HALI ya uchaguzi wa TFF imeendelea kuwa ya sintofahamu baada ya leo Kamati ya Uchaguzi chini ya Mwenyekiti wake Deogratius Lyato kutangaza kusitisha uchaguzi huo kwa kile alichodai kuwa ni matatizo ya kikanuni.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Lyato amesema kuwa zoezi hilo limesitishwa hadi hapo atakapotangaza upya tarehe ya uchaguzi huo ambao tayari umeshaingia dosari kwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais,Richard Rukambura ambaye alienguliwa kwenye kinyang'anyiro hicho kwenda kupinga maamuzi hayo mahakamani huko Kanda ya Mwanza na kesi hiyo inatarajiwa kusomwa kwa mara ya kwanza Februari 19.
Akitangaza uamuzi wa kusimamisha uchaguzi huo Lyato alisema "Kamati ya Uchaguzi ya TFF imepitia mchakato mzima wa uchaguzi na bodi wa TFF ili kujiridhisha kuwa mchakato mzima unakidhi kikamilifu matakwa ya kanuni na katiba ya TFF,tumebaini kuwa kuna matatizo ya kikanuni ambayo yanapaswa kuzingatiwa kwanza kabla ya kuendelea na mchakato wa uchaguzi.
Akifafanua zaidi alisema "Mfano kanuni inasema mtu anayeweka pingamizi lazima aweke saini kwenye fomu yake lakini unakuta hakuweka na sisi tukalijadili hilo ni tatizo.
"Viongozi wa TFF wanatakiwa kuchaguliwa kwenye mtindo ulionyooka na sisi kama tumetilia shaka hatuwezi kushinikizwa tu kukimbilia kufanya uchaguzi wakati kuna matatizo.
"Ili uchaguzi ufanyike Februari 24 lazima kampeni zianze kesho, lakini kutokana na matatizo haya haziwezi kuanza na ndio maana nimesitisha mchakato mzima hadi hapo tutakapotangaza upya:
"Hali si njema kwa afya ya mpira watu wamefikia hatua ya kutoa lugha chafu kitu ambacho ni hatari, viongozi wa michezo lazima watambue dhamana waliyonayo, mtu mwenye dhamana kama mimi hapa ni mwenyekiti wakati wa kutoa maoni yangu natakiwa niwe makini sio kwa vile nimevaa suti ndio mwenyekiti,nakutwa Leaders Club nimevaa bukta nafanya mazoezi mimi ni mdau hilo si sawa chochote unachosema ujue kitachukuliwa kuwa ni mwenyekiti siwezi kukwepa hilo.
Kauli hiyo ya Lyato ni kama dongo kwa Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo Amos Makala ambaye alizungumzia mchakato wa uchaguzi wa TFF kama mdau wa mpira kwa kile alichoeleza kuwa ameshtushwa na kuenguliwa kwa Malinzi kwenye kinyang'anyiro na kudai kuwa kamati ya rufaa chini ya Idd Mtiginjola imenunua dharau kwa gharama ndogo.
Alisema Kamati yake imefikia uamuzi huo kwa mujibu wa kanuni ya 10(1) ambayo inasema kamati ya uchaguzi ya TFF kwa mujibu wa katiba ya TFF inatakiwa kutoa tangazo kupitia vyombo vya habari ikiwemo TV, Radio na Magazeti kwa kipindi kisichopungua siku 40 kabla ya kutangaza siku ya uchaguzi.Vigezo vya wagombea, tarehe ya kuchukua na kurudisha fomu.
Alisema pia Kanuni ya 8 (2) ambayo inasema rufaa dhidi ya maamuzi ya kamati kuhusu mgombea na utaratibu uliotumika kumpitisha rufaa hiyo itapelekwa kwenye kamati ya rufaa ya uchaguzi ikiwa ni pamoja na ada ya shilingi600,000 huku kanuni ya 12 (4) Wakati huo huo Kamati ya rufaa ya uchaguzi ilitarajiwa kukaa jana kupitia upya rufaa ya mgombea Jamali Malinzi na Hamad Yahaya ambao wameomba marejeo ya rufaa zao.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...