Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya tukio la leo, Jumapili, Mei 5, 2013 la mlipuko kwenye Kanisa Katoliki la Mt. Joseph Mfanyakazi la Olasiti Jijini Arusha.  Tukio hilo la kigaidi limesababisha mtu mmoja kupoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa.  

Rais Kikwete analaani vikali shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu katili, waovu na wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa Tanzania na watu wake. 

Rais Kikwete ameagiza vyombo vya usalama nchini kumsaka mtu au watu waliohusika na kitendo hicho kiovu na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.  Vile vile Rais Kikwete amewataka wananchi wote kuwa watulivu wakati Serikali na vyombo vyake inaendelea kufuatilia tukio hili.  
"Tutawasaka popote walipo na kupambana nao bila huruma.  Aidha, tutakabiliana na aina yoyote ya uhalifu nchini iwe ni ugaidi au aina yoyote ya uhalifu wa namna hiyo au wa namna nyingine, uwe na chimbuko lake ndani ya nchi ama nje ya nchi yetu.  
"Kamwe hatutakubali kuwaacha wavuruge amani na usalama wa Tanzania na watu wake" amesema Rais ambaye anaamini kuwa Serikali, kwa msaada na ushirikiano wa wananchi, watu hao watapatikana na kuadabishwa ipasavyo.
 Aidha, Rais Kikwete anatoa rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wafiwa na wale wote ambao wamejeruhiwa katika tukio hilo. Anaungana nao katika machungu na msiba. Rais pia anawaombea wote walioumia katika tukio hili wapate nafuu ya haraka na waendelee na shughuli zao za ujenzi wa taifa.

Rais Kikwete vilevile anatoa pole nyingi kwa viongozi na waumini wa Kanisa Katoliki kwa tukio hili la kusikitisha na kuvurugika kwa ibada na shughuli yao muhimu ya uzinduzi wa Kanisa lao.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
 5 Mei, 2013

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 06, 2013

    toka lini tukawa na matukio kama haya? na chanzo chake nini na wakina nani? watu bwana hatuko mazuzu zuzu eti magaidi mnawazimu wadanganyika tumeshamka bwana siyo wote watanganyika ni wadanganyika

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...