Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali Saidi Mwema kuomboleza kifo cha askari WP2494 Koplo Elikiza ambaye amepoteza maisha kwa kugongwa na gari leo, Jumatatu, Machi 18, 2013 saa saba mchana katika eneo la Bamaga, Dar Es Salaam.
WP 2494 Koplo Elikiza amegongwa wakati alipokuwa anamsimamisha dereva mmoja aliyejaribu kujiunga, kinyume cha taratibu, mwishoni mwa msafara rasmi wa magari ya Mheshimiwa Rais Kikwete, alipokataa kusimama baada ya kupewa amri ya kusimama na askari huyo,  na akamgonga.
Amesema Rais Kikwete: “Nimepokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Koplo Elikiza ambaye nimejulishwa kuwa aligongwa na gari leo  akiwa kazini katika eneo la Bamaga, Dar Es Salaam, wakati alipokuwa anaongoza msafara rasmi.”
“Ni jambo la kusikitisha na kuhuzunisha kuwa Koplo Elikiza amepoteza maisha yake akiwa kazini kwenye utumishi wa jeshi lake na nchi yake, na wakati taifa letu bado linaendelea kuhitaji sana nguvukazi yake. Tutaendelea kumkumbuka kwa uaminifu wake kwa Jeshi la Polisi na kwa taifa lake la Tanzania,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kifo chake siyo tu kwamba ni pigo kwa nchi yetu, bali ni pigo kwa Jeshi la Polisi nchini na ni pigo hasa kwa familia yake ambayo bado ilikuwa inahitaji mapenzi, uangalizi na usimamizi wa mama.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Nakutumia wewe IGP salamu zangu za rambirami kuomboleza kifo hiki. Aidha, kupitia kwako nawatumia makamanda na askari wote wa Jeshi la Polisi Tanzania kwa kuondokewa na mwenzao. Vile vile, naomba kupitia kwako unifikishie salamu za pole ya moyo wangu kwa familia ya marehemu. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huuo mkubwa na naelewa machungu yao.”

“Aidha, napenda wajue kuwa naungana nao katika kumwombea marehemu, na pia kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, ailaze pema poponi roho ya Marehemu Koplo Elikiza. Amina.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Enzi za Mwalimu huyo dreva alikua hana tofauti na MHAINI.Kosa hapo si kumgonga trafiki bali kosa kubwa sana ni kuingilia msafara halali wa Rais tena kwa kukiuka kwa jeuri kabisa amri halali ya askari wa barabarani na hata kudiriki kumgonga na kumuua?...Hivi siku hizi mambo yamekua rahisi kiasi hicho?Hatuheshimu hata mamlaka?...Huyo anastahili kunyongwa mpaka afe.

    ReplyDelete
  2. Nimesikitishwa sana na kifo cha askari huyo, ambae amefariki akiwa kazini. Ukiukwaji wa sheria za barabarani umekwenda mbali zaidi, kuanzia kusimamishwa na askari ukagoma, kuingilia msafara wa raisi, na mbaya zaidi kupoteza maisha ya mwanausalama barabarani

    ReplyDelete
  3. Mdau wa kwanza, Enzi za mwalimu hata mamlaka zilikuwa zinawaheshimu wananchi hivyo kulikuwa na kitu kuheshimiana na ndio maana adhabu ikitolewa ilikuwa inakubalika

    ReplyDelete
  4. Tusimuhukumu Mtuhumiwa mpaka mahkama imtie hatiani. Huwezijuwa nini kilitokea kwa dereva.

    Mungu aiweke roho ya WP2494 panapostahuki.

    ReplyDelete
  5. Mungu amrehemu, apumzike kwa amani

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...