Na Lydia Churi- MAELEZO
Serikali imewasimamisha kazi na itawafungulia mashtaka ya kijeshi Maafisa watano wa Jeshi la Polisi nchini kutokana na tuhuma mbalimbali za ukiukaji wa maadili na taratibu za jeshi hilo.


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi (pichani kulia) amewataja waliosimamishwa kazi kuwa ni  Elias Mwita aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya, Jacob Kiango aliyekuwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya na Charles Kinyongo aliyekuwa Mkuu wa kikosi cha kutuliza Ghasia Mkoa wa Mbeya.

Dkt. Nchimbi amesema leo jijini Dar es salaam kuwa  viongozi hao wamesimamishwa kazi tangu jana kutokana na kukiuka maadili ya jeshi la Polisi nchini ambapo wanatuhumiwa kwa madai kuwa walipeleka chumvi na sukari kwenye Ofisi ya Mkemia Mkuu badala ya kilo 1.9 ya madawa ya kulevya aina ya Cocaine yaliyokamatwa na askari mkoani Mbeya mwezi Machi mwaka jana.

Waziri Nchimbi alisema vitendo hivyo vinavyofanywa na viongozi wa jeshi la Polisi vinawavunja moyo na kuwapa hofu askari wa ngazi ya chini ambao hushindwa kufanya kazi zao kwa uadilifu unaotakiwa.  

Katika hatua nyingine, aliyekuwa mkuu wa Upelelezi mkoani Kagera Peter Matagi amesimamishwa kazi na atafunguliwa mashtaka ya kijeshi kutokana na kukiuka taratibu za kazi kwa kuwabambikiza kesi zisizo na dhamana wananchi 13 wa kata ya Nyakasimbi wilaya ya Karagwe mkoa wa Kagera Kutokana na vurugu za kugombea ardhi ambazo hazikuwiana na aina ya mashtaka walioshtakiwa hali inayoonesha dalili ya uwepo wa rushwa

Waziri Nchimbi alisema wananchi hao walibambikizwa kesi ya ujambazi wa kutumia silaha ambapo walikaa mahabusu kwa muda wa miezi miwili na baadaye timu ya uchunguzi iliyoongozwa na waziri mwenyewe kugundua kuwa mashtaka waliyoshtakiwa hayakuwa sahihi hali ambayo ilisababisha Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) aliifuta kesi.

Aidha, Serikali pia imemsimamisha kazi aliyekuwa Mkuu wa Polisi wilaya ya Serengeti Paul Mng’ong’o kwa kosa la kuingia katika Hifadhi ya Mbuga za wanyama ya Serengeti na kupanga njama ya kuchimba madini aina ya dhahabu ndani ya hifadhi hiyo hali iliyosababisha kiongozi huyo kushtakiwa  kwenye mahakama ya kiraia huko Serengeti.

Wakati huo huo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi aliyekuwa anasimamia ajira katika jeshi hilo nchini Renatus Chalamila amepewa likizo ya mwezi mmoja baada ya kutajwa mara nyingi kuhusika na kuwatoza fedha vijana walioomba ajira ya jeshi la polisi ili awapatie kazi hiyo.

Alisema Chalamila amepewa likizo hiyo na mapendekezo kupelekwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama mamlaka ya nidhamu  ili Rais afanye maamuzi juu ya tuhuma zinazomkabili askari huyo.
Kufuatia hali hiyo jeshi la polisi limelazimika kuwaondoa katika mafunzo askari wanafunzi 95 waliokuwa wamejiunga na chuo cha polisi baada ya kubainika kuwa walipata fursa hiyo kwa kutoa fedha.

Waziri Nchimbi alitoa wito kuwa Serikali itawaunga mkono askari wanaofanya kazi kwa uadilifu ila watakaoenda kinyume na maadili na taratibu za jeshi la polisi serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafukuza kazi.

Hatua zilizochukuliwa na Serikali kwa viongozi wa jeshi la polisi ni sehemu ya makubaliano ya Maafisa waandamizi wa jeshi la Polisi nchini waliokutana hivi karibuni mjini Dodoma kulinda maadili ya jeshi hilo na kukabiliana na vitendo vyote vinavyolichafua jeshi hilo kwa jamii ili  kutatua kero za wananchi na kuzingatia utawala bora. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. mbona wapo wengi sana kama hao wanaokamata mizigo mbali mbali na badae wanapotelea mbalini na mizigo na kutafuta mauzo na badae kuneemeka na mihela

    hatua nzuri sana hongereni sana wahusika kwa kupambana na matukio kama hayo nina uhakika ipo siku ya siku mambo kama hayo yatapotelea mbalini tutabaki kuwa watumishi halali wa serikali.

    ReplyDelete
  2. Uadilifu ukiwepo hakutawepo na msuguano kati ya polisi na wananchi. Tatizo liko kwa waliopewa dhamana ya kulinda raia kwenda kinyume na sheria.

    Mfano polisi anaweza kumpigisha kichura raia ambaye ametuhumiwa kosa. Sasa unashindwa kuelewa, ivi kichura ndiyo adhabu anayostahiki huyo mtuhumiwa??? Sasa kama ndiyo adhabu yenyewe sasa kuna haja gani ya kumpeleka mahakamani???

    Utaratibu bora ni huu: kama kuna tuhuma kwa raia kuhusiana na jambo fulani, apelekewe barua ili aende polisi. Na kama italazimu polisi kwenda kumkamata, waende tu hapo mahali na kumwambia twende kituo cha polisi. Wasimpige na wala wasimfunge pingu.

    Kama akikataa; basi watumie nguvu zinazositahiki. Na akifika mahala husika; kulingana na kosa lenyewe apewe dhamana haraka inavyowezekana; tatizo hapa ni kuwa anatuhumiwa tu; haijathibiti.

    Tusije tukamkosea mtu kwa kumweka ndani muda mrefu halafu baadae akaonekana hana kosa. Hapa tutakuwa hatujamtendea haki raia; na kesho mbele ya haki tutakuja kujibu.

    Njia nyingine ya rahisi ni kwamba kama wanadhamira ya kumweka ndani basi wawe na uhakika kwamba kosa ametenda na kinachofanyika ni kumpeleka mtuhumiwa mahakamani moja kwa moja; bila kuchelewa.

    Mahakamani hakimu anaishughulikia kesi siku hiyo hiyo na kutoa hukumu; kwa kuwa kila kitu kilishafuatiliwa hata kabla ya mtuhumiwa hajakamatwa.

    Kwa mtindo huo hatutawadhalilisha wananchi wa Tanzania na watakuwa wanawapenda polisi sana tena sana kwa imani kwamba wanafanya hasa lile jukumu walilokabidhiwa na wananchi wa Tanzania.

    Mwisho nawapongeza viongozi wetu (Dr.Emmanuel Nchimbi na IGP Said Mwema ) kwa yote; cha kukumbuka tu ni kwamba changamoto bado ziko nyingi.

    Kila la kheri.

    ReplyDelete
  3. Asante Mheshimiwa Dkt. Nchimbi.

    ReplyDelete
  4. Polisi yetu inahitaji marekebisho ya kutosha badala kugusa gusa tu tatizo. UKWELI WA MAMBO JESHI LETU LA POLISI LIMEKOSA UELEKEO.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...