Kaka Michuzi,
Kwanza kabisa naomba nikupongeze kwa kutupatia habari kwa wakati, hongera sana. Pili naomba kaka Michuzi unisaidie kufikisha kilio chetu sisi wakazi wa Kata ya Kunduchi, Mtaa wa Pwani – Tegeta kwa Mamlaka husika DAWASCO.
Mnamo tarehe 26/4/2013 baada ya mvua kubwa kunyesha katika jiji hili la Dar es Salaam baadhi ya sehemu zilipata mafuriko ikiwa ni pamoja eneo tulipo Mchakani jirani na Shule ya Education Plus mkabala na Baa ya Nyamachabes.
Diwani alifika eneo la tukio baada ya kupata taarifa ya mafuriko hayo, alichukua hatua ya kuchimba mtaro ili maji hayo yapate njia kuelekea baharini kabla ya kufanya hivyo alifahamishwa kuwa eneo hilo analotaka kuchimba mtaro huo kuna bomba la maji safi lakini aliendelea na maamuzi yake, kitendo hicho kilipelekea kukata mabomba ya maji safi ya DAWASCO na maji kumwagika na kupotea kwa wingi. Baada ya DAWASCO kupata taarifa hiyo walifika na kufunga bomba kubwa eneo hilo, hivyo kupelekea wakazi wa eneo husika kukosa maji safi ya matumizi ya nyumbani tangu tarehe 26/4/2013 hadi leo hii ninapotoa kero hii.
Aidha mpaka sasa hakuna juhudi yoyote inayofanywa kurejesha maji safi, wakazi tunaendelea kutaabika na adha ya kukosa maji safi. Tunaomba Mamlaka husika DAWASCO iweze kusikia kilio chetu cha kuturejeshea huduma ya maji safi kwa matumizi ya nyumbani. Wakazi tulioathirika tuko tayari kutumia gharama zetu wenyewe kuunganisha bomba zetu kurejesha katika hali ya awali.
Asante!
Mdau Kunduchi
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...