Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imekutana jana tarehe 10/06/2013 chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Dr. Jakaya Mrisho Kikwete. Kikao hicho kilikuwa cha siku moja na maalum kwa ajili ya kupokea rasimu ya katiba mpya.

Kamati Kuu inaipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini kwa kazi nzuri na kukamilisha kazi kwa wakati.

Kamati Kuu imepokea rasimu hiyo na kuelekeza kuwa; Kwa kuwa rasimu hii ni ya kwanza ambayo inapelekwa kujadiliwa tena kwa wananchi kupitia mabaraza mbalimbali ya katiba baada ya kuisha kwa hatua ya kutoa maoni.

Kamati Kuu imekiagiza Chama kijipange kuijadili rasimu hiyo ndani ya Chama kama baraza la kitaasisi la katiba na kuwataka wanachama na wapenzi wa CCM wajitokeze kwa wingi na kushiriki kwenye mabaraza haya.

Ushiriki huu wa CCM baada ya kupokea rasimu umekusudia kushirikisha wanachama wetu kwenye ngazi ya tawi, wilaya, mkoa na Taifa.

Lakini pia Jumuiya za CCM zimekusudia kushiriki kama mabaraza ya Katiba na hivyo kuongeza ushiriki wa wanachama na wapenzi wa CCM katika mchakato huu.

CCM kama baraza la katiba la kitaasisi litaipitia rasimu iliyowasilishwa kifungu kwa kifungu na kwa kuzingatia maoni ya CCM yaliyotolewa mwanzoni kabisa mwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba, wanachama wetu watashiriki kutoa maoni yao.

Pamoja na kazi nzuri ya Tume ya Mabadiliko ya katiba, Kamati Kuu inaiomba Tume hiyo kueleza vizuri mchakato mzima kutoka rasimu ya kwanza mpaka rasimu ya mwisho ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi juu ya mchakato mzima hasa baada ya rasimu ya kwanza kutoka.

Kamati Kuu inawasihi Watanzania kushiriki tena kwenye kutoa maoni kupitia mabaraza ya katiba kwa rasimu ya kwanza, bunge maalum la katiba kwa rasimu ya pili na kupitia kura ya maoni kwa rasimu ya tatu, kwa amani,utulivu na kuvumiliana ili mwisho wa siku tupate Katiba nzuri ya nchi yetu kwa masilahi ya Watanzania walio wengi.

Nape Moses Nnauye
CCM Secretary for Ideology & Publicity

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. SeraphinaJune 11, 2013

    Nadhani ni vizuri kwamba watu wanapotoa maoni yao wawe na mtazamo mpana na madhumuni(objectives) za Katiba.Ni vizuri sana watu kutoa maoni kupitia taasisi mbalimbali,lakini pia ni vizuri viongozi wa vyama wasiwe na influence kuhusu nini wananchi waseme.Hii ni kwa sababu katiba ya nchi si ya chama, na Katiba itatakiwa kuendelea kuwa na maana na kumlinda mwananchi whether yupo katika chama fulani au taasis fulani au la.Kwa hiyo mtu asitoe maoni kwa mfano eti kwa kuwa leo yupo kwenye upande fulani wa muungano,kwenye imani fulani ya kidini,kwenye itikadi fulani ya siasa, kwenye taasisi ama chombo fulani cha serikali kwa kuwa hayo yote yanaweza kubadilika lakini katiba itabaki na itakuwa juu ya sheria zote.Nashauri watu wawe objective,waachwe waiangalie Katiba objectively,waangalie maslahi ya sasa kwao na kwa wengine na vizazi vijavyo.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...