Na Frank Geofray wa Jeshi la Polisi.
Wakurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI’s) kutoka Umoja wa Wakuu wa Polisi Kusini mwa Afrika (SARPCCO) kesho jumatatu wanatarajia kuanza mkutano wa siku mbili jijini Dar Es Salaam chini ya uenyekiti wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wa Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari, Msemaji wa Jeshi la Polisi Advera Senso amesema Mkutano huo wa siku mbili utafunguliwa na Mwenyekiti wa sasa wa SARPCCO ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania IGP Said Mwema.
Amesema katika mkutano huo mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo jinsi ya kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa kufanya operesheni za pamoja na ushirikiano baina ya SARPCCO na umoja wa Wakuu wa Polisi wa nchi za Afrika Mashariki (EAPCCO).
Advera amesema mkutano huo pia utajadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na wakuu wa Polisi wa SARPCCO katika mkutano uliofanyika Zanzibar mwezi Septemba mwaka 2012.
Aidha amesema Kamati Tendaji za SARPCCO ambazo zinajumuisha wajumbe kutoka nchi wanachama katika nyanja za Sheria, Mafunzo na kamati tendaji inayoshugulikia mambo ya wanawake na jinsia zitajadiliana ili kutoka na maazimio ambayo yatapelekwa katika mkutano wa Wakuu wa Polisi wa SARPCCO mwezi Mei mwaka huu.
Tayari wajumbe wa mkutano huo wameanza kuwasili hapa jijini Dar Es Salaam kuhudhuria mkutano huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...