Mkutano wa  kumi na nane wa mwaka kwa Wakuu wa Majeshi ya Polisi kutoka nchi za  Kusini mwa Afrika (SARPCCO) unatarajia kufanyika  Mei 15, 2013   jijini Dar es Salaam  chini ya mwenyekiti wa umoja huo kwa mwaka 2012/2013 Inspekta Jenerali wa Polisi Tanzania, IGP Said Mwema.
Mkutano huo utatanguliwa na Mkutano wa  kamati tendaji za SARPCCO ambao  utafunguliwa na IGP Said Mwema  Mei 13, 2013 na kufuatiwa na Mkutano wa Wakuu wa Polisi wa nchi hizo utakaofunguliwa Mei 15, 2013 na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Dkt Emmanuel Nchimbi.
Katika mkutano huo mambo mbalimbali yatajadiliwa ikiwemo jinsi ya kukabiliana na uhalifu unaovuka mipaka kwa kufanya Operesheni za pamoja na ushirikiano baina ya SARPCCO na Umoja wa Wakuu wa Polisi wa nchi za Afrika Mashariki (EAPCCO).
Vilevile, mkutano huo utajadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa na Wakuu wa Upelelezi wa SARPCCO pamoja na kamati tendaji za sheria, Mafunzo na kamati tendaji ya Jinsia na watoto katika mkutano wao uliofanyika mwezi Machi jijini Dar es Salaam.
Aidha suala la michezo baina ya Majeshi ya Polisi kwa nchi wanachama nalo linatarajiwa kujadiliwa katika mkutano huo.
SARPCCO iliundwa mwaka 1995 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa Majeshi ya Polisi kwa nchi za Kusini mwa Afrika katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu. Mpaka hivi sasa umoja huo unaundwa na Nchi kumi na nne ambazo ni Tanzania, Angola, Botswana, Malawi, Lesoto, Mauritius, Congo, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Zambia, Zimbabwe, Swaziland na Madagascar.
Imetolewa na:-
Advera Senso-SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 08, 2013

    Wewe afisa wa polisi uliyandika, rekebisha Kiswahili chako. Siyo "kamati tendaji" bali ni "Kamati ya Utendaji."
    Msituharibie Kiswahili chetu na kifo chenu cha elimu.

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 09, 2013

    Anonymous hapo juu unapaswa kuwa mstaarabu , tazama toa kwanza boriti kwenye jicho lako ndipo utaona kibanzi kwenye jicho la mwenzako.Wewe unaona umeandika kwa usahihi neno " uliyandika"? Pole kwa kutazama makosa ya wenzako ukidhania kuwa wajua kumbe nawe watanga na jua.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...