambacho nimependa nikifanye katika
maisha yangu lakini sijapata bahati ya kufanya.
Ndugu zangu,
Hayo ni mawili makubwa niliyotaka kuyasema kupitia salamu za mwaka mpya wa 2013.
Ni
matumaini yangu, Desemba 31, 2013 Mungu atanijalia uhai na kurudi tena
hapa kutoa tena salamu za mwaka mpya huku hayo mawili yakiwa tayari
yameshafanyiwa kazi kwa nguvu za pamoja, ikiwamo ushirikiano wenu.
Nawatakia Heri na Fanaka Za Mwaka Mpya wa 2013.
Maggid Mjengwa,
Morogoro
0788 111 765
http://mjengwablog.com
Brother Mjengwa kwanini leo blog yako haipatikani hewani?
ReplyDeleteHeri ya mwaka mpya
Brother Mjengwa kwanini leo blog yako haipatikani hewani?
ReplyDeleteHeri ya mwaka mpya